Ushindi wa Kishindo au Ufisadi wa Kishindo?
Maswali muhimu ya kujiuliza kuhusiana na Tangold Ltd. ni haya yafuatayo. Kwanza, ilikuwaje kampuni ambayo haikuwa hata imeandikishwa kisheria ikalipwa mabilioni ya fedha za walipa kodi na/au ya umma na bila maelezo yoyote? Pili, ilikuwaje Serikali, kwa kupitia Waziri Karamagi, itoe taarifa ya uongo Bungeni kwamba Tangold Ltd. ni kampuni mpya na imeanzishwa ili kurithi mali na madeni ya Meremeta Ltd. wakati makampuni yote mawili yalikuwa yakipeana mabilioni ya fedha za umma wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu katika mazingira ya kutatanisha? Tatu, kwa nini malipo ya mabilioni haya yalikoma mara baada ya Uchaguzi Mkuu? Nne, kama Tangold Ltd. ni kampuni inayomilikiwa na Serikali je ofisi zake ziko wapi? Watendaji wake wakuu ni kina nani? Fedha za kigeni dola za Marekani 13,340,168.37 zilizolipwa na BOT tarehe 29 Desemba 2005 zilikuwa ni kwa ajili gani na kwa nini zimeendelea kuwa katika akaunti ya Tangold Ltd. hadi wakati huu?
Hivi karibuni baadhi ya wanachama wa CCM wameanza kuhoji matumizi makubwa ya fedha wakati wa mchakato wa kumpata mgombea Urais wa CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita. Kama mnavyokumbuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Bwana Joseph Butiku ametoa hadharani barua aliyomwandikia Mwenyekiti wa CCM aliyepita Bwana Benjamin Mkapa akidai kuwepo kwa ushahidi kuwa “fedha nyingi zinatumiwa katika uchaguzi huu.” Na kama alivyohoji Mzee Butiku katika barua yake kwamba “fedha hizo zinatoka wapi na ni za nani”, nasi tunawaomba wananchi wa Tanzania waidai Serikali iwaeleze mabilioni haya ya fedha za umma yalilipwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2005 kwa ajili gani.
Ili kupata majibu sahihi ya maswali yote haya, Serikali haina budi kuridhia kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi wa tuhuma zote hizi na zile zilizotolewa katika Orodha ya Mafisadi. Ni tume huru pekee itakayoweza kuchunguza ufisadi huu bila woga, upendeleo au hila. Na ni ripoti ya tume huru pekee ndiyo itakayotumika kuwawajibisha wale wote watakaobainika kushiriki kulisababishia taifa letu hasara kubwa namna hii.
Tunatambua kwamba Serikali imeteua wakaguzi wa mahesabu kutoka kampuni ya Ernst Young LLP ili kufanya uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za umma katika akaunti ya malipo ya nje inayoendeshwa na BOT (EPA) kwa niaba ya Serikali. Tunaomba kuweka wazi msimamo wetu kuhusiana na uchunguzi huo kuwa hauhusu ubadhirifu, wizi na/au ufisadi ndani ya BOT tuliouelezea katika Orodha ya Mafisadi na katika Taarifa hii. Vile vile uchunguzi huo hauhusu ufisadi unaohusu kusainiwa kwa mikataba mibovu na ambayo imeliingizia na italiingizia taifa letu hasara ya mabilioni ya fedha za kigeni. Kwa maana hiyo, tunatoa taarifa mapema kwamba ripoti ya wakaguzi wa Ernst Young LLP haiwezi na isije ikachukuliwa kuwa ndio majibu ya Serikali kwa tuhuma za ufisadi, wizi na/au ubadhirifu wa fedha za umma zilizotolewa katika Orodha ya Mafisadi na katika Taarifa hii. Tunapenda kusisitiza kwamba tuhuma hizi zinaweza kujibiwa tu na tume huru ya uchunguzi.
Kutokana na uzito wa masuala tuliyoyaeleza katika Taarifa hii, tunapenda kuwataarifu wananchi wa Tanzania kwamba iwapo Serikali itashindwa na/au kukataa kuridhia kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi wa tuhuma hizi hadi kufikia 25 Novemba mwaka huu, vyama vyetu vitatoa maelekezo kwa wanachama wetu na wananchi kwa ujumla juu ya hatua za kuchukuliwa nao ili kuondokana na ufisadi, wizi na/au ubadhirifu wa mali ya wananchi tuliouelezea katika Taarifa hii na katika Orodha ya Mafisadi.
Asanteni sana.
Freeman Aikaeli Mbowe - Mwenyekiti, CHADEMA
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba - Mwenyekiti, CUF
James Francis Mbatia - Mwenyekiti, NCCR-MAGEUZI
Agustino Lyatonga Mrema - Mwenyekiti, TLP