Katika Gazeti la Mtanzania la Jumamosi Novemba 25,2006 kuna habari katika ukurasa wa 3 yenye kichwa cha habari ‘Tanzania yawashangaza vijana wa Afrika’. Katika habari hii amenukuliwa Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Mheshimiwa John Chiligati akieleza sifa ambazo Tanzania imepewa kwa kuwashirikisha vijana katika vyombo vya maamuzi. Katika habari hiyo waziri ametoa takwimu mbalimbali kuhusu ushiriki wa vijana kwenye vyombo vya maamuzi ambazo ndizo zimetumiwa kama kigezo cha Tanzania kuonekana nchi ya kusifiwa katika kuwashirikisha vijana kwenye vyombo vya kutoa maamuzi. Sehemu kubwa ya takwimu ambazo amezitoa hazilingani na ukweli na kwa hivyo kupotosha vijana na watanzania. Kwa vyovyote vile takwimu hizi zikichukuliwa zilivyo zinaweza kupunguza jitihada za vijana, serikali na mashirika ya kimataifa kama UNICEF za kuhakikisha vijana wanashiriki na kushirikishwa katika vyombo vya maamuzi. Katika habari hiyo waziri amenukiliwa akisema: Mosi, Kwamba Tanzania imetenga nafasi maalum kwa ajili ya vijana bungeni, Pili, kwamba vijana sasa ni asilimia 60 katika mabaraza ya madiwani, Tatu, kwamba kuna vijana 30 katika bunge letu na Nne; kwamba vijana ni asilimia 10 ya bunge nzima. Takwimu hizi zote haziendani na ukweli wa hali halisi iliyopo.
Kwanza tuweke bayana kwamba kwa mujibu wa sera ya taifa ya vijana ya mwaka 1996 ambayo ndiyo inayotumiwa na wadau wengi kijana anatafsiriwa kwa muktadha unaotumiwa pia na Umoja wa Mataifa wa miaka 15 mpaka miaka 24. Hatahivyo, hivyo serikali imekuwa ikitamka mara kwa mara toka mwaka 2002 kwamba imeifanyia marejeo(review) sera hii na kwamba sera ya sasa ya vijana(ambayo mpaka sasa haijasambazwa kwa wadau wengi) inatafsiri kwamba vijana ni watanzania wenye kati ya miaka 15 na 35. Tafsiri hii ya umri wa ujana inatumika katika nchi kadhaa za Afrika na ndiyo tafsiri pia iliyomo katika sera ya vijana ya CHADEMA. Hivyo tunaamini kwamba wakati waziri anatoa taarifa yake alitumia tafsiri ya ujana ya serikali ya sasa ya miaka 15 mpaka 35.
Ukweli ni kuwa hakuna nafasi na viti maalum vilivyotengwa na serikali katika bunge letu tukufu ambavyo ni maalum kwa vijana. Mfumo wa kikatiba na kisheria wa nchi yetu umetenga viti maalum kwa ajili ya wanawake pekee. Kilichopo hivi sasa ni vyama vyenyewe vinapopewa viti maalum vya wanawake huchagua kwa mujibu wa vigezo ambavyo vimejiwekea. Mathalani CHADEMA iliweka kipaumbele katika kuteua wabunge vijana wa viti maalum(wanaowakilisha pia maeneo waliyotoka) ambapo vijana kama Mhonga Said na Halima Mdee wameteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum wanawake. Aidha CCM imetenga viti maalum vya wanawake vijana ambapo Waheshimiwa Lucy Mayenga na Amina Chifupa wameteuliwa kupitia chama hicho.