TAMKO LA BARAZA KUU LA CHADEMA KUHUSU UCHAGUZI MKUU 2005
Sisi, wajumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA tuliokutana leo Mei Mosi mwaka 2006 katika Ukumbi
wa Haidery Plaza, tumepokea ripoti ya uchaguzi mkuu 2005 ambayo
inajumuisha taarifa za uchaguzi toka kwa ngazi mbalimbali za chama kote
nchini, tumetathmini na kujadili kwa kina uchaguzi husika na kwa pamoja
tumeazimia kutoa tamko hili linaolotoa msimamo wa CHADEMA kuhusu mapungufu,
mafanikio, mapendekezo na mwelekeo kuhusu uchaguzi mkuu 2005. Tunaamini
tamko hili litakuwa changamoto kwa wanaCHADEMA, mamlaka zinazohusika,
wadau mbalimbali na Watanzania kwa ujumla kuboresha mchakato
wa demokrasia nchini hususan katika chaguzi zinazofuata. Aidha tunawashukuru
watanzania wote waliotuunga mkono kwa hali na mali na tunawapongeza
walioukuwa wagombea wetu wote katika uchaguzi mkuu pamoja na viongozi
wa CHADEMA ngazi mbalimbali kwa jitihada walizozifanya katika uchaguzi
mkuu 2005.
MAPUNGUFU
Uchaguzi Mkuu 2005 HAUKUWA
HURU NA HAKI
kutokana na mapungufu yafuatayo ya msingi:
- Ahtari za Uchaguzi wa ngazi za
Mtaa na Vijiji wa Mwaka 2004: Mfumo wa utawala wa
nchi yetu katika maeneo mengi unaanzia katika vijiji na
mitaa ambayo ina mamlaka kadhaa ya kiutendaji na kimaamuzi.
Uchaguzi wa ngazi hii hufanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi
mkuu hivyo hutumika kama msingi wa vyama vya siasa katika
uchaguzi mkuu na kuandaa mfumo wa chama kutawala kuanzia
ngazi za chini. Uchaguzi huu kwa mwaka 2004 haukuwa huru
na haki kwa mapungufu mengi mathalani upigaji kura kutokuwa
wa siri, fujo katika vituo, matayarisho hafifu, kuingiliwa
na maafisa watendaji wa kata na vijiji ambao walifikia hata
hatua ya kuwatisha wananchi na kutotoa taarifa za muhimu
za uchaguzi, kukosekana kwa daftari la wapiga kura na uchaguzi
kusimamiwa na chombo kisicho huru cha kiserikali moja kwa
moja (Wizara ya TAMISEMI). Kutokana na mapungufu haya CCM
ilishinda kwa asilimia 96 na kupata mtaji haramu wa kisiasa
ambao ilianza nao kama hujuma katika uchaguzi mkuu 2005
na kufanya uwanja wa ushindani wa kisiasa usiwe sawa.
- Mapungufu katika Uandikishaji: Vituo
vya kujiandikisha vilikuwa mbali na hivyo baadhi ya watu kushindwa
kuandikishwa. Pia wananchi wa maeneo mapana waliandikishwa katika eneo
moja na hivyo kufanya utaratibu wa kugawa vituo na wananchi kufahamu vituo
vyao kuwa mgumu. Ushiriki wa vyama vya siasa katika kuhakikisha kuwa mawakala
wa vyama wanakuwepo siku zote za uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura (DKWK) ulikuwa mdogo. Pia vifaa vilikosekana katika baadhi
ya maeneo kabla ya siku ya mwisho ya uandikishaji na hivyo wengine kukosa
fursa ya kuandikishwa. Zoezi la kuhakiki daftari nalo lilikuwa duni. Vyama
vilipewa DKWK yenye orodha ya watu milioni 16 siku chache kabla ya kwenda kupiga kura na taratibu
hazikutoa fursa ya wapinzani kuhakiki. Hivyo watu mbalimbali wengi wao
wakiwa wanachama wa upinzani walinyimwa kuandikishwa na wengine waliofamika
kuwa ni wana CCM hata
wasio na sifa waliandikishwa hasa Zanzibar.
- Wananchi hususan Wanachama wa Upinzani kunyimwa
ama kuogopeshwa kwenda kupiga kura:
Palikuwa na utaratibu wa majina kubandikwa nje ya vituo ambapo
katika maeneo mbalimbali baadhi ya wananchi wengi wao wakiwa
ni wanachama wa vyama vya upinzani walizuiwa kupiga kura pamoja
na kuwa na vitambulisho vya kujiandikisha kwenye DKWK - ama kwa
kukosa majina yao nje ya vituo au taarifa zao kuwa na mapungufu
au kutokuwepo kabisa katika daftari. Ishara zinaonyesha kuwa
huu ulikuwa ni mkakati rasmi kwa kuwa siku kadhaa kabla
ya uchaguzi watendaji wa chama tawala hususan wajumbe wa nyumba
kumi walipita na kuandikisha namba za wapiga kura katika maeneo
yao. Kwa kuwa wananchi wengi walikuwa na elimu finyu ya uraia na kwamba katika
baadhi ya maeneo wajumbe hawa wanasikilizwa sana na/au hata kuogopwa, wapiga
kura wengi waliorodheshwa na hata wengine kutishwa kuwa kura zao zitajulikana
na hivyo wasipoipigia kura CCM watashughulikiwa. Vitisho hivi
vilipata nguvu kutokana na utaratibu wa kuchukuliwa namba za shahada za wapiga
kura na wasimamizi wa vituo wakati wa kupiga kura. Hii ilifanya uchaguzi
usiwe huru.