Taarifa kwa Umma
UTANGULIZI
Itakumbukwa kwamba Serikali kupitia Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo walitoa kile walichoita tamko ama ufafanuzi juu ya tuhuma za rushwa na ufisadi zinazoendelea hapa nchini na kama zilivyoibuliwa na Mbunge wa Karatu - Dkt. Willbroad Slaa kupitia ‘orodha ya mafisadi’ (list of shame) aliyoitoa hadharani.
Taarifa hiyo ya serikali imeendeleza utamaduni uleule wa kutumia propaganda katika kujibu masuala muhimu ya kitaifa. Pia ufafanuzi huo wa serikali ulitolewa kwa mfumo ule ule wa kutumia kauli za kubeza badala ya kujibu hoja bila kujali athari za rushwa na ufisadi kwa ustawi wa taifa hili.
Lifuatalo ni tamko la CHADEMA kuhusu ufafanuzi wa serikali juu ya tuhuma za ufisadi; tamko ambalo linabainisha jinsi ambavyo serikali imekwepo kujibu hoja zilizotolewa na linachambua ni maeneo yapi haswa ambayo serikali ilipaswa kuyatolea ufafanuzi. Bado tunaendeleza kusisitiza kuwa tunahitaji majibu ya kina kutoka serikalini na yenye kujibu hoja na kuchukua hatua badala ya kutoa kauli ambazo zinaashirikia kukwamisha jitihada za kuondokana na ufisadi na kuhakikisha rasilimali za Tanzania zinatumika kuleta maisha bora kwa wananchi walio wengi.
I. TUHUMA KUHUSU BENKI KUU YA TANZANIA
Tunaamini ili serikali isiendelee kuwapotosha wananchi inatakiwa kutoa majibu ya kina na kuridhisha kuhusu tuhuma za ufisadi katika benki kuu. Taarifa iliyotolewa kutokana na Maelezo ya Hoja binafsi iliyokuwa iwasilishwe Bungeni na Dr Slaa ilikuwa na maswali ya msingi ambayo hayawezi kujibika tu kwa kutamka kuwa ‘ni ya uzushi’.
Serikali inatakiwa kujibu maswali ya msingi yaliyokuwepo kwenye maelezo yaliyotajwa mathalani:
- Kwa nini serikali isitoe mkataba wa ujenzi wa ‘Twin Towers’ utolewe hadharani ili wananchi wajue kuwa tuhuma ni uzushi au la? Wazabuni (Tenderers) walikuwa nani? Zabuni(Tender) ilitolewa lini na mchakato wake ulikuwaje? Mshindi wa zabuni ni nani na wakurugenzi wa Kampuni hiyo na sifa zao? Gharama ilivyokuwa kwenye Mkataba na tofauti (variations) ni zipi?, na jinsi gani ziliidhinishwa?(mihuktasari ya vikao vilivyoidhinisha ziko wapi)?
Vinginevyo: Majibu ya Serikali hayajakidhi na hayatakidhi haja, na hayajawasaidia watanzania ambao ndio wenye mali na ndio wanaotaka kujua ukweli. Ukweli haupatikani kwa tamko uchi bila vielelezo vyovyote.
- Uchunguzi unaofanywa na inayotajwa kuwa Kampuni ya Ukaguzi wa Kimataifa (‘International Auditing Firm”) ni tone la sukari katika Bahari. Ukaguzi huo hauhusishi maeneo yaliyoelezwa ambako fedha za Walipa kodi zimetumika katika makampuni binafsi ya Meremeta, Tanagold, Mwananchi Gold Company Ltd, na kadhalika. Inahusu tu eneo la EPA, Isipokuwa kama hadidu rejea (“Terms of Reference”) zimeongezeka tofauti na zilizotolewa Bungeni.
Hivyo basi: Ukaguzi unaofanyika ni sehemu ndogo sana na hoja haziwezi kupata majibu kutokana na ukaguzi unaoendelea. Tunachukua fursa hii kutoa mwito kwamba ukaguzi na uchunguzi mpana ufanyike kuhusu tuhuma hizi za ufisadi utakaohusisha maeneo na masuala yote yaliyotajwa. Serikali isijifiche nyuma ya kivuli cha ukaguzi huu mdogo kuficha ufisadi mkubwa uliofanyika ndani ya Benki Kuu (BOT).
UKAGUZI WA BOT
Maelezo ya Serikali yanayoonyesha aliyeyatoa hajui msingi wa hoja ,au hajasoma au hajafanya utafiti wa kina kuhusu tuhuma zilizotolewa na Dr. Slaa:-
- Taarifa ya ukaguzi ya BOT inayosemekana ilipelekwa kwa Kamati ya Fedha hazijafika Bungeni. Hadi leo hii, karibu ya mwaka mzima kinyume na Sheria ya BOT Taarifa hiyo haijawasilishwa Bungeni. Tunaitaka serikali itazame sheria inayohusika. Huu ni uvunjaji wa Sheria usioweza kuvumilika kwa Taasisi kubwa kama BOT.
- Inawezekana serikali haijachunguza Maelezo ya Hoja na Taarifa ya Ukaguzi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) iliyowasilishwa kwa Kamati ya Fedha. Hoja zote zilizotolewa hazijajibiwa. Ni vema serikali ikachukua muda wake kufanya utafiti wa kina, isome maelezo ya hoja ya msingi, na yapatiwe majibu. Lugha inawezekana imerekebishwa kidogo lakini hoja za msingi ziko pale pale, watanzania wanatakiwa kufahamu kilichojiri, na maelezo ya kina.
- Serikali inasema hoja za Dr. Slaa hazina ushahidi. Ni wazi, Ushahidi wa kamili upo, baadhi ya ushahidi huo unatoka katika taasisi za serikali yenyewe na mwingine utatolewa pale utakapohitajika kisheria na sio vinginevyo. Serikali ingelikubali Kuunda Kamati Teule, ushahidi wote ungelitolewa katika Kamati hiyo. Hivyo ushahidi utatolewa siku itakapokuwa lazima kuutoa yaani Mahakamani, na iwapo Serikali inania ya kuupata siyo kwa kutoa matamko uchi bali kwa taratibu za kawaida za kisheria.
UJENZI WA MAJENGO YA BOT
Inawezekana wahusika anafanya kazi na nyaraka zisizo sahihi. Ni vyema wasome hoja ya Dr. Slaa ilieleza nini kuhusu thamani ya Tshs 522,459,255,000. Hoja hiyo inahitaji majibu, na yatapatikana kimsingi wakati Serikali itakapoweka hadharani mkataba wa ujenzi, na Hati mbalimbali zilizopitisha matumizi husika.