Mei 27, 2006, Naibu Katibu mkuu UV-CCM bara aliupotosha umma wa Watanzania kuhusu tathimini iliyotolewa na
CHADEMA kuhusu siku 100 za Kikwete madarakani kama ilivyoripotiwa katika gazeti la Majira, toleo namba 4527 la Mei 29.
Bwana Makala katika hotuba yake hiyo aliyoitoa wilayani Temeke, alidai kuwa “Mbowe alitoa kauli kuwa rais Kikwete amekuwa
ni mtu wa kutoa ahadi, kuzunguka na kutokaa ofisini”. Makala alidai kuwa “Kikwete anafanya hivyo kuonyesha kuwa anawajali
wananchi na matatizo yao na ndio maana anazunguka ili ajue na kufanya utafiti na sio kukaa ofisini na kusubiri matatizo.”
Nimeamua kumjibu Makala kwa maslahi ya Watanzania hususan vijana wenzangu wa nchi hii wakiwemo wale wa CCM ambao Bw. Makala
amekuwa akizunguka wilaya kadhaa na kuwapotosha kila alikozunguka kwa kutumia ujumbe huu.
Inavyoelekea Bw-Makala hakulielewa vyema tamko la CHADEMA kuhusu siku 100 za Kikwete ama sivyo, ameamua kupotosha kwa
kuwafanyia vijana wenzake na umma wa Watanzania propaganda badala ya kuwaeleza ukweli.
Katika tamko la CHADEMA, kipengele cha pili sehemu ya mafanikio, Mbowe alisema “Serikali imerejesha matumaini ya kinadharia
kwa wananchi.” Mh. Mbowe alimsifu rais Kikwete kwa kuonyesha kuwa karibu na wananchi na kwamba amevunja uzio uliojengwa
na awamu ya tatu wa kutenga kwenye tabaka moja, viongozi wa serikali na CCM, wawekezaji na wafanya biashara wakubwa
katika upande mmoja na wapinzani, waandishi wa habari, wakulima, wafanyakazi na wananchi masikini kwa upande mwingine.
Kwa maneno mengine Mbowe hakumaanisha Kikwete asiwekaribu na wananchi kama Bwana Makala anavyotaka kuwasadikisha
Watanzania na hususan vijana wenzake wa UV-CCM. Hoja ya Mbowe si Kikwete kutokuwa karibu na wananchi bali Kikwete
kushughulikia matatizo ya wananchi kwa kuipatia nchi uelekeo. Na kwa upande mwingine kuwa karibu na wananchi katika
matukio ya muhimu na kuhimiza watendaji wengine nao kuwa karibu na wananchi.
Mh Rais amekuwa akizunguka huku na kule, mara leo yupo gerezani, kesho sokoni keshokutwa Muhimbili lakini kote huko
hakuna matokeo ya kutosha yanayoonekana, hakuna kinachobadilika na katika baadhi ya maeneo hali imezidi kuwa mbaya.
Kikwete anayafahamu vizuri matatizo ya Watanzania. Hii ndio hoja ambayo CCM ilikuwa ikiisema wakati wa kampeni na
kujivunia kwamba tayari alishakuwepo katika utawala kwa muda mrefu hivyo anafahamu hali halisi ya Watanzania. Vipi leo
Makala atake Kikwete apite kuyafahamu matatizo ya wananchi? Hoja ya Makala kuwa Rais anawatembelea wananchi ili kufanya
utafiti haina msingi kwani matatizo ya Watanzania yapo wazi, na kama itabidi utafiti ufanyike, hauwezi kufanywa na Rais
tena kwa kuzunguka sokoni na hospitalini. Serikali inatumia mabilioni ya pesa kudhamini tafiti mbalimbali, Sasa kama
Bwana Makala anasema Rais anapita sokoni ili kufanya utafiti kuna sababu gani ya kutumia mabilioni ya walipa kodi
masikini wanaokufa kwa njaa kugharamia tafiti za umasikini?
Katika mifumo ya utawala kuna mfumo wanaita ‘Management by Walking Around’ ambapo kipimo ni namna kiongozi anaweza
kuzungukia na kukagua, na pili kuna “Management by Results or Objectives” ambapo matokeo na malengo ndio kigezo cha
kupima mafanikio ya utawala. Sasa tunajiuliza Mh Rais ameamua kutumia staili ipi? Na Je, Watanzania wanataka staili
ipi? Wanataka “siasa-penda” za kutembelewa pekee au matokeo ya ufumbuzi wa matatizo yao?
Kimsingi hakuna maana yoyote Rais kwa kutembelea masoko kwa madai ya kujionea hali halisi ya bei zilivyopanda halafu
hakuna kitu kinachobadilika baada ya hapo. Wala hakuna maana yoyote Rais kutembelea hospitali anakuta wagonjwa wanalala
sakafuni halafu baada ya hapo hakuna kinachoendelea. Wagonjwa hawawezi kupona kwa kutembelewa na Rais, wala bei haziewezi
kushuka kwa sababu Rais katembelea soko. Wagonjwa wanapata huduma bora na bei zinashuka kwa maamuzi ya kisera na kimwelekeo.
Na kwa upande mwingine wapo wanaolalamika kuwa inaonekana wazi kuwa sasa Mh Rais anafanya kazi zisizokuwa zake, Rais hawezi
kuzunguka kila sehemu na kukutana na kila mwenye matatizo, na hii ndio sababu ukawepo uongozi katika kila ngazi. Rais kama
kiongozi wa juu anapaswa kuwapanga viongozi na watendaji wake vizuri ili waweze kutekeleza majukumu yao. Ndio maana
tunaamini kwamba wakati umefika wa Rais kuwaongoza watendaji wengine na wao wawaongoze watendaji wa chini yao mpaka
tufike wakati ambapo hata mwenyekiti wa kijiji au mtaa anatembelea wananchi na kutatua kero zao.
Hali ya sasa inaonekana wazi kuwa Rais anawaacha askari wake wa miamvuli tena kwa mbali kabisa, haya ni mapungufu na
kikwazo kwa ufanisi kwani Rais kama kiongozi hawezi kuwafikia wananchi wote wenye matatizo, lakini viongozi wakipangwa
vizuri wanaweza kuwafikia wananchi wote wenye matatizo. Hivyo Mbowe alichofanya ni kuwa mpinzani anayejali maslahi kwa
taifa kwa kumkosoa Rais kuboresha utendaji kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali itikadi.
Kwa upande mwingine sababu ya Mbowe kumshukia Kikwete aache kuendelea kuahidi kumetokana na ukweli kuwa wakati wa kampeni, CCM ndio chama kilichoongoza kwa ahadi nyingi, lakini cha kushangaza hata baada ya uchaguzi Mh Rais ameendelea kutoa ahadi lukuki huku baadhi ya ahadi alizotoa tayari muda wake umepita na bado hazijatekelezwa!
Mifano ya ahadi ambazo alizitoa na tayari muda wake umepita ni mingi, Agosti 26, 2005 Mh Rais aliahidi kuwa barabara ya Masasi-Songea kupitia Tunduru itakuwa imemalizika ifikapo Nov 2005, miezi miwili baada ya uchaguzi, leo hii ni miezi takribani sita bado ahadi haijatekelezwa kikamilifu.
Januauri 18, 2006 alimuagiza waziri wa kilimo kuhakikisha kuwa hakuna mtu anaye kufa kwa njaa. Hadi sasa wananchi ni mashahidi, Januari 28 iliripotiwa kuwa Mkoa wa Tabora pekee watu saba walikufa kwa kukosa chakula. Mkoa wa Mara watu wawili wamekufa kwa njaa. Huku Mkuu wa wilaya ya Kishapu Shinyanga akitangaza kuwa wananchi wa wilaya yake walianza kula nyasi baada ya kukosa chakula.
Mh Rais aliahidi kuwa serikali itaanza kujenga kiwanda cha mbolea mwaka huu, hadi sasa bado haijaeleweka hata ni wapi kiwanda hicho kitajengwa na sasa tunaelekea katikati ya mwaka.
Wakati akizitembelea wizara, Mh Rais alidai kuwa anasikitishwa na viongozi kutembelea mashangingi huku wananchi wanakula mlo mmoja. Sasa tunashangaa katika muda mfupi tayari serikali yake imeidhinisha mkopa wa milioni 40 kwa kila Mbunge huku wananchi wanaendelea kula mlo mmoja na hata wengine kukosa kabisa. Inasikitisha Mh Rais kutenga mabilioni ya shilingi kwa mashangingi ya wabunge lakini anakataa serikali kupoteza fedha kwa kupunguza kodi ya mafuta ili bei ishuke, nauli zipungue, wananchi wapate ahueni.
Hoja ya Mbowe si kumuhukumu Kikwete katika muda huu ambao kimsingi bado ni mapema, hoja ya Mbowe ni kumuasa Mh Rais kuendelea kuporomosha ahadi hewa. Hii ni hoja ya kizalendo inayopaswa kuungwa mkono.
Huu ndio ukweli ambao umekuwa ukisisitizwa na vyombo vya habari makini likiwemo gazeti la Mwananchi. Tunakubali kuwa ipo haja ya kumpa muda Mh-Jk kutekeleza ahadi lakini si kutoa ahadi. Barrack Obama seneta maarufu wa Marekani aliwahi kuwaambia wananchi wake kuwa kuahidi kufanya kila jambo ni kuwajengea wananchi matumaini ya upofu, na huko ndiko tunapo elekea. Sidhani kama Makala angependa tuelekee huko. Ukimya wa Kikwete kujibu tamko la Mbowe pengine ni ishara kuwa ameona mantiki ya ushauri aliopewa.
Hadi sasa haileweki ni mambo gani nchi imeamua kuyasimamia kama vipaumbele, hakuna muelekeo wa kisera na itikadi, haieleweki nchi inaongozwa kwa kutumia sera za upinzani kama ambavyo ameanza kuchomoa baadhi ya sera za upinzani (ingawa si kosa na CHADEMA iliipongeza serikali kwa kufanya hivyo kwani matokeo ya utekelezaji ni kwa maslahi ya Watanzania wote bila kujali mrengo), au nchi inaongozwa kwa ilani ya CCM au maelekezo aliyoyatoa kwenye semina elekezi ya Ngurudoto au nini hasa tumeamua kufuata kama muongozo. Inapaswa kuwa bayana kwa kila mdau kama tunaongozwa kwa MKUKUTA au mwelekeo gani ili wadau wote waweze kuunga mkono jitihada za pamoja. Na katika hili kuna haja ya kuzingatia ushauri wa Mbowe na CHADEMA wa kuchagua sekta kipaumbele ambazo kuendelea kwake kutaboresha na sekta zingine.
Upungufu wa Mh. Rais kutotulia na kuweka mambo sawa sote tumeiona, kwa muda mfupi tangu aingie madarakani amekuwa akitofautiana na hata Mawaziri wake kuhusu muelekeo wa masuala ya msingi kabisa mathalani wakati Mh Rais alitangaza kuwa bei ya umeme isingepanda na kwamba lazima TANESCO ihakikishe kuwa bei inashuka, muda mfupi baadae waziri wake wa fedha anakanusha na kwamba bei ya umeme lazima ipande. Wakati Mh Rais akiutangazia umma kuwa anawafahamu wala rushwa kwa majina, waziri Marmo alimpinga bungeni kwa kusema serikali haina ushahidi wa msingi kuhusu majina ya wala rushwa.
Kimsingi kila kiongozi na vyake, ndio maana hatukushangaa pale Rais alipotembelea daraja ambapo kimsingi waziri wa miundo mbinu aliwajibika kuwepo lakini baada ya kuhojiwa kulikoni hakuwepo aliwajibu kwa kujiamini kabisa, “sikuwepo kwasababu sikuwa na taarifa”. Mramba alinukuliwa na vyombo vya habari akilalamikia kutokuwepo kwa taarifa.
Ndio maana nasisitiza kauli ya Mwenyekiti Freeman Mbowe kuwa Mh Rais akae ikulu aipatie “Nchi visheni, tofauti na hapo atakuwa hapingani na kauli yake kuwa nchi haiwezi kuendeshwa kwa misheni town.”
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana