Sisi, viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR Mageuzi na TLP tuliokutana Equator Hotel tarehe 20 Septemba 2007 hapa Arusha tumeitafakari “Orodha ya Mafisadi” (List of Shame) na tumejadili kauli za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Siasa na Uhusiano wa Jamii-Mheshimiwa Kingunge Ngombale-Mwiru alizozitoa 18 Septemba 2007 na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari Jumatano 19 Septemba 2007 na kwa pamoja tumeazimia kutoa tamko lifuatalo:
Kingunge anapotosha umma, apuuzwe; wapinzani wanatetea taifa
Tunaunga mkono uamuzi wa viongozi wetu wa kitaifa kuanika wazi kwa umma orodha ya mafisadi; hii ni kwa sababu rasilimali zinazofujwa ni za wananchi watanzania, wanaoathirika kutokana na ufisadi ni umma wa watanzania na wenye uamuzi wa mwisho wa kuwawajibisha viongozi mafisadi ni umma wa watanzania. Kwa kuzunguka nchini kueleza yaliyotokea bungeni (hususani kusimamishwa kwa Mbunge Zitto Kabwe na kupigwa danadana kwa hoja ya kashfa ya ufisadi ndani ya Benki Kuu iliyokuwa iwasilishwe na Dr Wilbroad Slaa) wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti uliomalizika hivi karibuni, wabunge wa upinzani wanatimiza wajibu wao kama wawakilishi wa kweli wa wananchi. Kwa kuzunguka nchini kueleza kuhusu ufisadi unaendelea nchini, viongozi wa upinzani wanatekeleza wajibu wao wa kisiasa wa kuwazungumzia wananchi wote wa Tanzania wanaoguswa na ufisadi bila kujali itikadi ama uanachama; ikumbukwe kuwa vyama vya siasa sio vyombo vya uchaguzi tu bali ni taasisi muhimu katika jamii katika kuchochea uwajibikaji na maendeleo. Kwa mantiki hiyo basi Waziri Kingunge anaupotosha umma anaposema kwamba ziara za viongozi wa upinzani zinatokana na ‘hasira ya kushindwa uchaguzi mkuu 2005, kambi ya upinzani kushindwa kumtetea Zitto bungeni, wivu wa kuona CCM inatekeleza ilani yake vizuri, na kwamba wanautumia vibaya mfumo wa vyama vingi’. Tunapenda kusisitiza kuwa Viongozi wa umma wanaokiuka na/au kuvunja masharti ya katiba ya Jamhuri ya Muungano na Sheria za Maadili ya Viongozi wa umma lazima waanikwe hadharani na kuwajibishwa na yoyote anayetoka kauli ya kubeza jitahada hizi ni vyema watanzania wakampuuza. Kama viongozi wa upinzani wanavunja sheria kwa kutoa uzushi na kufanya uchochezi kama Waziri Kingunge anavyodai kwa nini serikali haiwakamati na kuwapeleka mahakamani badala ya kutoa matamko ya kulalamika?
Kauli za Kingunge ni msimamo wa Serikali? Ikulu itoe tamko!
Tumezijadili kauli za Waziri Kingunge na katika hatua ya sasa tusingependa kuamini kama zinawakilisha msimamo wa serikali kwa ujumla wake; hatutaki kuamini kwamba kauli hizo ni msimamo wa pamoja wa Serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri. Katika hatua ya sasa tunazichukulia kauli hizo kuwa ni maoni binafsi ya Bwana Kingunge mpaka hapo Ikulu itakapothibitisha vinginevyo; hivyo kwa tamko hili tungependa ikulu itoe ufafanuzi kuhusu kauli hizo. Lakini tunapenda pia kutoa tahadhari kwamba inawezekana kauli hizi za Bwana Kingunge amezitoa kwa nia ya kupoteza lengo tuanze kuzijadili kauli zake badala ya kujadili orodha ya mafisadi na hatma ya rasilimali za nchi yetu. Hivyo tungependa kusisitiza kuwa ikulu ijibu hoja zilizotolewa na viongozi wa upinzani ambazo zimemgusa moja kwa moja Rais na serikali.
