TAMKO LA BARAZA KUU LA CHADEMA KUHUSU UCHAGUZI MKUU 2005
- Takrima na Rushwa wakati
wa Uchaguzi: Hoja ya kupigia kelele rushwa wakati
wa uchaguzi ikiwemo takrima ilijitokeza kabla ya uchaguzi ikiongozwa na
wanasiasa wa upinzani na viongozi wa dini. Hata hivyo hii
haikuondoa vitendo vya rushwa kujitokeza wakati wa kampeni.
Wakati huohuo dhana ilijengeka miongoni mwa raia kwamba
wakati wa uchaguzi ndio wasaa pekee wa kupata ‘chochote’ toka
kwa wagombea hususan baada ya sheria kuruhusu takrima.
Kwa upande mwingine takrima ilichukua nafasi kubwa katika
uchaguzi ikiwemo kusambazwa kwa hali ya juu kwa khanga,
fulana nk. Vitendo hivi vilielekea kuathiri uamuzi wa wapiga
kura. Hii ilikuwa ni mkakati rasmi kwa kuwa sheria ya kuruhusu
takrima mnamo mwaka 2002 kama wa kuelekea katika uchaguzi
wa 2005 kwa upande mmoja na kwa upande mwingine wabunge
walipewa mamilioni ya fedha kama kiinua mgongo mwezi wa
saba wakati mishahara na posho zao viliendelea kutolewa
hata baada ya bunge kuvunjwa. Ni jambo linaloacha maswali
mengi kiinua mgongo kutolewa kabla ya kukoma utumishi wao.
- Matumizi Makubwa ya Rasilimali wakati wa Kampeni
hususan na Chama tawala: Kutokuwepo
kwa sheria na utaratibu unaodhibiti matumizi ya raslimali wakati
wa uchaguzi ulifanya pawe na utofauti mkubwa wa raslimali
baina ya chama tawala ambacho kilikuwa kinatumia vyombo vya
dola kutafuta raslimali na vyama vya upinzani kwa upande
mwingine ambavyo vilikuwa vinadhibitiwa na dola kukusanya
raslimali. Palikuwa na utofauti mkubwa wa uwingi wa matumizi ya raslimali
hususan fedha baina ya wagombea hasa wa chama tawala kwa upande mmoja
na wa upinzani kwa upande mwingine. Wakati vyama vikubwa vya upinzani
vimetumia mamilioni kadhaa kwenye uchaguzi CCM kwa upande wake imetumia
mabilioni kadhaa. Utofauti ulikuwa bayana hata katika zana za kampeni
ambazo zilitumika. Hii ilitofautisha uwezo wa kuwafikia wananchi kufikisha
ujumbe kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kujenga dhana kwa baadhi
ya wapiga kura kuwa ‘mwenye
uwezo wa raslimali ndiye mwenye uwezo wa kuleta maendeleo
baada ya kuchaguliwa’ na
hivyo kuathiri uamuzi wa nani wampigie kura. Vipo baadhi ya
vyama na wagombea ambao walishindwa kabisa kufanya kampeni
za kuonekana kutokana na ukata wa raslimali. Pia uwingi wa
raslimali ambazo zilitumiwa na chama tawala unaacha maswali
kuhusu vyanzo vya raslimali husika, aidha wafanyabiashara wakubwa, baadhi
ya taasisi za umma na vyanzo vingine visivyofahamika na kutojulikana
uhalali wake vilitumika.
- Mapungufu ya Tume katika Kusimamia Uchaguzi: Vyama
vya siasa viliendelea kudai tume huru ya uchaguzi wakati wa
marekebisho ya 14 ya katiba yaliyofanyika karibu na uchaguzi
mkuu. Hata hivyo suala la muundo wa tume huru ya uchaguzi halikujadiliwa
wala kuingizwa kama sehemu ya marekebisho hayo. Matokeo yake maandalizi
ya uchaguzi yalifanywa na tume ile ile ambayo ilisemwa kipindi chote kwamba
haiko huru. Malalamiko yametolewa baadhi ya maeneo hususan yale yaliyokuwa
na upinzani mkali kwamba vyama havikushirikishwa ipasavyo na watendaji
wa tume ya taifa ya uchaguzi ngazi ya wilaya, majimbo na kata. Wakati wa
kampeni watendaji hawa wameonekana kuegemea chama tawala. Hali
hii iliendelea katika maeneo mengi hata katika hatua za kuhesabu kura,
kujumlisha kura na kutangaza matokeo hususan katika ngazi za majimbo. Katika
mfumo wa tume hakuna utenganisho kati ya usimamizi na utekelezaji katika
muundo wa tume ngazi za chini ya makao makuu ya tume. Uteuzi wa watendaji
wa chini ulifanywa na wasimamizi wa uchaguzi ambao ni watekelezaji (ambao
walikuwa ni watumishi wa serikali) badala ya chombo huru cha kusimamia
uchaguzi hivyo walitumiwa na dola kupika ama kuchezea matokeo.