WAKATI wa enzi za Mwalimu tulikuwa na msemo wa kimombo uliosema ‘Argue. Don’t shout’.
Msemo huu ulisisitiza kwamba tujadili mambo au tubishane kwa utulivu na kwa mantiki, na si kwa kupaza sauti na kupiga kelele.
Sasa inaonekana msemo huu umesahaulika kabisa, hasa pale viongozi katika Awamu ya Nne wanapotaka mambo yao yafanyike haraka.
Licha ya kwamba mambo mengi wanayotaka yafanyike, yakifanyika yatatuletea maisha bora na maendeleo, ni vizuri kutambua kwamba uendeshaji wa nchi yoyote ile, unahitaji uchambuzi wa kina katika hali ya utulivu.
Ni lazima uwe uchambuzi unaokaribisha michango mingi ya kitaalamu na ya aina mbali mbali, kwani kuna Watanzaniaa wengi wanaojali kwa dhati maendeleo ya nchi hii.
Hakuna Mtanzania binafsi mwenye ukiritimba (yaani ‘monopoly’) wa uzalendo au uwezo na hekima kuweza kutoa maamuzi sahihi na endelevu kila wakati peke yake.
Ni lazima tupange kwa utulivu na kwa ushirikishaji wa akili, utaalamu na mazoea ya wote wanaohusika katika utekelezaji, kabla ya maamuzi kufikiwa na maagizo kutolewa.
Kububujika kwa maagizo na amri ambazo hazitekelezeki au hazitekelezwi ni dalili za viongozi kuwa na hamaki au kufilisika kimawazo. Hata imani ya wananchi kwa viongozi wakuu itafifia, na baya zaidi, viongozi wa ngazi ya chini watawaiga na kuburuza wananchi. Nitatoa mifano michache.
Kwanza, nakubaliana kabisa na uongozi wa Awamu ya Nne kwamba elimu bora kwa watoto wa Tanzania wengi iwezekanavyo ni muhimu na ni lazima sana.
Lakini hatuna budi kukiri na kukubali kuwa awamu zilizotangulia zilizembea kuandaa mazingira ya elimu bora kwa wote, au ziliboronga katika maandalizi, kuwezesha elimu ya aina hiyo kutolewa mara moja na kwa sasa hivi.
Kwa hiyo ni lazima tuandae na tuweke mazingira yatakayotuwezesha kufikia malengo yetu mapema iwezekanavyo.
Hapa namaanisha kwamba, iwapo mkoa au wilaya fulani imeamua kujenga na kumalizia idadi kadhaa ya shule, si tu ni lazima majengo yenyewe yawe yanakidhi viwango vya usalama na afya kwa watoto, bali ni lazima papo hapo tuwe tumehakikisha kuwa walimu wanaohitajika watakuwapo.
Ni lazima tuwe na vifaa vya kufundishia na huduma muhimu kama nyumba za walimu, madawati, maabara, vitabu na vingine. Itakuwa tumepotosha umma na/au kufuja mali ya umma, endapo shule zitafunguliwa na watoto wengi kuhimizwa kujiunga nazo, halafu tukakuta vifaa muhimu havipo na walimu hakuna au ni wachache na/au wanataabika mno kuweza kutoa huduma ipasavyo.
Tusirudie ule mtindo wa UPE wa mwaka 1978, ambapo vijana waliomaliza shule za msingi mwaka 1978 walianza kufundisha watoto wenzao.
Matokeo yamekuwa ni watoto waliomaliza elimu ya msingi katika miaka ya 1980 na 1990 kutoweza kusoma au kuandika barua ya kuomba kazi.
Shule nyingi zilikuwa na madarasa chini ya mwembe na watoto wengi walikuwa wanakalia mawe au matofali, au walikaa sakafuni; na wengi wao wakidhani wazazi wao walikuwa wanawatesa. Wengi wamechukia shule tangu wakati huo.
Mfano mwingine ni kuhusu kilimo. Maagizo yakitolewa na wakuu kwamba uzalishaji wa zao fulani ni lazima ufikie kiwango fulani baada ya miaka kadhaa, ni lazima hayo maagizo yatokane na uchambuzi wa kina.
Uchambuzi utahusu pembejeo na zana zinazohitajika, ardhi inayofaa itakayotengwa kwa ajili ya zao hilo, motisha kwa wakulima husika, mikopo na huduma muhimu, mbegu bora, mpangilio wa kuuza mazao yenyewe, miundombinu kama barabara za kudumu kuwezesha zana na pembejeo kufika mashambani na mazao kusombwa mara baada ya kuvunwa, n.k.
Hayo si maagizo yanayoweza kutokana na semina au warsha ya maofisa wa kilimo na wadau wengine kadhaa wanaohudhuria kwa siku moja au mbili.
Mfano wa tatu unahusu afya na magonjwa ya milipuko. Hivi karibuni kumetokea maagizo ya kutokomeza kipindupindu katika muda mfupi, bila ushauri wa kitaalamu, hata kuwafanya wengi wetu tuone hilo agizo ni kichekesho.
Sababu za magonjwa haya zinajulikana. Hizi sababu ni pamoja na tamaduni zetu zisizokwepa uchafu, mazingira duni ya kula na kunywa yanayosababishwa na umaskini uliokithiri, elimu ya afya kuwa finyu, huduma za kijamii kama za maji safi na maji taka kutokidhi viwango sahihi, na mila na desturi za wengi kutokwenda na wakati. Sababu hizi haziondolewi kwa amri za haraka haraka.
Licha ya kwamba mlipuko ukizuka mahala fulani ni lazima kila juhudi za haraka zifanywe na viongozi na umma kwa jumla kuzuia kuenea kwa majanga, hilo si jambo la kuagiza litokomezwe kwa muda mfupi. Matukio kama hayo yatugutue na kutufanya tuongeze juhudi endelevu za dhati za kuondoa hizo sababu za msingi. Haya matukio yatukumbushe kwamba bado bajeti yetu ya huduma za kijamii ni finyu mno na kwamba kipaumbele tunachotoa kwa huduma hizi, kulinganisha na sekta nyingine, si sahihi.
Mfano unaodhihirisha kwamba viongozi wa ngazi za chini wanaiga wakuu wao na kutoa amri zinazoathiri masilahi ya umma ni amri zilizotolewa hivi karibuni kutumia magari ya zimamoto na magari ya wagonjwa kusindikiza maandamano ya CCM huko Moshi, huku magari hayo yakipaza ving’ora, ili wananchi wajiunge na waandamanaji na kumiminika uwanjani.
Imeelezwa kwamba eti hiyo ilikuwa ni amri ya meya wa manispaa katika juhudi za kupinga matamshi ya hivi majuzi ya Mwenyekiti wa CHADEMA.
Kama kungekuwa na mjadala, ingeonekana kwamba maagizo kama hayo ni hatari kwa usalama wa umma, licha ya kwamba ni ufujaji wa mali ya umma kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
Kwa hiyo nashauri kwa dhati kabisa tujadili mambo. Amri na maagizo yamezidi.