Viongozi wake wengi hususani Makamba ni waumini wa rushwa
Tumeamua kutoa tamko leo hii kufuatia taarifa za vyombo vya habari kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM, kimezindua utaratibu wa kupambana na rushwa ndani ya chama chao kwa kutenga siku maalumu ya kuzungumzia rushwa katika ngazi ya shina mpaka taifa kama ilivyoelezwa na Katibu Mkuu wa CCM, Mh Luten Yusuph Makamba, ambaye alidai mpango huo una lengo la kukitakasa chama hicho dhidi ya rushwa.
Kuzinduliwa kwa mpango huu kunazua maswali mengi zaidi kuliko majibu, na kama wanavyodai kuwa wanaanzisha vita dhidi ya rushwa basi sisi tunaamini vita hivyo havina wapambanaji na hivyo vitashindwa kama ambavyo wameshindwa katika miradi mengine ya chama hicho na hata ya Taifa.
Lakini pili, tumeshangazwa kuona watu ambao tuna hakika na ushahidi wa kutosha kuwa walingia madarakani kwa rushwa halafu wageuke wapambanaji wa rushwa. Sisi tunaamini huo ni unafiki, ni kuwalaghai watanzania na kuwafanya wananchi hawajui nini kilitokea na hatimaye nini kitaendelea.
Lakini kubwa zaidi, tunaamini kuwa kikwazo kikubwa cha mpango huo ni kwamba viongozi wa juu wa Chama hicho ni waumini wa rushwa kupindukia.
Tunamfahamu Makamba, tuna hakika hawezi kusimamia mkakati wa kupambana na rushwa, Tunapenda kuwa kumbusha watanzania kuwa Makamba anayedai kuongoza mkakati huo wa kupambana na rushwa binafsi ameshiriki vitendo vya rushwa tena hadharani na ushahidi tunao.