Tamko la Mkurugenzi wa Vijana wa Taifa wa CHADEMA kuhusu kauli ya Serikali ya Kuwakana Vijana wa Kitanzania waliotelekezwa Ukraine
"Nimesikitishwa na kauli ya serikali ya kutangaza kutowatambua vijana hawa
wa kitanzania wakati ambapo vielelezo mbalimbali vilivyotolewa na wazazi
wa watoto hao vinaonyesha kuwa walikuwa na baraka za serikali wakati wa
kuondoka kwao. Aidha inashangaza kwamba pamoja na suala hili kufikia hatua
ya juu kwa maana ya kufahamika na Rais Kikwete, Waziri Mkuu Lowasa na hata
balozi mbalimbali, kauli ya kutowatambua imetolewa na mtendaji wa
serikali. Tulitegemea Waziri mwenye dhamana ya wizara hii angejitokeza
sasa kutoa ufafanuzi kuhusu suala zima. Hii ni ishara ya kukosa
uwajibikaji. Sijui Waziri Msolla anafanya kazi ya kuwatumikia walipa kodi
wa nchi gani kama masuala yanayowahusu watanzania yanayoigusa wizara yake
anakwepa kutolea ufafanuzi. Alikuwa kimya katika kipindi cha mgomo wa vyuo
vikuu vya SUA na UDSM. Sasa yuko kimya tena katika suala la wanafunzi wa
kitanzania waliotelekezwa Ukraine. Na uko ushahidi kwamba amekuwa akikata
simu akipigiwa kuulizwa kuhusu suala hili. Vijana wa CHADEMA tunaunga
mkono kauli iliyotolewa na viongozi wakuu wa upinzani ya kumtaka Profesa
Msolla ajiuzulu mara moja. Mfumo mzima wa uchangiaji wa elimu ya juu na
utendaji wa bodi ya mikopo unaliingiza taifa kwenye malumbano yenye hasara
kwa wanafunzi na nchi kwa ujumla; hivyo yeye kama waziri wa wizara
inayohusika na suala hili anapaswa kuwajibika. Hivi kwani hakuna
watanzania wengine wenye kuweza kuendesha wizara ya elimu ya juu zaidi
yake?
Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru ambayo itapewa mamlaka ya kuchunguza
ukweli wa madai ya vijana hawa na kuchukua hatua mara moja ya kutatua
suala hili. Pendekezo linalotolewa ni kuwa, kabla ya lolote kufanyika
serikali ikubali kuwadhamini vijana hawa kwa mwaka ujao wa masomo (kwani
tayari wameshaanza masomo miezi hii yote) na iachane kabisa na wazo la
kuwanunulia tiketi warudi nyumbani. Wazo la kuwarudisha nyumbani ni wazo
la watu walioshindwa! Endapo vijana hawa watarudi nyumbani itakuwa ni
ishara ya viongozi wetu kushindwa kabisa kutatua matatizo na badala yake
kung'ang'ania visivyong'ang'anika. Kama tumeweza kuvumilia na kuwapa muda
watendaji wengi wabovu wajirekebishe, nina uhakika serikali inaweza kabisa
kuwavumilia na kuwadhamini vijana hawa kwa mwaka huu wakati tume
inachunguza ukweli. Tume iwe na uhuru na uwezo wa kumuita na kumhoji
kiongozi yeyote na ifanye kazi zake mbele ya vyombo vya habari. Endapo
baada ya uchunguzi kufanyika itagundulika kuwa kuna makosa yalifanyika
basi serikali inaweza aidha kuwaambia vijana hivyo lakini kuendelea
kuwasomesha hadi wahitimu kwa makubaliano mapya au kuwarudisha nyumbani
kwa mpango wa kuwapa nafasi ya kuendelea na masomo yao nyumbani. Kwa
kufanya hivyo wanafunzi hawapotezi, na serikali haishindwi.
Na endapo itaonekana kuwa viongozi kule bodi ya mikopo na wizarani
waliboronga basi hatua za kinidhamu zichuliwe dhidi yao. Jambo la maana ni
kuunda tume huru ambayo itakuwa na uwezo wa kumhoji kiongozi yeyote
hadharani na kuita vielelezo vyovyote. Kwa kufanya hivyo, serikali
itaonesha kulipa uzito unaostahili suala hili badala ya kutulazimisha
tukubali matamshi yake tu hata kama matamshi hayo yanazua maswali zaidi
kuliko majibu.