Anayelinda ufisadi ndiye anayekwamisha maendeleo na huduma za kijamii
Tunashangazwa na uamuzi kauli ya Kingunge kwamba uamuzi wa Viongozi wa Vyama na Wabunge wa Upinzani kuzunguka nchini ni mkakati wa kisiasa wa kuitoa serikali kwenye mstari wa kushughulikia maji, afya na barabara. Tunapenda kumbukusha Waziri Kingunge kuwa katika orodha hii ya mafisadi pekee zaidi ya shilingi trilioni 1.3 (1,300,000,000,000.00) ambazo kama zingetumika vizuri ni wazi zingeweza kutumika kuboresha maji, umeme na barabara bila kuendelea kuwakamua zaidi wananchi masikini. Ukweli ni kuwa kwa kuendelea kulea ufisadi serikali inajitoa yenyewe kwenye mstari wa kutumia vyema kodi za wananchi na rasilimali za taifa katika kushughulikia shughuli za maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo maji, afya na barabara. Ni ukweli pia kwamba kwa kuwawajibisha mafisadi viongozi wa upinzani wanatimiza wajibu wao wa kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa ustawi wa wananchi walio wengi.
Vyombo vya dola tayari vinayo orodha ya mafisadi; vichukue hatua
Tunashangazwa na kauli ya Waziri Kingunge ya kuhoji sababu za Viongozi wa Upinzani kushindwa kuziwasilisha kwenye vyombo vya dola tuhuma walizozitoa dhidi ya vigogo hao iwapo kweli wanao ushahidi wa kuzithibitisha. Tunashangazwa na kauli hii kwa kuwa tunaamini kabisa Waziri Kingunge anafahamu kabisa kuwa sehemu kubwa ya tuhuma hizi zipo katika Ripoti za Mkaguzi wa Serikali ikiwemo ile ya mwaka 2005/06 na kwamba vyombo vya dola vinafahamu uwepo wa tuhuma hizi lakini kwa zaidi ya miaka miwili vyombo hivyo havijachukua hatua dhidi ya vigogo waliotajwa. Tunaamini kwamba viongozi wa upinzani walichofanya ni kuamua kushtaki kwa wenye mali walioibiwa ambao ni wananchi wote wa Tanzania ili kwa pamoja tuweze kuvitaka vyombo vya dola viweze kuchukua hatua. Tunashangazwa na kauli hii ya Waziri Kingunge ya ‘kuwahukumu’ viongozi wa upinzani kwa kushindwa kupeleka ushahidi kwa kuwa kauli hii inapingana na kauli zingine ambazo zimewahi kutolewa na viongozi wa serikali kuhusu tuhuma hizo hizo. Tunapenda kumkumbusha Waziri Kingunge kwamba tayari Spika Wa Bunge-Samuel Sitta alishasema kwamba anavipeleka polisi vielelezo vyote vya ushahidi alivyotoa Dr Slaa ili vichunguzwe. Pengine Kingunge angetoa hukumu hiyo kwa Spika kwa kushindwa kupeleka vielelezo. Pia ikumbukwe kwamba ni serikali hiyo hiyo iliyowahi kutoa taarifa kwa umma kwamba tuhuma za ufisadi ikiwemo za BOT zinachunguzwa na TAKUKURU. Kadhalika Waziri Mkuu-Edward Lowasa alitoa kauli baadaye kwamba Serikali iliyafahamu madai ya Kashfa ya ufisadi Benki Kuu (BoT) kabla ya upinzani. Kwa upande mwingine, madai ya kutaka kushughulikia rushwa kubwa kubwa ikiwemo za kwenye mikataba yalianza kutolewa na Rais Kikwete wakati akifungua Mkutano wa Kwanza kabisa wa Bunge mwaka 2005. Lakini baadaye ni Rais Kikwete alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba anawafahamu wala rushwa na anawapa muda wajirekebishe; tulitarajia Waziri Kingunge kama mshauri wa Rais wa masuala ya siasa angemshauri apeleke ushahidi katika vyombo vya dola na si kuwahukumu viongozi wa upinzani ambao wametoa orodha ya mafisadi na ushahidi kutoka kwenye taasisi za serikali yenyewe!. Na ni jukumu la vyombo vya dola kuchukua hatua za kufuatilia baada ya orodha ya mafisadi kuwekwa hadharani.
