Kaimu mkurugenzi wa wanawake wa CHADEMA Mama Suzan Kiwanga ameunga mkono kwa niaba ya wanawake wa CHADEMA tamko la wanaharakati la kumkosoa Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete juu ya ushiriki wake kwenye sherehe za kimila za Swaziland ambapo mfalme wa nchi hiyo hupata fursa ya kuchagua mke bikira kila mwaka.
“Nimeamua nitoe tamko kwa niaba ya wanawake wa CHADEMA kuhusu suala hili baada ya kuona kuwa wanaharakati wanashambuliwa sana kwenye vyombo vya habari kupitia makala mbalimbali kuhusu suala hili. Napata hisia kwamba kuna mkakati wa kumsafisha na kumtetea mke wa rais. Napata hisia hizi kwa kuwa makala nyingi zinaandikwa bila hata ya majina ya waandishi kuandikwa.”
“Pamoja na kuwa mwanasiasa mimi ni mwanaharakati. Sasa ninapoona wanaharakati wanalalamikiwa katika masuala yenye maslahi kwa taifa sidhani kama kunyamaza itakuwa ni kutenda haki.”
“Lakini pia ndani ya hili tukio kuna masuala yanayohusu haki za vijana wa kike ambayo nimeshauriana na wanawake wenzangu na tumeona ni vyema tukazungumzia suala hili."
“Wanaomtetea Mama Kikwete wanaotoa hoja mbili kubwa. Mosi, wanasema wanaharakati wanalaumu yanayofanyika Swaziland lakini hawasikiki wakilaumu vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa kwa vijana wa kike kwenye baadhi ya mila zetu ambazo wanazitaja mathalani ukeketaji, ndoa katika umri mdogo nakadhalika”.
“Wanaotoa kauli hizi hawawatendei haki wanaharakati. Wanapaswa kufahamu FEMACT ni muunganiko wa zaidi ya mashirika 50 yasiyo ya kiserikali ambayo yanafanya kazi mbalimbali zinazoheshimika katika jamii yetu. Yapo ambayo yanafanya kazi ya kuchochea elimu kwa katika jamii za wamasai na mengine yachochea maadili kwa ujumla. Yapo ambayo yanapiga vita ukeketaji na mila nyingine zenye madhara. Nani hafahamu mchango wa mashirika kama TGNP katika kutetea jinsia na haki za wanawake? Wanapaswa kukumbuka kwamba hata sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 (SOSPA) ambayo inakataza uzalilishaji wa kijinsia ilitokana na msukumo wa wanaharakati wa mashirika kama TAMWA na mengine ambayo ni wanachama wa FEMACT.”
“Hivyo wanaharakati walipomkosoa Mama Kikwete ni katika kuhakikisha kwamba viongozi wetu hawawi sababu ya kuweka mazingira ya kurudisha nyuma jitihada hizo ama kuhalalisha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika nchi nyingine. Ipo mikataba ya kimataifa kuhusu masuala haya ambayo Tanzania pia imeridhia hivyo tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuonyesha mfano wa kuigwa.”
“Hapa Tanzania wanaharakati wamekuwa wakiikosoa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwamba ina ruhusu ndoa katika umri mdogo. Hivi karibuni wizara ya sheria imetoa msimamo wakati wa maadhimisho ya Kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) kwamba sheria hii itafanyiwa marekebisho. Vipi mwanamke wetu wa kwanza kabisa (First lady) awe kiti cha mbele kushuhudia mabinti wadogo wakiozwa. Hii inatofauti gani na kwenda kushuhudia kijijini Tanzania ‘ngoma ya chakulaga’ ambayo wanaharakati wanakaribia kuitokomeza kutokana na kuchochea mazingira ya maambukizi ya UKIMWI?”. (Chakulaga ilikuwa ni ngoma ya wasukuma ambao mabinti walikuwa wanacheza ngoma na wanaume wanapita kuchagua wanaocheza vizuri zaidi huku wakiwa na mavazi ya wazi na kuwachukua kuwa wapenzi wao). "
“Lakini hata kama ingekuwa kweli kuwa wanaharakati wapo kimya kuhusu masuala ya unyanyasaji wa vijana wa kike nchini ama masuala mengine ya uvunjaji wa maadili hatuwezi kutumia kosa moja kuhalilisha kosa lingine.”
“Sababu ya pili inayotolewa ni kwamba Mke wa Rais asingiweza kukosoa au kuacha mwaliko huo kwa manufaa ya kidiplomasia.”
“Sikubaliani kabisa na hiki kisingizio. Sina nia ya kusema kwamba Mama Kikwete angepaswa kwenda na kuwakosoa wa Swaziland mbele ya mfalme wao. Huku ndiko kungekuwa kusababisha mgogoro wa kidiplomasia usio na lazima. Lakini tukumbuke kwamba Mama Kikwete hakushiriki tukio hilo kwa kuhamakishwa (by surprise). Laiti kama angekuwa yuko kwenye msafara wa rais halafu akaalikwa kwenye dhifa na bila kutegemea kukawa na tukio hilo hapo walau kidogo utetezi huo ungekuwa na mantiki. Lakini yeye alipewa mwaliko rasmi akijua kabisa ni wa sherehe ya kuchagua wanawari. Akapanda ndege ya rais ambayo inatembea kwa gharama kubwa kwenda kuhudhuria sherehe hii. Haya ni matumizi ya anasa. Hivi kama Mama Kikwete angetoa udhuru kwamba hataweza kushiriki sherehe hizo kutokana na kutingwa na majukumu mengine ya kitaifa angesababisha mgogoro gani wa kidiplomasia? Hivi kama badala ya kwenda Swaziland angepanga ratiba ya kwenda katika jamii za wafugaji kuhamasisha watoto wa kike kupelekwa shule angeingia katika mgogoro gani wa kidiplomasia? Na je, Tanzania ina manufaa gani makubwa ya kidiplomasia na Swaziland kiasi cha kuingia gharama zote hizo?”
“Mimi nilikuwa mmoja wa watu ambao tulivutiwa sana na ujumbe wa Mama Kikwete wa kupiga vita UKIMWI ‘kwamba mtoto wa mwenzio ni wa kwako-mlinde’. Lakini tukio hili kwa kiasi kikubwa limekinzana na kauli hiyo nzuri. Hapa sidhani kama Mama Kikwete alijali kwamba watoto wa kiswaziland ni watoto wake na kwenda ‘kuwalinda’.”
“Nadhani wakati umefika wa Mama Kikwete mwenyewe kutoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wake katika sherehe hiyo ya kimila ambapo mfalme huchagua mke bikira hiyo na manufaa ya safari ya safari yake ya Swaziland kwa ujumla.”
Suzan Kiwanga
Kaimu Mkurugenzi wa Wanawake-CHADEMA