|
WATANZANIA TUKUBALI KUWA KUNAHITAJIKA KUWEPO MABADILIKO
KATIKA MFUMO NA MUUNDO WA TAWALA ZA MIKOA!
TUONDOKANE NA “MAZOEA TU”
Miaka 44 sasa baada ya nchi yetu kuwa huru, hatuna haja wala ulazima wa kuendelea kukumbatia mfumo na muundo wa Tawala za Mikoa
tuliorithi kutoka kwa wakoloni. Ni muundo wa kuwa na mamlaka (Rulership) juu ya watu kama ilivyokuwa wakati wa Tanganyika ya
Ukoloni. Utawala wetu sasa unatakiwa kuwa wa kuongoza watu (Leadership).
Nyakati za mfumo wa siasa za Chama Kimoja na Dhana ya Chama
kushika hatamu za utawala wa nchi, muundo wa tawala za mikoa
uliendelezwa kwa maslahi ya kiitikiadi. Wakati huu wa zama na udikiteta wa kisiasa, muundo huu
ulitumika kuunganisha mamlaka
na madaraka ya utawala na shughuli za chama. Kwa ajili hii chama kiliweza kudhibiti Nguvu ya Umma kwa kuwanyima watu fursa ya
kupata na kujua maoni na mitazamo tofauti ya kisiasa. Chama kilichukua nafasi ya kuwa kiunganishi cha jamii ya Watanzania
badala ya serikali. Serikali ilifanywa chombo cha kutumiwa na chama badala ya kuwa chombo cha watu, raia huru wa nchi.
Leo CCM na Serikali zake vinatetea na kuukumbatia mfumo na muundo huu kwa maslahi ya kisiasa tu na siyo kwa sababu ya ufanisi
wa kuwaendeleza wananchi kimaisha. Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kama watu binafsi hawawezi kuwaendeleza watu zaidi ya
kuwatawala.
Serikali za Mitaa na siyo Tawala za Mikoa ndilo jibu sahihi katika kuleta ufanisi wa kuwaendeleza Watanzania. Wakuu wa Mkoa
na Wakuu wa Wilaya wako na wanajishughulisha zaidi na maslahi ya kisiasa ya chama chao na ndio maana uteuzi wao ni wa kiitikadi
zaidi ya taaluma, ujuzi na uzoefu wa maswala ya utawala. Ni vema ikumbukwe kuwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ndiyo nguzo za kuwezesha
CCM kushinda uchaguzi. CCM na Serikali zake hawako tayari kuzifanya nyadhifa hizi kuwa za kitendaji katika utumishi Serikalini.
Hii ni kwa sababu wanaogopa kupoteza nguvu hii kubwa ya kisiasa.
|