TAKUKURU inajipotezea imani yenyewe!
Tumeshangazwa pia na kauli ya Waziri Kingunge ya kuwalaumu viongozi wa upinzani kwa kutokuwa na imani na TAKUKURU. Kwa misingi ya kauli zao ambazo wamezitoa katika nyakati mbalimbali, viongozi wa upinzani wamekuwa wakikisisitiza kuwa TAKUKURU inajipotezea yenyewe imani kwa wananchi kutokana na taarifa zake na kwamba wamekuwa wakiipa changamoto TAKUKURU kuchukua hatua. Mathalani TAKURU kuisafisha kampuni ya RICHMOND. “….hakuna ushahidi wowote uliopatikana kuthibitisha vitendo vya rushwa, uzembe na upokeaji wa kamisheni watendaji wa serikali….uchunguzi huo umethibitisha udhaifu wa kawaida katika utendaji na ambao haukuhusisha rushwa au manufaa ya aina yoyote ile kwa upande wa watendaji na hakuna hasara iliyosababishwa na udhaifu huo” (Mwananchi 12/5/2007). “….baada ya kuona hivyo, Richmond ilionekana kufahamu mwenendo wa mambo serikalini…” (Tanzania Daima 12/5/2007). Maswali yaliyobaki mpaka hivi sasa ambayo si TAKURU wala TAKUKURU ya sasa hawajayajibu ni pamoja na: Ni kwanini Kamati ya Waziri Mkuu iliipa tenda Richmond baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kuitaka bodi yake ya sabuni kutangaza upya zabuni hiyo kwa kutimia zabuni za kimataifa? Richmond kuweza kufahamu mwenendo wa mambo ya ndani serikalini sio ishara ya rushwa ya kimadaraka? Ni kweli kama hakuna hasara iliyosababishwa na uamuzi huu wakati ambapo watanzania wamekaa bila umeme kwa miezi mingi bila kupata umeme wa dharura waliotarajia wakati wa dharura, Rais amekiri kwamba umeme ulichangia kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi na hata kuongeza mfumuko wa bei na mpaka leo bado megawatts 100 hazijatimizwa na Richmond/Dowans? Tunapenda kumkumbusha Waziri Kingunge kwamba Mkataba wa Richmond/Dowans pekee umeligharimu taifa zaidi ya Bilioni 200 mpaka sasa ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye elimu, afya na barabara. Viongozi wa upinzani wanapohoji utendaji wa TAKUKURU wanataka ichukue hatua za haraka kushughulikia mafisadi na kuendelea kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa na si Taasisi ya Kulinda, Kusafisha ama Kutetea Rushwa !
