Pingamizi dhidi ya Uteuzi wa Mgombea Ubunge
Wanaoruhusiwa kutoa pingamizi
- Mgombea yeyote wa Jimbo la Mgombea anayepingwa
- Mkurugenzi wa Uchaguzi
- Msimamizi wa Uchaguzi
Mtu mwingine yeyote haruhusiwi
Muda wa kutoa pingamizi
Baada ya saa kumi (10.00) jioni ya siku ya uteuzi, mpaka saa kumi (10.00) jioni ya siku inayofuata
Sababu za pingamizi
Sababu ya pingamizi inaweza kuwa yoyote kati ya zifuatazo:
- Maelezo yaliyopo katika fomu ya uteuzi hayatoshi kumtambulisha mgombea;
- Fomu ya uteuzi haitimizi au haikuwasilishwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Sheria;
- Kutokana na maelezo yaliyoandikwa katika Fomu ya uteuzi ni dhahiri kwamba Mgombea Uchaguzi hana sifa zinazotakiwa;
- Uthibitisho wa Msimamizi wa Uchaguzi unaopaswa kutolewa haukutolewa;
- Mgombea hana sifa zote zinazohitajika;
- Hakuna picha ya mgombea;
- Hakuna uthibitisho kuwa mgombea amelipa dhamana ya shilingi Elfu hamsini (50,000/=)
Utaratibu wa Msimamizi wa Uchaguzi Kutoa Pingamizi
Kwa mujibu wa kifungu cha 40(5) cha Sheria ya Uchaguzi namba 1/85 endapo Msimamizi wa Uchaguzi atakuwa na pingamizi dhidi
ya mgombea, ataweka pingamizi na kumwarifu Mgombea kwa maandishi kabla ya kutoa uamuzi wake. Kama mgombea ana maelezo
atayawasilisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi. Baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kutoa uamuzi atawasilisha uamuzi wake Tume
ya Taifa ya Uchaguzi akiambatisha maelezo ya mgombea.
Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi
Kabla ya kutoa uamuzi juu ya pingamizi, Msimamizi wa Uchaguzi atamjulisha mgombea nayepingwa ili aweze kuitolea maelezo
kama atakuwa nayo. Baada ya kupata taarifa za pande zote, Msimamizi wa Uchaguzi anaweza kuendelea kutoa uamuzi wake.
Hata kama anayepingwa hatatoa majibu, Msimamizi wa Uchaguzi anaweza kutoa uamuzi wake.
Rufaa dhidi ya pingamizi
- Msimamizi wa Uchaguzi atamweleza aliyetoa pingamizi, kukata rufaa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi endapo hakuridhika
na uamuzi wa Msimamimzi wa Uchaguzi katika muda wa saa 48 tangu kutolewa kwa uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi. Rufaa
itawasilishwa kwa kutumia Fomu namba 12.
- Msimamizi wa uchaguzi atapokea rufani hizo na kuziwasilisha Tume pamoja na maelezo yake.