Ni jambo la kusikitisha kwamba mjadala unaoendelea Tanzania sasa kuhusu hatma ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unaonekana kutekwa na watu waliokata tamaa au na watu wasioamini katika sababu na misingi mikuu ya ushirikiano.
Mimi binafsi nikiwa mmojawapo wa Watanzania waliohusika kwa karibu sana katika uendeshaji wa Jumuiya iliyosambaratika mwaka wa 1977, na pia katika EACSO iliyoitangulia, naona kwamba nina wajibu wa kutoa maoni yangu pamoja na kuelezea baadhi ya yaliyotokea. Huenda hata ushauri wangu unaweza kusaidia jinsi ya Tanzania kujipanga ili tuweze kuendeleza ushirikiano wenye manufaa kwa taifa letu na vizazi vijavyo.
*[ Kwa taarifa, niliteuliwa Deputy Secretary katika ofisi ya Secretary
General, EACSO Januari 1963, nikafanya kazi kama Personal
Assistant wa S.G. na pia Clerk to EACSO Authority. Baadaye
nikapandishwa kuwa Secretary Administration nikiendelea kuwa
Clerk to The Authority. June 1964 niliteuliwa kuwa Financial
Secretary wa EACSO lakini mara nikaitwa kurudi katika Serikali
ya Tanzania nilikopewa madaraka mengine kuanzia Septemba
1964. Miaka 10 baadaye, yaani mwaka 1974 niliteuliwa na EAC
Authority kuwa Katibu Mkuu, na niliendelea na wadhifa huu hadi
Jumuiya iliposambaratika mwaka wa 1977. Baada ya EAC
niliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na katika wadhifa huu
nilihusika pia katika uteuzi wa msuluhishi Victor Umbricht,
nikishirikiana na mawaziri wenzangu wa Kenya na Uganda.
Inavyofahamika, Ripoti ya Umbricht iligawa mali na madeni ya
EAC kwa wanachama husika na katika ripoti hiyo aliweza
kupandikiza mbegu ya kufufua ushirikiano.]
Misingi na Sababu za Ushirikiano (Basic Principles and Reasons)
Hakuna ubishi kwamba ushirikiano ni chanzo cha nguvu na kinyume chake, yaani utengano, huleta udhaifu. Katika siasa za kimataifa na za kitaifa, katika uchumi na katika maendeleo yoyote ya kijamii, ushirikiano wa dhati baina ya nchi, watu au taasisi zozote unaimarisha na utengano unadhoofisha.
Katika siasa za kimataifa, kwa mfano UN, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya au Shirikisho la Merikani , yaani United States (a federation of states) akinyoosha kidole na kuonyesha nia ya kuchangia mjadala, Mwenyekiti wa mkutano mara moja humpa nafasi. Lakini sio hivyo tu: Wajumbe wengine wa mataifa karibu yote wanarudi haraka kwenye nafasi zao na kuchukua earphones zao na kuanza kumsikiliza. Hata wana habari wanatega masikio na kuweka vinasa sauti vyao tayari ili kila atakalosema lirekodiwe. Vinchi vingine kama Fiji, Djibouti, Gabon, Uruguay, Malta au hata Tanzania wakianza kuzungumza, wajumbe wanaondoka kwenye ukumbi kwenda kunywa kahawa. Wanaobaki kwenye nafasi zao wengi wanaendelea kuandika hotuba zao watakazotoa baadaye. Mjumbe mwingine yeyote akitanguliza kusema kwamba anazungumza kwa niaba ya nchi za SADC, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki au Jumuiya ya Amerika Kusini, n.k. wajumbe watakaa wamsikilize. Huu ndio ukweli wa siasa za kimataifa. Na maamuzi yanategemea wanaosikilizwa wanasema nini. Kwa hiyo kama tunataka tusikilizwe tukitoa ushauri au hata tukilalamika, hatuna budi kushirikiana au kuungana.
