Lengo la Serikali itakayoongozwa na CHADEMA ni kuunda Taifa la watu walio huru lenye kuzingatia misingi ya utawala bora na linalotoa fursa kwa wananchi wake kuboresha maisha yao. Ilani hii ya uchaguzi ni ahadi na mkataba wetu kwa wananchi wa Tanzania. Utekelezaji wa Ilani hii ndiyo utakaopelekea kuwa na Taifa tunalokusudia.
Ilani hii ni ilani ya uchaguzi kitaifa na inazungumzia mikakati ya kikazi kama CHADEMA itashinda uchaguzi na kuongoza dola. Vilevile ilani hii ndio itakayokuwa rejea yetu katika michango ya wabunge wa CHADEMA katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata kama si serikali itakayokuwa madarakani haitakuwa serikali ya CHADEMA. Kutokana na mwelekeo wa ilani hii, Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji zitatunga ilani zao ili kuelezea jinsi Mabaraza ya madiwani yatakayoongozwa na CHADEMA yatakavyoweza kushirikiana na wananchi katika mchakato wa kuleta maendeleo, kuimarisha demokrasia na kujenga Taifa linalokusudiwa. Ilani za CHADEMA za kila Wilaya zitagusia changamoto mahususi zilizopo katika wilaya husika.
Katika Ilani hii Tumegusia masuala machache ambayo CHADEMA inadhani ni muhimu sana katika kuirudisha Tanzania katika njia ya maendeleo. Haya ndiyo wanaCHADEMA tunaamini, kwamba yakifanyiwa kazi tutajenga Taifa la Watanzania walio huru, wasio waoga, wenye fursa ya kuboresha maendeleo yao. Tanzania yenye haki na isiyovumilia ugandamizaji wa aina yeyote kwa mwanamke au mwanaume wa Kitanzania.
Utangulizi
Mojawapo ya vigezo vya utawala mbaya ni sera mbovu. Kwa muda mrefu sasa Tanzania imepita katika vipindi tofauti vyenye
mielekeo na sera tofauti. Kuanzia mwaka 1967 hadi 1987 tukiwa chini ya utawala wa chama kimoja, Tanzania ilikumbatia itikadi
ya ujamaa na kujitegemea. Mpaka sasa ni dhahiri kwamba itikadi hii imeachwa na wenyewe wa CCM ingawaje bado imebakizwa
kwenye katiba na maneno ya baadhi ya viongozi. Hii ina maana kwamba CCM haijawa na mwelekeo ulio wazi.
Mazoea ya utawala katika ilani na programu za chama chao ni kuorodhesha kila kitu bila kuweka kipaumbele au kuchanganua
jinsi maeneo tofauti yanavyotegemeana katika kusukuma maendeleo kwa ujumla. Ni kawaida kwa mfano kwa ilani za CCM
kuorodhesha kilimo; ufugaji; viwanda; elimi; afya n.k. bila kuweka uzito na kuonyesha ni kipi kitangulie. Utekelezaji wake
umekuwa ni wa ubabaishaji kwa kuwa unagusa kila eneo ili mradi ionekane machoni pa wananchi kuwa mambo yamefanyika katika
kila eneo. Matokeo ni kwamba hakuna hata kimoja kinachofanyika kwa ufanisi na maeneo mengine muhimu kama kilimo hutelekezwa,
maendeleo kudidimia na umasikini kukithiri hasa miongoni mwa wakulima.
Ili kuleta mabadiliko ya kweli katika suala la sera na utekelezaji wake, CHADEMA imeazimia kufanya mabadiliko ya kweli ili
kuleta uhuru na maendeleo ya kweli katika maeneo makuu matano, nayo ni: Elimu; Afya; Kilimo; Ajira, na
Mfumo mpya wa Utawala.
Katika kuhakikisha kuwa sera hizi zinatekelezeka, CHADEMA itafanya yafuatayo:
- Kupambanisha maeneo machache muhimu ambayo kwa pamoja yatachangia kutoa chachu ya kufufua uchumi na maendeleo ya jamii.
- Kutambua sekta ongozi na kuipa kipaumbele maalum ili iweze kuyasukuma maeneo mengine. Hii ni sekta ya elimu.
- Kuchanganua na kueleza umuhimu wa maeneo hayo na yanavyoungana ili kuongeza tija na ufanisi katika kuleta maendeleo.