Ni matumaini yangu kuwa serikali itaonesha busara na si papara na itatumia
hekima ya hali ya juu ili kuhakikisha kuwa vijana wetu wanaendelea na
masomo, taratibu zinafuatwa na Taifa letu linaendelea kuheshimu elimu ya
juu bila ya kujali hadhi au hali ya mtu.
Hili tatizo linafanana sana na tatizo lililo wakumba wanafunzi wa Tanzania
nchini Poland mwaka 1996/97. Mtu aliyekuwa anawakwamisha ni Prof.
Mahalu,Wakati hupo akiwa mkurugenzi wa elimu ya juu. Na wenyewe waliambiwa
hivyo hivyo hawatambuliwi na warudi nyumbani. Waliorudi ndio hawakusoma
tena labda baadaye sana. Kuna vijana wengine wakazamia Magharibi.
Bahati nzuri baada ya kama mwaka tatizo lao likatatuliwa na wote waliokuwa
bado wako Poland, wakasoma na sasa wamemaliza masomo na wanaitumikia
serikali yao.
Jitihada zifanywe ili hawa wanafunzi wamalizie masomo yao huko huko waliko
maana wakirudi Tanzania kwanza kwa mwaka 2007/8 hawawezi kwenda vyuoni
maana muda umepita. Hata huko mbele itakuwa ngumu na itabidi wagombanie
hizo nafasi na wanafunzi wengine wa miaka ijayo.
Hata kama kuna kosa limefanyika, suluhisho rahisi ni kuwasaidia hao vijana
wamalizie masomo yao huko huko Ukraine.
Kwa kuwa hali ya wanafunzi kule Ukraine ni mbaya, natoa rai kwa watanzania
wenye mapenzi mema walione jambo hili kuwa ni janga linalohitaji misaada
ya kibinadamu. Wakati jambo hili linatafutiwa ufumbuzi lazima tuchukue
hatua za kuokoa maisha ya watanzania wenzetu. Hapa natarajia mashirika
yanayohusika na haki za binadamu yataangalia swala hili kwani vijana wale
wanaishi kwenye mazingira magumu sana na hili linahatarisha hata
mustakabali wa maisha yao kwani huenda wengine wakapatwa na matatizo ya
kiakili na kuamua kufanya jambo lolote ambalo nlitayahatarisha maisha yao.
Natoa mwito kwa watanzania kuchangia harambee ambayo viongozi wa vyama vya
upinzani wameomba shirika lisilo la kiserikali la TANLET liratibu kwa
ajili ya kuwaokoa vijana hawa wa kitanzania wasikose elimu.
Mwisho narudia tena rai ya kuitaka Wizara inayohusika kuendesha mjadala
kuhusu Uchagiaji wa Elimu ya Juu nchini kabla ya Bunge kujadili bajeti ya
Mwaka wa Fedha 2007/2008 ili kuepusha migogoro katika vyuo vya elimu ya
juu nchini ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na suala hili. (Rejea
taarifa ya Tume iliyoundwa na serikali miaka ya hivi karibuni kuchunguza
vyanzo vya migomo na migogoro katika elimu ya juu). Baadhi ya mambo
muhususi yanayopaswa kushughuliwa ni: Mifumo ya Uchangiaji wa gharama za
elimu ya juu; Kusitisha mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria na. 9 ya mwaka
2004 yenye kulenga kuimarisha uwekaji wa madaraja na viwango vya asilimia
katika uchangiaji wa elimu juu; Haja ya kupandisha madaraja ya utoaji
mikopo na kuweka stahili ya mikopo kwa wote wenye kupata udahili
(admission); mifumo ya kutambua uwezo wa wanafunzi (means testing);
Kiwango cha ruzuku na menejimenti/uendeshaji wa bodi ya mikopo na mifumo
ya urejeshaji wa fedha za mikopo kwa wanafunzi. Tuko tayari kutoa maoni
yetu ya ziada pindi utaratibu utakapotangazwa. Mabadiliko yaliyotangazwa
na bodi ya mikopo hivi karibuni ya kuweka viwango vipya vya mikopo bado
hayajajibu hoja za wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu nchini. Bado
serikali imeendeleza utaratibu wenye kuchochea madaraja na matabaka katika
elimu ya juu nchini hivyo mjadala kuhusu suala hili ni jambo linalohitaji
kufanyika mapema iwezekanavyo. Tunaweza kuona suala la watanzania 29
waliotelekezwa Ukraine ni jambo dogo; lakini linabeba ujumbe mzito kuhusu
mapungufu yaliyomo katika mfumo wetu wa elimu ambayo yapaswa
kushughulikiwa kwa hatma ya Taifa letu"
Tamko hili limetolewa tarehe 29 Mei 2007:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana