Katika uchaguzi wa mwaka 2000, kati ya kata 13, CHADEMA kilishinda kata 9 huku CCM ikiambulia chini ya nusu ya viti tulivyovipata yaani viti 4 na hivyo kufanikiwa kuiongoza halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Na katika uchaguzi wa mwaka 2005, CHADEMA kilishinda katika ngazi ya ubunge na zaidi kiliendelea kukishinda CCM kwa idadi kubwa ya madiwani kwani CHADEMA kilipata madiwani 11 dhidi ya madiwani 8 wa CCM.
Katika mazingira ya chaguzi za nchi yetu ambapo wakati wa uchaguzi CCM inatumia vyombo vya usalama na viongozi wote wa serikali , katika mazingira ya chaguzi zetu ambapo tume ya uchaguzi sio huru na hupendelea chama tawala, kukishinda Chama cha mapinduzi katika ngazi ya ubunge katika chaguzi zote na kushinda halmashauri mara mbili kati ya mara tatu hata kama ingekuwa kwa kura moja bado ni ushindi mkubwa kutokana na ukweli kuwa serikali kwa kushirikiana na chama tawala wamekuwa wakifanya ghiriba na uzandiki wa hali ya juu kupinga utashi wa wananchi.
Hivyo basi tunamuomba Mh Makamba aache propaganda kuuhadaa umma unaeolewa fika kuwa Karatu ni ngome ya CHADEMA hata pale Chama cha Mapinduzi kinapotumia nguvu ya dola sanjari na mifumo mibovu ya chaguzi zetu na badala yake aelimishe jamii juu ya namna CCM inavyopoka ushindi kwa nguvu ya dola kila uchaguzi.
Kwa upande wa pili CHADEMA tunapenda kumfahamisha Makamba kuwa wakazi wa Karatu na wananchi kwa ujumla hawahitaji CCM ishindanishwe na CHADEMA kwa vigezo vya idadi ya kura hata kama katika eneo hilo pia CHADEMA ipo juu ya CCM,
Wanachotaka kusikia wananchi ni mashindano ya kati ya CHADEMA na CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo, wananchi hawana njaa ya takwimu za kura bali maendeleo.
CHADEMA tumeshinda halmashauri ya Karatu mara mbili, na sasa tuna miaka mitano tangu tuanze kuongoza halmashauri hiyo na mabadiliko ya kweli yameonekana katika maisha ya wanakaratu kama ifuatavyo ukilinganisha na miaka arobaini ya uongozi wa CCM kama ifuatavyo.
Kwa muda wa miaka mitano, CHADEMA tumejenga shule za sekondari kumi dhidi ya shule moja ya sekondari iliyojengwa na CCM kwa miaka arobaini
Kwa kipindi cha miaka mitano ya CHADEMA Karatu, tumejenga miradi 35 katika vijiji 45 dhidi ya mradi mmoja tu wa CCM katika vijiji 45 katika miaka arobaini ya utawala wa CCM
Pia kwa miaka mitano ya CHADEMA, tumejenga zahanati 9 kati ya 7 zilizojengwa na CCM kwa miaka 40. Na zaidi kwa muda wa miaka mitano CHADEMA kimeweza kujenga barabara zilizoshindikana katika utawa la wa miaka arobaini ya CCM, mfano halisi ni ujenzi wa barabara inayotoka Makhoromba kwenda Mangola.
Haya ndio mambo ambayo wananchi wa Karatu wanahitaji kuyasikia, na sio kupiga propaganda tu huku wananchi wanataabika.