Katika mambo ya uchumi ni vivyo hivyo. Soko la pamoja la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki litakuwa na watu takriban 100 milioni. Soko la Tanzania lina watu 36 milioni, la Kenya 32 milioni na la Uganda 27 milioni. Hata kama tutaendelea kuwa maskini, mjumbe wa soko la pamoja la Afrika Mashariki, akienda kujadili mkataba wa biashara au wa uwekezaji na nchi au jumuiya yoyote duniani atasikilizwa kwa umakini zaidi na anaweza kupata unafuu zaidi kwa vile anaweza kuuza zaidi na kununua zaidi ya nchi moja ikiwa peke yake. Tukitaka kujenga kiwanda cha aina yoyote tukiwa soko la Jumuiya itakuwa ni rahisi zaidi kwa vile bidhaa zitakazozalishwa zitauzika kwa urahisi katika Jumuiya kuliko kama nchi moja peke yake ingetaka kufanya hivyo. Hata kama ni kuuziana wenyewe kwa wenyewe, tutakuwa soko kubwa na tutaweza kuwa na viwanda vikubwa zaidi kama ni soko la Jumuiya. Haya yote ni ukweli usiopingika. Waingereza wasema hizo ni “economies of scale”.
Hata katika miradi ya kijamii, tukitaka kwa mfano kuwa na hospitali kubwa ya kisasa itakayoshughulikia magonjwa sugu kwa utaalamu wa kimataifa wa hali ya juu, itajengeka kwa urahisi endapo itaweza kutoa huduma kwa Jumuiya nzima. Vivyo hivyo kama chuo kikuu kitajumuisha nchi za Jumuiya, itakuwa ni rahisi kukipatia vifaa, majengo na mabingwa. Narudia kuwa hakuna ubishi kwamba kwa pamoja tutaweza kufanya makubwa na kwa ufanisi zaidi kuliko kama tutafanya peke yetu. Suala la kujadili ni kwa namna gani tushirikiane ili kila mshiriki afaidike na ushirika uwe wa kudumu.
Umuhimu wa nchi hizi kushirikiana ulitambuliwa hasa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na alidiriki hata kutamka kwamba alikuwa tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika, endapo kufanya hivyo kungewezesha sisi Tanganyika, Kenya na Uganda kupewa uhuru siku moja ambapo shirikisho la nchi zote tatu lingetangazwa papo hapo. Kwa bahati mbaya haya matarajio hayakutimizwa. Tukapata uhuru siku tofauti, na shirikisho limebaki kuwa ni ndoto.
Ushirikiano Endelevu Utapatikanaje?
Kama ushirikiano ni muhimu kwa maendeleo na hili halipingiki, suala ni kwamba ushirikiano wa kudumu na utakaokidhi maslahi ya washiriki wa nchi zote husika utapatikanaje? Afrika Mashariki tulishirikiana katika mambo mengi sana tangu enzi za ukoloni. Tuliendeleza ushirikiano baada ya uhuru katika EACSO (yaani East African Common Services Organization) hadi mwaka wa 1967. Kuanzia 1967 viongozi wa nchi huru za Tanzania, Uganda na Kenya wakaidhinisha rasmi huo ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Awamu ya Kwanza ya Jumuiya ilidumu hadi 1977.
Sasa kwa miaka saba tumejaribu kuunda Jumuiya upya, hatua kwa hatua; na mjadala unaoendelea baina ya wananchi wa nchi zote tatu sasa ni sehemu ya hatua hizo. Hatua hii inawataka wananchi wahusike katika maamuzi ya jinsi ya kujenga ushirikiano endelevu. Wananchi wanahusishwa kutokana na kwamba ushirikiano unaotokana na makubaliano baina ya viongozi tu hatimaye hugubikwa na ubishi na matatizo, punde viongozi hao wanapoachia ngazi. Na katika kuchangia, ni vizuri wananchi tujiulize ‘Kwa nini Jumuiya ya Awamu ya Kwanza ilivunjika mwaka wa 1977? Kama sababu zinatambuliwa, je sasa tumezishughulikia?’
Sababu za EAC I Kuvunjika na Jinsi ya Kujisahihisha
Nilivyojieleza hapo juu, mimi binafsi nilibahatika kuwa mtumishi wa ngazi ya juu katika Jumuiya iliyovunjika 1977 na pia nilitumikia kwa muda EACSO iliyoitangulia. Labda wakati ule haingewezekana kutambua kwa ufasaha udhaifu uliokuwapo, lakini sasa tunaweza kutazama nyuma na kutambua mengi kutokana na mafunzo ya historia tuliyoiishi. (Kiingereza wanasema “benefit of a hindsight”). Kwa kifupi:-
-
Sababu ya kwanza iliyoleta kusambaratika kwa EAC I, kwa maoni yangu, ilitokana na itikadi na misimamo ya kiuchumi ya serikali za washiriki kutowiana. Licha ya kwamba kikatiba Tanzania na Kenya zilikuwa zikiendeshwa na serikali za chama kimoja, Tanzania ilikuwa ikizingatia mfumo wa kisoshialisti (au ‘ujamaa’) katika uchumi wake, ambapo Kenya ilifuata mfumo wa soko au kibepari. Kwa upande wa Uganda, utawala wa kimla wa Dikteta Idi Amin ulizingatia mfumo wa kati pale ilipowezekana kuuelewa.
