Tamko la Uchaguzi wa Kiteto
V. Ushiriki wa TAKUKURU katika Uchaguzi
Mduara wa ufisadi katika Taifa hili unaanza kwa namna viongozi wanavyopatikana. CHADEMA tulidhani kuwa TAKUKURU walikuja Kiteto ili kukabili matendo ya rushwa lakini kilichotokea nii TAKUKURU kushangaa vitendo vya rushwa vikifanywa kwenye mikutano ya hadhara bila kuchukua hatua, na hata walipofikishiwa malalamiko rasmi bado TAKUKURU iliogopa kuchukua hatua hata kwa kusema chochote mpaka sasa. Baadhi ya matukio ya rushwa yaliyofanywa hadharani ni pamoja na;
- Katika kata ya Kijungu Mkuu wa mkoa wa Iringa Hajjat Amina Said Mrisho alitoa mabati 30, mifuko ya simenti wakati wa mkutano wa hadhara wa CCM mbele ya Polisi na TAKUKURU lakini hawajachukua yoyote mpaka sasa.
- Katika kata ya Matui alikuwepo Waziri wa Viwanda na biashara Mary Nagu na Lusinde Hawakufanya mikutano yoyote. Kilichokuwa kikifanyika ni kununua shahada za kura. Polisi na TAKUKURU walielezwa lakini hawakuchukua hatua mpaka sasa. Hata baada ya Katibu wetu wa wilaya kuandika barua ya malalamiko kwa TAKUKURU, Badala ya TAKUKURU kuchukua hatua walimshikilia na kumhoji Katibu wetu.
- Katika kata ya Kijungu Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Makamba alitoa mifuko 30 ya simenti kwenye mkutano wa hadhara lakini si polisi wala TAKUKURU waliochukua hatua.
VI. Ushiriki wa Watendaji wa Serikali
Miongoni matatizo makubwa ya uchaguzi wa Kiteto na taifa hili kwa ujumla ni pamoja na watendaji wa serikali kutumia mamlaka yao kukisaidia Chama Cha Mapinduzi kushinda jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utumishi. Baadhi ya mambo yaliyojitekeza wazi kwa watendaji wa serikali kutumia nafasi zao kukisaidia CCM wakati wa uchaguzi wa Kiteto ni pamoja na haya yafuatayo;
- Mkuu wa Mkoa wa Iringa Haijjati Amina Mrisho aliacha ofisi yake kwenda Kiteto kwenye kampeni akitumia gari la serikali na akizungumza majukwaani kama mkuu wa mkoa na alilipotiwa kwenye vyombo vya habari, Hivyo Waziri Mkuu na hata Rais wanafahamu kuwa Mkuu huyu wa mkoa alikuwa kwenye kampeni za CCM kwa gharama za serikali. Baada ya kulalamikiwa ndipo akaomba likizo kwenda kwenye kampeni Kiteto na hakuna hatua aliyokwishachukuliwa kwa makosa hayo mpaka sasa.
- Mkuu wa mkoa wa Manyara akijua kuwa wilaya ya Kiteto kuna uchaguzi alianza kuzindua miradi ya maendeleo sambamba na kampeni za uchaguzi.
- Katika kuipigia kampeni CCM na kuidhoofisha CHADEMA Mkuu wa wilaya ya Kiteto aliwaeleza wakazi wa Kijungu kwenye mkutano wa hadhara yeye kama mkuu wa wilaya anajua kuwa CHADEMA isingekwenda kwenye kampeni na Helikopta katika kata ile.
- Mtendaji wa kijiji Cha Mchanila alimwandikia barua mchungaji wa KKKT wa kijiji hicho kumtaka ahakikishe watu wake hawajihusishi na CHADEMA.
- Ofisi ya serikali ya kijiji cha Dongo ilitumika kama ofisi ya kampeni za CCM. Na Watumishi hao walielekeza kuwa watu wa CHADEMA wasipewe huduma ya maji inayotolewa na kijiji hicho kwakuwa wanapinga CCM.
- Katika Kata za Lengatei na Sunya Watendaji wa kata waliwaandika barua za kuwatisha kuwa wamekataa kutoa michango kwa ili kuwatisha watoroke wasipige kura.