Mapendekezo ya Muungano wa Vyama
Mitazamo kadhaa ya Vyama vya Upinzani Kushirikiana
Huu ni mwaka wa uchaguzi. Vyama vimejipanga kwa ajili ya uchaguzi. Hata hivyo bado kuna kilio cha wananchi kutaka vyama vya upinzani kuungana au hata kushirikiana ili kukiondoa chama kinachotawala madarakani.
Hapa chini tunatoa mapendekezo ya jinsi ya kuungana au kushirikiana. Tunaomba mapendekezo haya yajadiliwe kwa kina na kuyaboresha ili tupate ushirikiano kwa faida ya wananchi.
Pendekezo la Kwanza:
CHAMA KIMOJA CHA KISIASA
- Vyama vyote vya siasa kuungana na kuunda chama kimoja cha siasa. Katika utaratibu huu, chama kipya inabidi kisajiliwe au moja ya vyama kubadili jina lake na katiba yake na vyama vingine vyote kujivunja na kujiunga na chama hiki chenye jina Jipya.
- Iwapo chama kimojawapo kilichopo kitajibadili ili kufungulia milango ya vyama vingine kujiunga nacho,inabidi si tu katiba kubadilika bali pia madhumuni na muundo wa chama hicho. Muundo wa chama ndio unaweza kukabili migorgoro kwani viongozi wa chama hiki wanaotokana na vyama vya zamani wataweza kujiona ni vipi nafasi zao za kisiasa zinakuwa katika chama kipya.
Hatua za kuchukua:
- Viongozi wa vyama vyenye nia ya kuungana wakutane na kuteua kamati ya ufundi ili kuandika katiba mpya, sera mpya na kuangalia muundo wa muda mfupi wa chama kipya (transitional leadership).
- Rasimu ya katiba mpya na muundo wa kipindi cha mpito kujadiliwa kwa kila chama chenye nia ya kuungana na kupitisha baada ya mapendekezo.
- Iwapo chama kinachoundwa ni kipya kabisa, vyama vyote vinatakiwa kujivunja kwa mujibu wa katiba zao na kuanza usajili wa chama kipya kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa (political parties act No.5) ya 1992.
- Iwapo moja ya chama kilichopo kinajibadili na kuwa chama kipya, inabidi chama hicho kiitishe Mkutano mkuu maalumu na kuridhia katiba mpya yenye jina jipya la chama na muundo mpya wa chama. Kisha Mkutano Mkuu wa chama kinachobadili jina kupitisha azimio la kipindi cha mpito cha uongozi.
- Wakati chama kinachobadili jina na uongozi kinapokuwa kinaridhia katiba mpya, vyama vingine vyote vinakuwa vinafanya mikutano yake sambamba ya kuvunja vyama vyao. Azimio la kipindi cha mpito litashughulikia masuala yote ya uongozi wa muda na uchaguzi wa viongozi wa chama kipya kuanzia ngazi za chini. Uongozi wa muda utahusisha viongozi wa vyama vyote vilivyoungana.
Azimio la kipindi cha mpito itakuwa ni kanuni ya kuongoza chama kipindi hicho wakati uchaguzi wa ngazi za chini unafanyika. Kwa ufupi Azimio hili litakuwa ni katiba ya muda inayosubiri utekelezaji wa Katiba mara baada ya muundo kukamilika. Kipindi hiki kwa mfano kutakuwa na Uongozi wa kubadilishana (Rotational leadership) miongoni mwa viongozi wa juu wa vyama vilivyoungana.
Faida za Pendekezo la Kwanza
- Kuwapo na chama kimoja chenye nguvu na rasilimali za kutosha (watu na fedha) kwani kitarithi rasilimali hizo kutoka vyama vilivyoungana.
- Kuwa na mgombea mmoja katika kila ngazi inayogombewa katika uchaguzi - Udiwani, Ubunge na Urais.
- Nguvu za wananchi kuwa pamoja na hivyo kuepuka mgawanyo wa kura.
- Kuwaridhisha wananchi kwani wamekuwa wakililia muungano wa vyama miaka nenda rudi.
- Kuimarisha demokrasia katika ngazi zote za uongozi - Vijijini, Mitaani, Halmashauri za wilaya na Bungeni.
- Kupata ruzuku nyingi zaidi kutokana na wingi wa kura (uwiano wa kura) na hivyo kupunguza takrima (rushwa) itolewayo na CCM.
- Kuwa na mtandao mpana zaidi wa chama kutokana na kurithi ofisi za vyama vilivyoungana.
Hasara za Pendekezo la Kwanza
- Vyama kupoteza viti katika mabaraza yote ya kutunga sheria isipokuwa chama kinachojibadili - Serikali za vijiji/Mitaa, Madiwani na Wabunge.
- Iwapo chama kipya kabisa kitaundwa, kuna hatari ya kunyimwa au kucheleweshewa kwa makusudi usajili wa kudumu na msajili aliyechaguliwa na CCM na hivyo kutoshiriki uchaguzi wa mwaka huu.
- Wanachama na viongozi (Baadhi) wa vyama vitakavyojivunja kukataa na hata kupelekea kesi kadhaa katika mahakama za Tanzania, hivyo mitafaruku itakayokatisha tamaa wananchi.
- Gharama kubwa za kutangaza na kujenga chama kipya. Vyama vilivyokaa muda mrefu na kujijengea umaruufu vitapotea kabisa na kazi kujenga jina jipya itaanza - inachukua muda mrefu sana kwa wananchi kuelewa, hasa wa vijijini ambao ni wengi.
- Vyama kupoteza mawasiliano (contacts) na marafiki na mashirika ya nje.
- Vita vya kugombea madaraka na nafasi ndani ya chama kipya vinavyoweza pelekea kupoteza watu wenye uwezo.
- Tutoweza kutekelezeka kwa muda mfupi kwani inahitajika imani ya hali ya juu sana.
- Kupoteza wanachama watakaokataa kujiunga na chama kipya.
- Kutokea kwa makundi ya watu watakaounda vyama kwa majina ya zamani ya vyama vilivyoungana na hivyo kukanganya wapiga kura.