Kwa sasa inaweza kutamkwa kwamba nchi hizi tatu za Afrika Mashariki zina mifumo ya kiuchumi ya soko na inawiana. Ingawa siyo lazima kila nchi shiriki iwe na sera za kiuchumi na misimamo inayofanana kabisa ili ziweze kushirikiana, misimamo ikihitilafiana mno kutakuwa na misuguano na migongano mara kwa mara; na hatimaye kuleta mpasuko. Misimamo hii iliyohitilafiana ilileta misuguano na kutokukubaliana hasa katika juhudi za kurekebesha soko la pamoja la Afrika Mashariki ili linufaishe pia Tanzania na Uganda. Minung’uniko ilikuwa kwamba Kenya ilikuwa inafaidika zaidi, na nchi hizi nyingine hazikupata mafao ya kuridhisha.
-
Msingi wa pili wa kuendeleza ushirikiano ni nchi shiriki kikatiba kuwa na mifumo ya kupata serikali na wawakilishi wake ambayo haihitilafiani mno. Hili ni jambo muhimu kwa vile wawakilishi wa nchi shiriki katika vikao vya Jumuiya au Shirikisho ni lazima wapatikane kwa njia zinazofanana fanana. Nchi moja ikiwakilishwa na wajumbe wa kuteuliwa na Mkuu wa nchi, na nchi nyingine wajumbe wake wakachaguliwa kidemokrasia na umma, mwishowe misukumo yao ya kuendesha EAC itatofautiana mno na kusababisha kutokuelewana.
Wakati wa EAC I, baada ya Idi Amin kuchukua madaraka huko Uganda kwa mabavu, tulikuwa na vituko vingi ambavyo mara kwa mara vilikaribia kusambaratisha Jumuiya. Wawakilishi wa Uganda katika ngazi za juu na katika vikao vya Jumuiya walikuwa ni wateule wa Amin, na licha ya kwamba jitihada za kutafsiri Mkataba wa Jumuiya wa 1967 zilifanywa ili kuendelea kuwatambua na kujaribu kushirikiana nao, msuguano huo haukuashiria hali endelevu. Hata itakumbukwa kwamba Rais Nyerere alikataa kukaa pamoja na Idi Amin katika EAC Authority. Maamuzi mengi yaliyohitaji kibali cha Wakuu wa Jumuiya ama hayakufanyika, au yalichukua muda mrefu mno kuweza kuleta ufanisi. Hatimaye misuguano hiyo ilichafua mahusiano na wengi wakakata tamaa.
Kwa hiyo ili kufanikiwa sasa, ni vizuri nchi shiriki ziwe na demokrasia ya kweli na hilo lionekane ni dhahiri kwa wote. Nchi moja ikiwakilishwa na Rais aliyejinyakulia madaraka kwa mabavu au hata kwa njia zinazodhihirisha ukiukaji wa demokrasia, na nyingine zikawakilishwa na viongozi waadilifu, nchi safi zitakuwa zinajitosa kwenye matatizo. Hapa nazungumzia kipindi cha Jumuiya, kabla ya kuwa na shirikisho kamili la kisiasa. Labda kwa kipindi hiki tutaweza kuvumiliana endapo tutatofautiana kidogo.
Shirikisho la kisiasa ni lazima liwe baina ya nchi zinazozingatia uhuru wa kidemokrasia kikamilifu, bila kuwa na viongozi wanaojinyakulia madaraka kwa mbinu chafu au kwa mabavu. Wakati huo ni lazima wawakilishi katika vyombo au taasisi za Shirikisho wawe wanachaguliwa na watu wote kwa uhuru na kwa haki kamilifu bila rushwa, mizengwe au mbinu chafu. Hata kwa serikali za nchi shirikishi (partner state governments) ni lazima ziwe zinatokana na mifumo isiyohitilafiana.
