Majeshi yetu tumeyarithi kutoka kwa mkoloni na kwa bahati mbaya baadhi yao bado yana ule mfumo wa utiifu (blind obedience) aliyekuwa anatarajia mkoloni kutoka kwao! Hisia za wananchi kwa baadhi ya vyombo hivi hasa Polisi na Magereza zimebaki kama ilivyokuwa kabla ya uhuru kwamba vyombo hivyo ni adui wa raia! Wananchi wanashambuliwa na polisi kwa maagizo ya wakubwa wao wa kazi wanaopokea amri zenye mnuko wa kisiasa kuliko ule wa kisheria.
Sera ya CHADEMA inajaribu kubadilisha imani, mwelekeo na maadili ya vyombo hivi ili imani ya wananchi irudi kuwa vyombo hivi vipo kwa manufaa yao na siyo kwa sababu tu ya kuwasumbua, kuwaumiza na kuwaswaga kifungoni kila wapendapo au wanapoamriwa. Vilevile inakusudia kuboresha hali duni ya wafanyakazi wa vyomho hivi. Afisa mwenye njaa kali hataacha kutumia cheo na wadhifa wake kudai na kupata rushwa kutoka kwa mwananchi. Vipi basi mwananchi huyu ataamini kuwa Afisa huyo na jeshi lake ni RAFIKI WA RAIA?