UTANGULIZI
Sisi vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo “CHADEMA” tuliokutana katika warsha ya “Vijana na Siasa” iliyofanyika Oktoba 20 mpaka 21 mwaka 2006 katika Hoteli ya Beach Comber mkoani Dar es salaam, kwa pamoja, tunachukua fursa hii kutoa tamko maalum kwa umma wa watanzania, kwa serikali na kwa CHADEMA juu ya masuala nyeti yanayohusu taifa na chama hiki.
Tamko hili ni matokeo ya kushiriki kwetu kikamilifu kwenye warsha ya “Vijana na Siasa” ambayo zaidi ya mafunzo, ilitupa wasaa wa kujadili kwa kina changamoto zinazolikabili Taifa na chama hususani katika muktadha wa ustawi wa vijana. Tunaongozwa na hiari na utashi wetu kutoa tamko hili, tunashawishiwa na umakini wetu kutetea vijana wa nchi hii, na tunashinikizwa na uzalendo wetu kwa taifa letu kuwajibika namna hii. Adhima yetu ni kuamsha fikra na tumaini jipya katika nafsi za wananchi wenzetu, ili tufikie mustakabali mufawadha wa Taifa letu – Naam, Taifa la Tanzania. Kwa jinsi hii, tunabainisha mapungufu na kutoa mwelekeo katika masuala yafuatayo.
MWELEKEO WA VIJANA NA TAIFA
Kimsingi, Vijana wa CHADEMA tumebaini kuwa tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani, mwelekeo wa maendeleo ya vijana na taifa umekuwa mashakani. Serikali imeendelea kupiga kampeni badala ya kutekeleza kwa vitendo ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Ikumbukwe kuwa CCM kiliongoza kwa kutoa ahadi nyingi kupitia ilani yake ya uchaguzi na ahadi nyingi zaidi zilitolewa na raisi, ambazo kimsingi zilikuwa nje ya ilani ya chama chake kama alivyokiri mwenyewe wakati akihutubia mkutano mkuu wa chama chake kwa kuziita kuwa zilikuwa ni ahadi za papo kwa hapo. Ahadi hizi hazikuishia hapo, Mheshimiwa Rais aliendelea kutoa ahadi lukuki kila alipokuwa akitembelea wizara mbalimbali sanjari na kutoa maagizo ambayo hata hivyo mengi ya maagizo hayo hayajatekelezwa licha ya muda alioutoa kwisha na mengi hayakutolewa ufafanuzi wa muda ili kuweza kupima.
Kwa hali hii serikali ya awamu ya nne imeendelea kupiga kampeni badala ya kuongoza nchi. Tunaendelea kusisitiza kauli ya Baraza kuu la CHADEMA kwa serikali kuwa wakati wa kampeni ulishakwisha, watanzania tunataka utekelezaji. Ni dhahiri kuwa serikali haina uhakika kama ni ahadi gani na ni ahadi ngapi imekwishazitoa mpaka sasa, lakini kubwa zaidi tuna wasiwasi na umakini wa serikali yetu kama kweli ina mkakati wa kutekeleza kile inacho ahidi. Msingi wa hofu yetu umejikita katika masuala kadhaa ambayo serikali yetu imeshindwa ama kuyatolea ufafanuzi au kuyapatia ufumbuzi licha ya kuwa na umuhimu.