CHADEMA YAIOMBA TFF ISHIRIKISHE
WADAU WENGINE KAMATI YA STARS
Utangulizi
Awali ya yote CHADEMA tunapenda kutoa pongezi zetu za dhati kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa kazi nzuri walioifanya kuhakikisha wanaifunga timu ya Bokina faso siku ile ya Septemba2, 2006.
CHADEMA tunaamini kuwa ulikuwa mwanzo mzuri na kwamba uwezo wa kushinda zaidi tunao, Na hivyo uwezo wa kufikia malengo ya kushiriki na kushinda katika fainali za kombe la Afrika mwaka 2008 na hatimaye kombe la Dunia mwaka 2010 tunao.
Hivyo tunapenda kuwatia shime vijana wetu wa timu ya Taifa, Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Serikali na wadau wengine wa soka ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa mstari wa mbele kushiriki kuchangia ili kuifanya timu yetu ya Taifa ifikie malengo bila wasiwasi wowote.
Kwa upande mwingine , CHADEMA tunaamini kuwa Soka ni moja ya nyenzo muhimu katika kujenga na kudumisha utaifa wetu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mchezo huu unapendwa na kugusa hisia za watu wengi bila kujali Imani zao za dini, Itikadi za kisiasa, Asili n.k
Kwa msingi huo basi, Tunategemea watanzania wote, TFF, Serikali na wadau wengine kuwa tutashirikiana na kushirikishana kwa moyo wa dhati bila kujali imani zetu wala itikadi zetu bali dhamira zetu kama wazalendo wa nchi hii, kwa kuzingatia kuwa kinachotuunganisha hapa ni utaifa wetu.