13/5/2007
Ref. No. C/HQ/ADM/SG/25/07
Mkurugenzi Mkuu
Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU)
Dar es Salaam
Ndugu:
TAKURU INALINDA NA KUTETEA RUSHWA?
Tunakuandikia barua kuomba ufafanuzi juu ya taarifa/kauli hizi ambazo wewe mwenyewe ama ofisi yako ilizitoa ambazo zikiachwa ziendelee kama zilivyo kwa maoni yetu zinaidhalilisha TAKURU na hatimaye kukwamisha mapambano dhidi ya Rushwa:
- TAKURU kuisafisha kampuni ya RICHMOND. “….hakuna ushahidi wowote uliopatikana kuthibitisha vitendo vya rushwa, uzembe na upokeaji wa kamisheni watendaji wa serikali….uchunguzi huo umethibitisha udhaifu wa kawaida katika utendaji na ambao haukuhusisha rushwa au manufaa ya aina yoyote ile kwa upande wa watendaji na hakuna hasara iliyosababishwa na udhaifu huo”(Mwananchi 12/5/2007). “….baada ya kuona hivyo, Richmond ilionekana kufahamu mwenendo wa mambo serikalini…”(Tanzania Daima 12/5/2007). Maswali ya kujiuliza: Ni kwanini Kamati ya Waziri Mkuu iliipa tenda Richmond baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kuitaka bodi yake ya sabuni kutangaza upya zabuni hiyo kwa kutimia zabuni za kimataifa? Richmond kuweza kufahamu mwenendo wa mambo ya ndani serikalini sio ishara ya rushwa ya kimadaraka? Ni kweli kama hakuna hasara iliyosababishwa na uamuzi huu wakati ambapo watanzania wamekaa bila umeme kwa miezi mingi bila kupata umeme wa dharura waliotarajia wakati wa dharura, Rais amekiri kwamba umeme ulichangia kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi na hata kuongeza mfumuko wa bei na mpaka leo bado megawatts 100 hazijatimizwa na Richmond/Dowans? CHADEMA tunaitaka TAKURU itupatie nakala ya ripoti ya uchunguzi wa TAKURU kuhusu Richmond na iweke wazi ripoti yote kwa umma.
- Wiki iliyopita umenukuliwa ukitamka kwamba TAKURU haitaliendeleza suala la kuchunguza tuhuma za Wabunge hususani wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kupewa Rushwa kama zilivyotolewa na Mheshimiwa Philemon Ndesamburo, Mbunge wa Moshi Mjini(CHADEMA) eti kwa kuwa spika alishafunga mjadala wa suala hilo bungeni.
- Kwamba “Mwenyekiti wa Taifa(CHADEMA), Freeman Mbowe alipotosha umma wakati wa ziara yake mwanzoni mwa mwaka 2007 aliposema kwamba Rais ametamka kuwa amepokea orodha ya wala rushwa na kwamba TAKURU inawasafisha wala rushwa”. Ofisi yako ilichapa matangazo kwa gharama za walipa kodi kukanusha kwamba Rais hajawahi kupokea orodha ya wala rushwa na kwamba TAKURU haiwasafishi wala rushwa. Miezi michache baada ya tamko lenu, Rais Kikwete amesema tena hadharani kwamba amewahi kuletewa orodha ya wala rushwa. Ofisi yako haijawahi kujitokeza tena mpaka sasa kukanusha kauli ya Rais ama kukiri kwamba palikuwa na makosa katika kauli ya awali ili kurudisha imani.
- Mara baada ya Mkurugenzi Mkuu mpya kuingia madarakani ulinukuliwa mwishoni mwa mwaka kwamba wala rushwa wajiandae unawapa kipindi cha sikukuu za Noeli(Xmas) na mwaka mpya na mara baada ya hapo wananchi wategemee maamuzi mazito juu yaw ala rushwa. Mpaka sasa ni Mwezi Mei, Ofisi yako haijazikanusha kauli hizi za kuwapa muda wala rushwa wala haijaeleza ni maamuzi/hatua gani kubwa zilizochukuliwa kama ilivyoahidiwa.
Rushwa ni kosa la jinai, rushwa ni adui wa haki. Kauli za kuwapa wala rushwa muda ama kukataa kuchunguza rushwa ni ishara ya kulinda uhalifu ambayo ni kinyume cha sheria kwa raia wa kawaida na hata taasisi za umma. CHADEMA, ikiwa ni chama cha siasa mbadala ni mdau muhimu katika kuchochea uwajibikaji wa serikali na vyombo vya haki na hatimaye kuchochea utawala bora, demokrasia na maendeleo. Ni katika muktadha huu tunakuandikia kutaka ufafanuzi rasmi asili na nia kauli hizi ili ambazo zinaelekea kuidhalilisha taasisi ili tuendelee kuwa na imani na Taasisi ya Kuzuia Rushwa(TAKURU). Kauli ya TAKURU kuacha kuchunguza suala la rushwa kwa sababu tu kiongozi mmoja ametamka kufunga mjadala kuhusu suala hilo ni ishara ya chombo hiki kufanya kazi kwa kuingiliwa na watu ama vyombo vingine na ni kinyume na dhana ya uhuru wa taasisi ya kupambana rushwa ambayo wadau mbalimbali tunaisimamia. Kama uratibu huu wa TAKURU kuacha kuchunguza rushwa kwa sababu tu ya kauli ya kiongozi mmoja basi mapambano dhidi ya rushwa yatakuwa mashakani. Mathalani, Je TAKURU ingeacha kuchunguza tuhuma za rushwa katika mkataba wa RICHMOND/DOWANS kwa sababu tu waziri Mkuu alitamka kwamba watanzania tusiendelee kujadili kampuni hiyo kwa sababu mvua zimenyesha na kwa sasa tunapata umeme ?
TAKURU inapaswa kuendelea kuwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa na si Taasisi ya Kulinda, Kusafisha ama Kutetea Rushwa.
Wako katika ujenzi wa Taifa
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa
Nakala:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Spika-Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Vyombo Vya Habari