Mapendekezo ya Muungano wa Vyama
Mitazamo kadhaa ya Vyama vya Upinzani Kushirikiana
Pendekezo la Pili:
KUSHIRIKIANA KABLA YA UCHAGUZI
- Katika utaratibu huu vyama vyenye nia ya kushirikiana ili kuingia katika uchaguzi dhidi ya chama kinachotawala vinakubaliana kuweka mgombea mmoja kuwakilisha vyama vyote katika ngazi ama zote au kadhaa.
- Vyama vyaweza kushirikiana kwa kuweka mgombea mmoja katika ngazi ya urais na kugawana majimbo ya ubunge na kata za udiwani. Hapa chama kimojawapo kinatoa mgombea Urais na mgombea mwenza na pia majimbo na kata zinagawiwa miongoni mwa vyama vinavyoshirikiana.
- Vyama vyaweza kushirikiana katika ngazi ya majimbo na kata tu na kila chama kuweka mgombea wake wa urais. Hii inawezekana kwa kugawa nchi kwa mujibu wa halmashauri za wilaya/Miji/Manispaa/Jiji na kisha majimbo na kugawana miongoni mwao Wilaya hizo. Lengo la njia hii ni kuhakikisha kutawala Halmashauri na kushinda jimbo au majimbo yaliyopo katika Halmashauri husika.
Hatua za kuchukua:
- Viongozi wa vyama vyenye nia ya kushirikiana kukutana na kuunda kamati ya ufundi itakayoshauri njia mwafaka na taratibu za kushirikiana. Kamati ya ufundi itaandaa mkataba wa kisheria wa ushirikiano utakaoweka bayana muundo wa ushirikiano ikiwemo vikao vya kisheria vya kutatua migogoro itakayotokana na ushirikiano.
- Mkataba wa ushirikiano uridhiwe na vikao halali vya vyama husika.
- Mkataba uunde bodi ya uchaguzi ya vyama vinavyoshirikiana itakayokuwa na wajumbe sawa kutoka kila chama. Bodi hii iwe ni ya kitaifa na pia kila wilaya iwe na bodi hii.
- Kama ushirikiano unahusu wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, vikao vya utetuzi vya vyama vinavyoshirikiana vikae sambamba ili uteuzi ufanyike wakati mmoja. Hii itasaidia sana kuondoa migogoro miongoni mwa vyama.
- Mkataba uoneshe makubaliano ya majimbo na kuruhusu bodi za uchaguzi za wilaya kukubaliana kuachiana kata.
- Bodi iwe na nguvu kubwa ya kuamua wagombea na kupendekeza kwa vikao vya vyama ili kuhakikisha hakuna jimbo linalopita bila kupingwa.
Faida za Pendekezo la Pili
- Vyama vitapata uwakilishi mkubwa katika vyombo vya maamuzi - Mabaraza ya madiwani na Bungeni. Hili litatokea kwa sababu kura za wananchi hazitakuwa zimegawanyika kwa vyama tofauti.
- Kila kura ya Mtanzania itakuwa na heshima kwani itachangia sana kwa ushindi badala ya kupotea.
- Itasaidia vyama vidogo kupata uwakilishi bungeni na hatimae kupata ruzuku za kujiendesha.
- Iwapo mgombea mmojawapo wa upinzani atakuwa ameshinda kiti cha Urais ataweza kuunda serikali bila tatizo na kuteua Waziri Mkuu kutokana na wabunge wa upinzani waliopo ndani ya Bunge na pia kuteua mawaziri [Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara 51(1)(2) na 55(4)].
- Iwapo Rais atatoka katika chama kinachotawala, lakini wabunge wengi wanatoka vyama vya upinzani ushirikiano utaweza kuhalalisha serikali ya mseto (rejea ibara za katiba hapo juu).
- Inakwepa hasara zote za Pendekezo la kwanza
Hasara za Pendekezo la Pili
- Vyama kugeuka vya kikabila na kikanda na hivyo kuigawa nchi na kuhatarisha umoja na mshikamano wa nchi.
- Vyama vikubwa kutokukua kufuatia kufungiwa katika eneo moja la nchi.
- Kudumaa kwa demokrasia kwa kuminya wigo wa chaguo kwa wananchi.
- Uwezekano wa migogoro katika kuachiana majimbo. Wagombea kutoka vyama vilivyo katika ushirikiano kutokubaliana nani agombee kwa chama kipi.
- Kupoteza faida za pendekezo la kwanza na hasa ile ya kuunda chama kimoja cha upinzani chenye nguvu.
CHADEMA INASEMAJE?
Kwa kuzingatia uchambuzi wetu hapo juu tunapendekeza kama ifuatavyo:
- Kwa lengo la muda mrefu la kuimarisha demokrasia nchini Tanzania, vyama vikubaliane
kuungana na kuwa chama kimoja kikubwa chenye nguvu. Hata hivyo,
muda huu sio mwafaka kwani ni muda wa uchaguzi. Badala ya kutumia
muda mwingi kuweka mikakati ya kuungana na kushiriki vikao vya kuungana
ambavyo ni virefu sana, muda utumike kuweka mikakati ya ushindi
katika uchaguzi Mkuu 2005. Hivyo mazungumzo ya kuunganisha vyama
yafanyike mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
- Kwa lengo la muda mfupi ambalo pia litapelekea vyama kuungana baada ya uchaguzi
mkuu 2005, tunapendekeza vyama kushirikiana katika maeneo yafuatayo:
- Kamati ya ufundi ianze kutafuta fedha za kuwezesha mazungumzo na shughuli za ushirikiano.
Waasisi wa CHADEMA waliamini kwamba ni lazima nguvu za upinzani ziunganishwe ili kuwa na umoja wenye nguvu utakaoweza kupambana na CCM. Katika uchaguzi wa 1995 CHADEMA kilishirikiana na NCCR-Mageuzi baada ya vyama vingine kujiengua kwenye muungano wa wapinzani katika dakika za mwisho. Hata hivyo kambi hii iliweza kushika nafasi ya pili katika uchaguzi huo. Mwaka 2000 CHADEMA tena kilishirikiana na CUF baada ya vyama vingine kususia muungano. Vilevile kambi hii ilishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo.
Watanzania wanataka vyama kuungana. Kuna ugumu sana kwa vyama kuungana na hata kushirikiana lakini uzoefu wetu unaonyesha kwamba hili linawezekana kama nia thabiti ipo. CHADEMA inasisitiza kwamba wananchi wapewe kile wanachokitaka. Tushirikiane ili kukidhoofisha chama tawala. Tutafaidika zaidi katika kushirikiana kuliko kutoshirikiana.