Wasomi na asasi za kijamii wako sahihi; Kingunge amelewa madaraka
Tumefadhaishwa na kauli ya Waziri Kingunge kwamba wasomi nchini wametathimini uamuzi wa Bunge wa kumsimamisha Mbunge Zitto Kabwe kwa kutanguliza jazba badala ya busara na kutilia wasiwasi uelewa wa makundi ya kijamii kuhusu mantiki ya uzalendo. Hatutaki kuamini katika hatua ya sasa kwamba huu ni msimamo wa serikali kwamba wasomi na makundi ya kijamii wametanguliza jazba na kukosa busara na uelewa katika kuijadili adhabu aliyopewa Mbunge Zitto Kabwe na hoja yake ya kutetea Rasilimali za nchi yetu hususani madini. Tunaamini kwamba kauli hii ni maoni binafsi ya Bwana Kingunge ambayo ni ishara ya kulewa madaraka kutokana kung’ang’ania serikalini toka wakati nchi hii inapata uhuru kwani hii si mara ya kwanza kutoa kauli za kubeza-aliwahi kuibeza CHADEMA kwa kumtaja Nyerere kwenye kampeni 2005 na hivi karibuni Julai 3, 2007 aliripotiwa na vyombo vya habari akitetea msimamo wa Rais Kikwete wa kutumia nafasi yake kama rais kudhoofisha upinzani kwa kufanya kampeni za CCM katika mikutano ya kiserikali. Tunapenda kumbukusha Waziri Kingunge maneno ya Shaban Robert kwamba “ elimu ilipokuwa bado kujulikana mvi zilihesabika kuwa alama ya hekima lakini fikra hizo wakati wake umeshapita haupo na wala hauji tena. Kisichobadilika ni kwamba mtu mzima bado anastahili heshima kutoka kwa mdogo” . Ni vyema Waziri Kingunge akafahamu kwamba wasomi kama Profesa Issa Shivji na makundi ya Kijamii mathalani Mtandano wa Jinsia (TGNP), Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walifanya tathmini yao kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa bila kujali itikadi.
Mafisadi zaidi waendelee kutajwa; serikali ijibu hoja
Hivyo tunapongeza na tutaendelea kuunga mkono jitahada zote za vyama vya siasa, asasi za kijamii na hata watu binafsi waliowataja na watakaoendelea kuwataja viongozi na/au maafisa wa umma na/au mawakala na/au washirika wao katika sekta binafsi ambao kwa namna mbali mbali wameshiriki katika kupora utajiri na/au fedha za umma na hivyo kulisababishia taifa na umma wa Watanzania ufukara na/au umaskini mkubwa. Kadhalika tunaunga mkono na kutoa mwito kwa vyama vya siasa, asasi za kijamii na hata watu binafsi kuendelea kuwawajibisha viongozi wa umma ambao kwa kutumia nyadhifa na/au vyeo vyao katika utumishi wa umma wamefanya maamuzi ambayo yamesababisha taifa limepoteza mapato na/au utajiri na rasilmali zake na kuwaneemesha raia na/au taasisi za kiuchumi na/au za kibiashara za kigeni. Kwa mfano, viongozi wa umma walioshiriki katika kusaini mikataba mibovu katika sekta za madini na/au nishati na/au maeneo mengine yenye umuhimu mkubwa kwa maisha ya taifa na jamii ya Watanzania. Na katika haya tunataka serikali ijibu hoja na si kupuuzia na kutoa kauli za kejeli kama "hao ni wapinzani hawana jingine la kufanya", "wana haki ya kutoa maoni yao na huo ndio uzuri wa demokrasia" . Waziri Kingunge na serikali kumbukeni kuwa watu wachache wanaweza kudanganyika katika muda mchache lakini watu wote hawewezi kudanganywa wakati wote. Watanzania wa leo na kesho si Watanzania wa jana na juzi.
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa (CHADEMA)
Na Mwenyekiti wa Kikao
Godbless Lema
Katibu Mwenezi Mkoa-Arusha (TLP)
Na Msemaji wa Ushirikiano wa Vyama vya Upinzani-Arusha
Mohamed Maabad
Mwenyekiti wa Wilaya-Arusha Mjini (CUF)
Na Mwenyekiti wa Ushirikiano wa Vyama vya Upinzani-Arusha
Ened Muro
Mwakilishi-Arusha (NCCR-Mageuzi)
Amos Kibanda
Katibu Mkoa-Arusha (CHADEMA)
Calist Lazaro
Mwenyekiti wa wilaya-Arusha Mjini (TLP)