Kwa sasa naona kwamba Jumuiya inadhoofishwa na mtindo wa Uganda kutia wapinzani kizuizini au Rais kulazimisha kwa mbinu katiba ibadilishwe ili kuendeleza utawala wake. Tuwe wazi na wakweli katika jambo hili. Hata kwa Museveni kusema eti anataka kuwa Rais wa kwanza wa Afrika Mashariki kunafedhehesha juhudi za kujumuika. Kuna nani katika Afrika Mashariki, nje ya Uganda atakayeweza kuchagua Rais aliye na uroho wa madaraka kiasi cha kutia wapinzani wake kizuizini?
- Kushirikiana ni mambo ya kuridhiana: nipe ili nami nikupe. Wakati wa EAC I ilikuwa vigumu sana kuwa na “compromises”. Political compromises zilikuwa vigumu sana kuzifikia. Labda hii ilitokana na kwamba hata mataifa yaliyoongoza dunia wakati huo yalikuwa yamegawanyika kwa mithili ya mipasuko: Magharibi na Mashariki. Kwa sasa inaonekana uongozi wa Afrika Mashariki unatambua kwamba ni lazima kuwe na “give and take” hasa kama tunataka kudumisha chombo kitakachotufaidia sisi sote kwa uendelevu.
- Maslahi binafsi yalitawala mno mitizamo mingi ya viongozi na hasa pale taasisi za Jumuiya zilipokuwa zinatoa ushindani kwa vyombo vyao. Ikumbukwe kwamba hata wawekezaji kutoka nje ya Afrika Mashariki waliona vyombo kama EAA na EAP&T kuwa ni washindani thabiti na walitaka vidhoofike ili waweze kuendeleza biashara zao, hasa katika mahusiano yao na Kenya.
Kwa sasa tunaweza kusema kuwa maslahi ya nchi zote tatu kibiashara hayahitilafiani na maslahi ya wawekezaji wa ndani au kutoka nje. Kwa hiyo ushiriki wa wageni hautugawi. Yumkini, dunia ya sasa inahimiza nchi hizi ziungane au zishirikiane kwa karibu ili mahusiano na nje yanoge zaidi. Hata wawekezaji wazalendo ambao wanaona mbali wanatambua kwamba kuna manufaa kwa Afrika Mashariki kushirikiana. Hata hivyo, labda ingekuwa ni vema serikali, hasa ya Tanzania, kutoa elimu mahsusi kwa wafanyakazi, ikisisitizwa kwamba, kwa mtazamo wa muda mrefu, ajira ni lazima iongezeke endapo Afrika Mashariki wataungana na kwamba Soko la Pamoja litasaidia wote kwa jumla.
- Mifumo ya kufikia maamuzi katika EAC I ilirundika majukumu mengi mno kwa viongozi wakuu kitaifa. Mrundikano huu ulichelewesha maamuzi na utatuzi wa matatizo. Hili limedhihirika kwa uongozi wa sasa, na ufumbuzi katika EAC II umekuwa ni kuipa Kamati ya Mawaziri jukumu la kufikia maamuzi juu ya mambo mengi zaidi. Hata hivyo sina hakika kwamba Kamati ya Mawaziri inaweza kufikia maamuzi haraka kwa vile mawaziri wote watatu ni lazima wakutane ili kuamua.
Labda jinsi tunavyoendelea kukua na kupanua sekta za ushirikiano, kila waziri apewe sekta yake ambayo atawajibika kuishughulikia na kuamua, halafu baadaye atoe taarifa kwa Kamati watakapokutana ili mambo yaidhinishwe. Jinsi majukumu ya Jumuiya yanavyoongezeka ningeshauri hawa Mawaziri wakae na kuishi Makao Makuu ya Jumuiya, ama sivyo hawataweza kushughulikia kikamilifu mambo ya Jumuiya kutoka miji mikuu ya serikali zao. Mtindo wa Resident Ministers ulikuwapo katika EAC I, lakini nasisitiza ni pale majukumu yanapoongezeka tu, mawaziri watakiwe kukaa Makao Makuu. Kwa sasa sio lazima kwa vile hata wafanyakazi wa Jumuiya wameweza kwenda likizo wote wakati wa mwisho wa mwaka 2006 bila kuathiri EAC.
- Hali ya Utulivu na Mshikamano Afrika Mashariki: Jambo linalohusiana na ushirikiano wa kiserikali ni utulivu na mshikamano ndani ya nchi shiriki. Licha ya kwamba vituko vilivyoleta kusambaratika kwa EAC I 1977 vililelewa kwa muda mrefu, inaweza kutamkwa kwamba mishikamano baina ya wananchi katika nchi zote husika hususan katika kutambua umuhimu na faida za EAC, ilikuwa dhaifu. Tukitaka kuwa wawazi kabisa tunaweza kuitaka Uganda, kwa mfano, kutatua tatizo lao huko kaskazini (L.R.A.) kama sharti la kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, hasa wakati huu tunapojadili jinsi ya kuingiza baada ya kukaribishwa katika Jumuiya, nchi za Rwanda na Burundi, ni lazima tuhakikishe hatuambukizwi madhara ya migongano baina ya jamii zao. Kufungua mipaka yetu kwa wananchi wa nchi zilizo na utamaduni wa mifarakano na vita vya ndani baina ya jamii zao, kunaweza kuturudisha nyuma kimaendeleo kwa kuchelewesha mikakati yetu ya kusonga mbele.
Ni jambo la faraja kwamba hivi karibuni Rwanda na Burundi zimeonyesha dalili za amani. Lakini ijulikane kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki haiwakaribishi ili kutatua mipasuko yao ya kitaifa. Ni lazima waridhiane ndani ya nchi zao wenyewe kwa wenyewe kwanza; na hilo liwe ni sharti la kuingia katika Jumuiya kikamilifu na kufungua mipaka yetu kwao, hususan endapo watataka kuingia katika Shirikisho la Kisiasa.
- Sababu nyingine iliyoleta kuvunjika kwa EAC I mwaka wa 1977 ni kukosekana kwa maridhiano (compromises) katika misimamo baina ya wana siasa viongozi. Hakuna jumuiya au taasisi yoyote inayoweza kudumu bila viongozi kukubali kujitolea mambo fulani ili wengine nao wajitolee mambo kadhaa. (Political goodwill of give and take). Kama kuna faida katika shirikisho, basi ni lazima kila mshiriki ajitolee kwa faida ya mwingine, ili mshiriki mwenzie naye aweze kujitolea kumfaidia. Uchumi, uwekezaji katika viwanda. Biashara, ajira n.k. vinahusika sana hapa.
Najua mikataba ya EAC II inayohusu Customs Union n.k. imeandikwa ili utekelezaji wake, hatua kwa hatua, uhakikishe tunaelekea katika uwiano wa kuridhisha kwamba kila nchi inafaidika. Katika majadiliano na utekelezaji utakaoendelea muda wote Jumuiya au hata Shirikisho linadumu, ni vizuri kila wakati kuwe na political goodwill itakayowezesha compromises, ili mambo yasikwame.
- Licha ya kwamba nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zinashirikiana katika nyanja nyingi hadi 1977, ushirikiano huu ulitokana hasa na maamuzi ya wakuu wa serikali za nchi hizo. Yumkini wakati wa ukoloni, ilikuwa ni serikali ya Uingereza inaamua ni vipi na ni katika nyanja gani serikali za haya makoloni zishirikiane. Matokeo yalikuwa ni kwamba wadau wa huo ushirikiano, yaani wananchi na asasi zao za kibiashara na kijamii hazikuhusika katika maamuzi. Hii siyo kusema kwamba wadau hawakufaidika; laa hasha. Lakini wakati viongozi wao walipohitilafiana na kuanza kuisambaratisha, waliendelea bila simile, wakiwa na dhana kuwa Jumuiya ilikuwa ni mali yao au hata kwamba wao binafsi ndiyo walikuwa Jumuiya!
Hadi sasa Jumuiya ya Awamu hii mpya pia imekuwa ni matokeo ya makubaliano baina ya viongozi. Ili Jumuiya au ushirikiano uwe wa kudumu na endelevu, ni muhimu wadau wote wakahusishwa katika mjadala na mchakato mzima wa kuunda ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mjadala ambao sasa unaendelea baina ya wananchi wa Afrika Mashariki ni sehemu ya kuhusisha wadau wengi iwezekanavyo. Lakini hata hivyo, inaonekana kwamba ule mtindo au utamaduni wa viongozi kuamua na kutekeleza kabla ya maoni au ridhaa ya wadau kupatikana, bado unakumbatiwa. Kwa mfano, kwa nini wakuu wa nchi hizi wamejiwekea ratiba ya kukamilisha majadiliano kuhusu Soko la Pamoja, Sarafu ya Pamoja na hata kuhusu ratiba ya kuundwa kwa Shirikisho la Kisiasa kabla wananchi hawajatoa maoni yao? Maoni haya yanayokusanywa sasa yana umuhimu gani kama ratiba na maamuzi ya miundo yamekwisha fikiwa?
Maoni ya wengi ni kwamba huu Umoja wa Forodha ni vizuri uendeshwe na ukisha tengemaa, Soko la Pamoja liundwe. Ni baada ya kuona ufanisi wa Soko la Pamoja na kwamba linaendeshwa vipi, ndio hatua zifuatazo kuhusu Shirikisho la kisiasa zichukuliwe vipi na lini. Mtazamo huu wa wengi ungezingatia mantiki za jinsi tulivyotarajia EAC ya 1967 iendeshwe na ifanye kazi. Mimi nina mawazo na mapendekezo tofauti ambayo nitayaeleza katika sehemu ifuatayo ya hii mada yangu.
Shirikisho la Kisiasa Kwanza Ndiyo Jawabu
Imekwisha elezwa kwamba ushirikiano Afrika Mashariki umekuwa ukighubikwa na manung’uniko kuwa manufaa yake hayasaidii nchi shiriki kwa usawa unaoridhisha. Katika miaka ya 1960, mara baada ya uhuru, wengi katika uongozi, Julius Nyerere akiwa mmoja wao, waliamini kwamba shirikisho imara la kisiasa Afrika Mashariki, ndilo lingeweza kutoa jawabu, kwa kuhimiza maendeleo ya kasi ambayo yangeondoa sababu za manung’uniko hayo. Kutokana na sababu ambazo sasa ni historia tu, mjadala wa shirikisho ulizimwa mwaka wa 1964. Mchakato wa sasa wa kuelekea Shirikisho la Kisiasa, hatua kwa hatua, unategemea dhana kwamba kuna wakati tutafikia kiwango ambacho manung’uniko kuhusu mafao ya ushirikiano yataondolewa au kupunguzwa kiasi cha kuridhisha kila mshiriki na akubali huo ndio wakati muafaka wa kuungana kisiasa.
Hapa naimanisha kwamba kuhusu Umoja wa Forodha, hatua hii ambayo tumeifikia sasa, itaendeshwa hadi hapo itakaporidhisha nchi zinazolalamika hazifaidiki, zitakapokubali kwamba hakuna haja ya kuwa na ushuru wowote baina yao na nchi ya Jumuiya. Hapo ndipo tutakuwa tunaweza kuunda Soko la Pamoja. Baada ya hapo sera za uwekezaji katika viwanda, za kiuchumi na fedha zitarekebeshwa na kutekelezwa katika kila nchi ili tuwe na Sarafu ya Pamoja na Soko la Pamoja litakalokidhi maslahi ya wote. Baada ya hapo, mifumo ya serikali na siasa itafanywa iwiane kiasi cha kuweza kukubaliana kuwa Shirikisho la Kisiasa litangazwe.
Licha ya kwamba ni rahisi kuorodhesha hatua hizi, maoni yangu ni kuwa viongozi wa kisiasa katika nchi hizi tatu (au ?tano endapo Rwanda na Burundi wanahusishwa), watakuwa wakitoa sababu ambazo zitaahirisha utekelezaji kufikia malengo. Nahisi itakuwa vigumu kisiasa kwa kiongozi mmoja kuweza kuahirisha kiwanda katika nchi yake ili nchi nyingine iweze kusonga mbele. Pia itakuwa ni siasa ngumu kutekeleza pale mwekezaji anayependekeza eneo fulani, kuambiwa ahamie nchi nyingine kukidhi madhumuni ya kuleta usawa.
Kwa vile inaonekana kwamba viongozi wakuu wa sasa wa Afrika Mashariki wanaamini kwa dhati kwamba ushirikiano imara ndiyo jawabu sahihi la kuharakisha maendeleo na maslahi ya wananchi wao, basi hawana budi kuhakikisha wanakuwa na mfumo wa kisiasa utakatekeleza na kufikia hayo malengo bila kutetereka. Na uongozi ambao hautatetereka katika kutekeleza ni ule ulio na dhamana kutoka wananchi wote wa Afrika Mashariki kuwaletea hayo maendeleo ya hakika. Hapa namaanisha kwamba uongozi wenye dhamana kisiasa ni Serikali ya Shirikisho ya kuchaguliwa.
Kwa hiyo kwa maoni yangu, kama viongozi wakuu wanadhamiria kwa dhati kuleta maendeleo ya kweli yanayoondoa manung’uniko yaliyodumu kwa muda mrefu, mjadala wa sasa baina ya wananchi wa Afrika Mashariki ungekuwa ni wa kuunda Shirikisho la Kisiasa kwanza. Viongozi wawaeleze wananchi kuwa dhamira yao ya dhati ni kuunda Shirikisho kama wananchi watawaunga mkono. Viongozi Wakuu waeleze kwamba wameridhika kwamba serikali za nchi shiriki peke yao haziwezi kurekebesha uwekezaji na maendeleo mengine ya kiuchumi ili kutufikisha katika kiwango cha kuondoa manung’uniko. Viongozi wataje sekta ambazo wanapendekeza zitakuwa ni jukumu la Serikali ya Shirikisho. Nyingine zitajwe zitaendelea kuwa katika majukumu ya serikali za nchi wanachama.
Kwa kuanzia Shirikisho lingeweza kushughulikia: Mambo ya Nje, Uhamiaji na Uraia, Ulinzi na Usalama wa Shirikisho, Sera za Uchumi na Uwekezaji, Fedha na Soko la Pamoja, Miundo mbinu na Mawasiliano, Usafiri wa Anga, Utabiri wa Hali ya Hewa na mambo mengine kama Ziwa Victoria, ambayo kwa sasa yako katika orodha ya shughuli za EAC mpya. Viongozi Wakuu wasisitize dhamira yao ya kutekeleza kwa dhati maendeleo yatakayoridhisha kila mwanachama wa Shirikisho na wafanye kampeni kushawishi wananchi wapige kura za maoni (Referandum) kukubali au kukataa shirikisho la kisiasa sasa.
Endapo wananchi watakubali Shirikisho la Kisiasa kwa kuanzia katika kura za maoni, Tume ya Pamoja iundwe ya kuandaa na kutoa rasimu ya Katiba ya Shirikisho. Ningependekeza hata hiyo rasimu ya katiba, baada ya kujadiliwa na kukubaliwa na Wakuu wa Nchi na kupitishwa na Mabunge ya nchi wanachama ipigiwe tena kura za maoni na wananchi wote wa Afrika Mashariki kama ndiyo Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Endapo Afrika Mashariki watakubali Shirikisho basi maandalizi yafanywe ya uchaguzi wa Rais wa Shirikisho na Makamu wake (mmoja au wawili) pamoja na wa Wabunge wa Afrika Mashariki kama Katiba itavyokuwa imetamka. Napendekeza katika taasisi ya kutunga hseria za shirikisho kuwe na Senate na House of Representatives ili katika Senate kuwe na wawakilishi ambao ni sawa kwa kila nchi shiriki, ambapo katika House of Representatives wawakilishi wawiane na idadi ya watu katika majimbo ya Shirikisho.
Serikali ya Shirikisho itakuwa na jukumu la kushughulikia masuala ambayo yamekwamisha ufanisi wa ushirikiano Afrika Mashariki kwa miaka mingi. Viongozi wake watakuwa wamechaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Afrika Mashariki baada ya kutoa ahadi katika ilani za vyama vyao vya siasa jinsi ya kutatua matatizo ya Shirikisho na kuleta maendeleo ya kuridhisha. Kama ni sera za uwekezaji, kama ni mipango ya kuendeleza viwanda, kama ni uhamiaji, ajira na teknolojia, kama ni kupanua miundo mbinu n.k. mambo hayo yatakuwa ni majukumu ya Rais wa Shirikisho na wasaidizi wake kuhimiza utekelezaji na kusahihisha ili kila sehemu ya Afrika Mashariki iridhike. Hawa viongozi watakuwa na dhamana ya kisiasa (mandate) kutekeleza kwa ufanisi, ama sivyo katika uchaguzi utakaofuata watachaguliwa viongozi m’badala na wananchi wa Afrika Mashariki.
Ni matumaini yangu kuwa wenye dhamana ya kuandaa muundo muafaka wa kuwezesha ushirikiano utakaokidhi maslahi ya wote Afrika Mashariki kwa muda endelevu, watapima kwa umakini mapendekezo katika hii mada yangu. Naamini haya mapendekezo yakitekelezwa yataondoa dalili nyingi za kusuasua na utekelezaji wa kusitasita katika mikakati ya kushirikiana kwa maslahi ya wote