lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

Wakulima lazima wawe huru

na
Edwin I.M. Mtei

INAONEKANA kama serikali na wananchi wengi wanadhani wakulima ni watu ambao hawana uwezo wa kuamua mambo yanayoweza kuwasaidia katika maisha yao.

Amri na maagizo yanayotolewa na watawala kama wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, hata mawaziri, siku hizi, yanadhihirisha dhana yao kwamba wakulima hawajui au hawawezi kuamua lolote linaloweza kuwasaidia.

Nitatoa mifano michache: Wakati njaa ilipokuwa inaathiri wananchi wengi, kulikuwa na wakulima ambao walikuwa na mahindi mabichi.

Mengi ya haya mahindi yalilimwa kwa umwagiliaji, kwa kuwa mvua ilikuwa haba. Baadhi ya hawa wakulima walipokata mahindi haya mabichi na kuyapeleka sokoni ili wapate fedha za kununulia mahitaji yao mengine kama mchele, maharage, nyama, sukari na hata nguo na vifaa vingine kwa ajili ya familia zao, viongozi hao, waliwarukia na kuwakataza wasiuze mahindi mabichi.

Sijui ni sheria gani walikuwa wanafuata, lakini ni lazima kuna wakulima wengi sana walioathirika binafsi kutokana na amri hizi.

Licha ya kwamba Watanzania wengi wanadhani ugali wa unga wa mahindi ndio chakula tu, ni lazima watawala wetu wajue kuwa mkulima anayelima kibiashara anaweza akahitaji kuuza mahindi kabla hayajawa tayari kufanywa unga ili apate mahitaji yake muhimu.

Hakuna sheria inayozuia kukata mahindi yangu yanapokuwa karibu kutoa mbelewele ili niyarundike katika shimo la ‘silage’ yavunde, ili kulisha ng’ombe wangu wa maziwa.

Nikiamua kuwa nitafaidika zaidi kulishia ng’ombe mahindi niliyolima, nitakuwa nimevunja sheria gani? Na nikiamua kukata mahindi yangu na kuuza kabla hayajakauka kwa vile mahitaji yangu muhimu yatapatikana, ni sheria gani inanizuia?

Jambo la pili ambalo linadhihirisha kwamba watawala wetu wananyanyasa wakulima ni jinsi tunavyoshughulikia biashara ya mpakani na nchi jirani.

Wakati tunapokuwa na uhaba wa chakula Tanzania, mwananchi yeyote akivuka mpaka na kwenda kununua mahindi au nafaka yoyote, anarudi katika baiskeli yake na gunia lake na kupokewa bila kubughudhiwa na polisi au ofisa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Biashara ya aina hii mara nyingi inafanyika bila kupitia katika ofisi za Idara ya Forodha na serikali imelifumbia macho suala hili kwa miaka mingi.

Mifugo pia hupitia njia hizo hizo ‘za panya’ na inauzwa au kununuliwa bila wafugaji, wafanyabiashara husika kubughudhiwa.

Lakini wakati nchi ina uhaba wa mahindi, ona tatizo linalowakabili wakulima wanaotaka kuuza mahindi yao ya ziada waliyovuna endapo watayabeba kwa baiskeli na kujaribu kuvuka mpaka.
Polisi wanawaburuza na kuwasweka rumande pamoja na kuwanyang’anya bidhaa zao. Wafanya biashara wakijaribu kuvusha shehena ya mahindi kufuata bei nzuri, hata malori yao yanafilisiwa.

Wakulima hawaruhusiwi kuuza mazao yao nje ya Tanzania kwa bei ya juu inayowavutia mpaka wapate kibali maalumu kutoka kwa serikali.

Eti ni lazima wauze kwa wananchi wenzao, licha ya kwamba bei zenyewe haziwezi kurudisha gharama za uzalishaji. Kama huo si uonevu, ni nini?

Linganisha hali hii na jinsi wazalishaji wengine wa bidhaa kama mafuta, viatu, nguo na nyinginezo hapa nchini ambao husaidiwa na kuhimizwa kuuza ng’ambo, bila kujali kama bidhaa yenyewe imeadimika nchini au la.

Tanzania ya sasa inasema inafuata mfumo wa soko. Kwa nini mkulima alazimishwe kuuza mahindi yake nchini kwa bei ya chini?

Serikali ikitaka wananchi wanunue mahindi ya wakulima wa hapa nchini haina budi kupanga bei ambayo itawavutia kwa kulinganisha na ile ipatikanayo katika nchi jirani.

Kama wananchi wa kawaida hawawezi kumudu bei hiyo, basi serikali iyanunue na kuuzia wananchi kwa bei ya chini.

Wakulima Tanzania wasifanywe ndio wanatoa ruzuku ya vyakula kwa wananchi wengine, kwa kutumia haya masharti yanayokwenda kinyume cha soko huru. Nasisitiza kutoa ruzuku ni jukumu la serikali.

Tatu, licha ya kwamba ni busura kwa mkulima anayelima mazao ya chakula kujiwekea kiasi fulani cha akiba kwa matumizi ya familia yake, ni lazima tukubali kwamba mazao mengi yanaharibika haraka sana kwa kuliwa na wadudu.

Kwa hiyo ni muhimu kwa hawa wakubwa wanaohimiza wananchi waweke akiba, watoe ushauri wa njia bora za kuhifadhi ambazo ni rahisi kuzifuata.

Ikiwezekana, Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) wahimizwe kutengeneza ‘Mini-Silos’ ambazo wananchi wanaweza kuweka nafaka kiasi cha tani moja au mbili.

Hizo Silos ziuzwe kwa bei nafuu kwa wakulima kuhifadhi mazao yao kwa chakula cha familia.

Hapo zamani tulikuwa tunatumia kihenge cha asilia, lakini aina ile ya mahindi haikuwa inapekechwa na wadudu. Pale ambapo mazao ni mengi, nashauri kwa dhati kabisa serikali ijenge silos kubwa na ifanye mpango wa kununua na kuhifadhi hayo mazao.

Utaratibu unaweza hata kupangwa ili kila mkulima anayewasilisha mazao yake katika silo ya umma apewe stakabadhi inayothibitisha kiasi cha mazao yake.

Atakapoyahitaji baadaye, ama kwenda kuyauza au kuyala, ataleta stakabadhi na kupewa mahitaji yake. Utaratibu huu unafuatwa chini ya sheria ya mwaka jana, lakini sheria hii inahusiana zaidi na kuwezesha mkulima akope fedha anaposubiri kuuza mazao yake.

Mazao mengi, hasa mahindi na maharage chotara yanayozaa sana, huharibiwa na wadudu hata kabla ya kuvunwa shambani.

Kwa hiyo, kama hakuna utaratibu wa kuyahifadhi kiusalama, mkulima akiharakisha kuyauza baada ya kuvuna, mara nyingi ni kutokana na kujaribu kuepuka hasara ya mazao yake kuharibika.

Na kama kwa kufanya hivyo atapata bei nzuri, ataweza kujiwekea akiba ya fedha na kununua mahitaji yake sokoni baadaye.

Ninachosisitiza ni kwamba, kama kwa kuvuka mpaka huyu mwananchi atapata bei nzuri zaidi, asizuiwe kwa masharti ya polisi bali serikali iwe tayari kuyanunua kwa bei inayovutia.

Wakulima wafuate soko huru kama wawekezaji na wazalishaji wengine wanavyohimizwa kufanya.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl