lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner
»Kwaheri Chacha
»Wasifu wa Marehemu
»Habari Mpya
»Matamko ya Chama
»Makala mbalimbali
»Uchaguzi wa Viongozi
»Uchaguzi Kiteto
»Bajeti ya Upinzani
»Ushirikiano Wapinzani
»Orodha ya Mafisadi
»CCM wezi wa Kura

Taarifa kwa Umma juu ya Hali tete nchini Zimbabwe

Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kujitoa kwa aliyekuwa Mgombea urais wa chama cha MDC huko nchini Zimbabwe kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kutokana na kuumizwa na hata kuuwawa kwa wanachama na wafuasi wa chama chake cha MDC ambao wanafikia zaidi ya 75 mpaka sasa.

Kutokana na hali ilivyo tete hivi sasa na jinsi tukio hili lilivyojitokeza muda mchache kabla ya uchaguzi husika kufanyika nchini humo (ulikua umepangwa 27/06/2008), limeadhiri mwenendo mzima wa mambo na usalama wa wananchi wote wa Zimbabwe.

Tunalaani matukio haya ya mauaji pamoja na hali ya kuhatarisha maisha ya wananchi wa Zimbabwe, na kauli tata ambazo mara kwa mara zimekuwa zikitolewa na viongozi wa Zimbabwe na haswa Rais Mugabe.

Tunaitaka serikali ya Tanzania ichukue hatua za haraka na za dharura ili kuweza kurudisha hali ya mambo nchini humo na haswa ikizingatiwa kuwa Zimbabwe ni marafiki zetu wa muda mrefu, hivyo kitendo cha nchi yetu kuendelea kukaa kimya sio cha afya hata kidogo kwa mustakabali wa Demokrasia Barani Afrika.

Tunaitaka serikali ya Zimbabwe ihakikishe kuwa uchaguzi ujao unakuwa huru na haki ,na tunamtaka pia Rais Mugabe atoe kauli hadharani kuwa atayakubali matokeo ya kura hata kama atashindwa na mpinzani wake kwani huko ndio kukomaa Kidemokrasia .

Tunautaka Umoja wa Afrika na Nchi za Kidemokrasia Afrika kuingilia kati suala hili kwani linahatarisha maisha ya Binadamu na Ustawi wa Zimbabwe kwa ujumla wake, na kama mfano huu ukiendelea kuachwa na kukomaa hili litakuwa ni somo baya kwa viongozi wa kiafrika waliopo madarakani kukataa kuheshimu matakwa ya Kidemokrasia.

Tunawataka wananchi wa Tanzania kwa ujumla wetu tushikamane na wananchi wa Zimbabwe na kuitaka serikali kuchukua hatua bila kujali Itikadi ya Vyama vyetu kwani bila kufanya hivyo hatakuwepo wa kututetea siku hali ikiwa hivyo hapa kwetu.

Tushikamane wote kuhakikisha kuwa Demokrasia inakuwa nchini mwetu na Barani Afrika kwa ujumla wake. Na tukumbuke kuwa wanaoteseka ni watoto na wakina mama pamoja na wazee kutokana na hali hii ya hatari ambayo imewakumba wananchi wa Zimbabwe.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete hana budi kuchukua hatua za haraka ili kunusuru hali ya maisha ya wananchi wa Zimbabwe na kuhakikisha kuwa anaokoa maisha ya wananchi masikini ambao maisha yao yanaangamia kila kukicha.

Tunawapa pole ndugu zetu wapigania Demokrasia Nchini Zimbabwe chama cha MDC na Kiongozi wao. Tunawapa moyo kwa kuendelea na mapambano mpaka hapo Demokrasia ya kweli itakapopatikana huko Zimbabwe.

Hatuwezi kukaa na kusema Tanzania ni nchi ya amani ilhali kuna waafrika wenzetu wanaendelea kuawa ndani ya ardhi ya Afrika tena na waafrika wenzetu. Kama Tanzania ilivyohakikisha uhuru kwa Zimbabwe unapatikana vivo hivyo tutaishinikiza serikali ya Tanzania kuhakikisha Demokrasia na Haki za Binaadamu zinalindwa nchini Zimbabwe.

Wakati huo huo tumeshashangazwa na kauli ya Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuanza kufikiria hatua za kijeshi wakati huu badala ya kuweka mkazo katika kuunganisha nguvu za Umoja wa Afrika na wapendademokrasia wote katika bara hili kushikiza kwa njia zingine kupatikana kwa ufumbuzi wa tatizo la Zimbambwe. Ni vyema kabla ya kuanza kutoa ‘kauli za kijeshi’, Rais Kikwete angetumia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuchukua hatua za vitendo za kufanikisha maazimio ya haraka ya Umoja huo katika kutafuta suluhisho za mgogoro wa Zimbabwe.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Imetolewa na;

Freeman Mbowe
Mwenyekiti CHADEMA Taifa
25/06/2008

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl