KUHUSU AJIRA
Wakati wa kampeni serikali iliahidi kutoa ajira milioni moja kwa miaka mitano. Katika hili Vijana wa CHADEMA tunaona matatizo ya aina mbili;
Kwanza, uwezo wa CCM na hatimaye serikali kufahamu ukubwa wa tatizo la ajira nchini unatia shaka, kwasababu ripoti ya mwaka 2002 ya tathmini ya nguvu kazi (Intergrated labourforce survey) inaonesha kuwa vijana wanaoingia kwenye soko la ajira kwa mwaka ni 650,000 mpaka 700,000. Hii inamaana kwamba baada ya miaka mitano, takribani vijana milioni nne watakuwa wameingia kwenye soko la ajira. Kwa ahadi ya ajira milioni moja, serikali inajenga mazingira ya zaidi ya vijana milioni tatu kukosa ajira.
Kwa upande wa pili, pamoja na ukweli kuwa ahadi ya ajira milioni moja ni ndogo bado serikali imeshindwa hata kufafanua namna hizo ajira milioni moja zitakavyotengenezwa na badala yake imekuwa ikitoa maelezo ya jumla tu. Serikali haielezi chochote kuhusu utaratibu wa kuifikia ahadi hiyo ndani ya bajeti ya mwaka 2006/2007 hali inayodhihirisha kuwa serikali haina mkakati maalumu unaofafanua utekelezaji wa ahadi ya ajira milioni moja hatua kwa hatua.
Aidha suala la bilioni moja zilizotengwa na serikali kwa kila mkoa limekuwa likitumiwa na serikali kama mkakati wa ajira kwa kila mtanzania. Kwa hili tuna hoja mbili. Kwanza, shilingi bilioni moja ni pesa kidogo kuweza kuondoa umasikini kwa staili ya kumgawia kila mtanzania, hii inatokana na ukweli kuwa, Mkoa kama wa Dar es Salaam, una wakazi takribani milioni moja wanaohitaji mikopo. Kama kila anayehitaji atapata hii ina maana kwamba kila anayehitaji mkopo atapata shilingi elfu tatu (3000). Vijana wa CHADEMA tunasema kuwa shilingi elfu tatu zikitolewa kwa kila mtanzania haziwezi kumkwamua mtanzania kuondokana na umasikini.
Pili, fedha hizo zimekuwa zikiambatanishwa na itikadi za kisiasa kama ambavyo fedha za benki ya dunia kupitia programmu ya TASAF zinavyotangazwa na viongozi wa CCM kuwa zimetolewa na chama hicho. Pia tumesikitishwa sana na kitendo cha Mheshimiwa Rais kuamua kuteua wajumbe wa CCM tu kusimamia suala zima la mikopo. Vijana tunasema kuwa huu ni mfano mbaya kwa kiongozi anayehubiri umoja wa kitaifa, na bila shaka hata vitendo vya wajumbe wa CCM mikoani kuihusisha mikopo hiyo na CCM ni kielelezo kuwa wanafuata nyayo za Mwenyekiti wao ambaye ndiye rais wetu.