Tatizo la njaa ni tatizo la umaskini. Nchi nyingi ambazo hazina mvua zinaweza kuwa na chakula kutosheleza watu wake kutokana na kukiagiza kutoka nje au kutumia teknologia ya hali ya juu kama kuchimba visima na kumwagilia mashamba yao. Mifano ni kama Saudia, Israel na Misri. Licha ya kwamba hizi nchi ziko jangwani, hata sisi tunaagiza bidhaa za vyakula kutoka kwao. Kwa hiyo tatizo la njaa Tanzania kimsingi litatatuliwa tu pale ambapo tutatokomeza umaskini. Hata kwa sasa , Watanzania wanaotaabika kutokana na njaa ni wale ambao hawana kipato cha kutosheleza. Kutokana na uhaba wa chakula na bei yake kupanda mno, hawa hawawezi kukinunua.
Ukame na Mafuriko
Ukame na kukosekana kwa mvua za kuridhisha, hasa katika kipindi hiki kumesababisha uzalishaji finyu wa mazao ya vyakula katika sehemu nyingi za nchi yetu. Mvua nyingi zinazoambatana na mafuriko pia zimesababisha uhaba wa mavuno. Kwa hiyo mikakati tofauti inahitajika ili kukabiliana na tatizo la uzalishaji finyu.
Kwanza, tatizo la ukame: Sehemu nyingi za nchi yetu zinageuka jangwa kutokana na sababu kuu mbili. Sababu ya kwanza ni uharibifu wa mazingira unaotokana na kukata miti ovyo, hasa kwa ajili ya kuni, mkaa, mbao na ujenzi. Misitu mingi ya asili imepunguka sana au kutoweka kabisa kwa vile kampeni za kupanda miti wakati wa kuvuna miti hazitiliwi maanani. Uchomaji moto wa misitu unaotokea mara kwa mara wakati wa kiangazi na wakati wa kuvuna asali, huongezea uharibifu huu kwa vile miti yote michanga huungua. Ni jambo la faraja kwamba Rais Kikwete ametilia mkazo maofisa misitu watekeleze wajibu wao kikamilifu bila rushwa au woga kutatua tatizo hili.
Sababu ya pili ya jangwa kuenea katika nchi yetu ni idadi ya mifugo kutodhibitiwa. Wafugaji wameachiwa kuongeza mifugo yao bila kipimo na pale malisho yanapopunguka wanahamia sehemu nyingine bila mpangilio. Kwa maoni yangu, viongozi wa siasa na serikali wanawaogopa au kuwaonea haya wafugaji, hasa wakati uchaguzi wa kisiasa unapokaribia. Wafugaji wamevamia vyanzo vya maji kama Ruaha Mkuu, wakati sote tunawaangalia, tukijua kuwa mabwawa kama ya Mtera na Kidatu yanaweza kuathirika na kusababisha janga kubwa la kitaifa. Tumeona haya au kufumbia macho wafugaji wakivamia kwa maelfu ya mifugo yao, sehemu za ukulima Mbeya, Rukwa na Iringa mpaka sasa uhasama umeongezeka baina ya wafugaji na wakulima. Mifugo yao imeongezeka hadi kufikia idadi inayoifanya ife kwa kukosa maji na majani. Licha ya kwamba Mlima Kilimanjaro uko upande wa Tanzania na unatuletea mvua hasa upande wetu, wafugaji wetu katika wilaya ya Longido, wamelazimika kuvuka mpaka kutafuta maji upande wa Kenya! Maji yanayoanzia mlima Kilimanjaro yanahifadhiwa kwa kisayansi zaidi upande wa Kenya.
Msafiri yeyote anayevuka mpaka wetu na Kenya pale Namanga anaweza kujionea mwenyewe tofauti. Upande wetu ni vumbi, ukame na mifugo iliyokondeana, ambapo wenzetu upande wa Kenya wana miti, majani, maji na mifugo iliyonona. Mashamba yao ya malisho (ranches), yana mipaka (fences) kwa kila mfugaji. Nahisi hata uongozi wao pia umewawekea kiwango cha idadi ya mifugo kwa kila ekari na wataalam wanawafuatilia kuhakikisha mazingira hayaharibiki.
Wizara yetu mpya ya Mifugo ni lazima iwaelimishe wafugaji wetu kuhusu umuhimu wa kila mmoja kuwa na sehemu yake maalum ya kufuga na ikiwezekana aigawe katika mafungu (paddocks), ili mifugo isile kiholela. Pia uashauri utolewe kuhusu idadi ya mifugo. Endapo dalili za ukame zinaonekana, wafugaji washauriwe (au hata walazimishwe) kuuza na kuipunguza kabla mifugo haijakonda. Haiingii akilini kwamba mfugaji mwenye ng’ombe zaidi ya 200 huko mkoani Shinyanga eti anakufa njaa! Pia hata mifugo yake inakufa njaa.
Kwanza ni lazima tuelimishe wafugaji wetu kuwa nyama ya ng’ombe ni sehemu kuu ya chakula bora. Nyama ya ng’ombe ikisalia inaweza kukaushwa katika jua au kwa moshi na kuwekwa kwa muda mrefu ikitumiwa kama chakula. Ng’ombe akiuzwa wakati anauzika fedha zipatikanazo zinaweza kutumiwa wakati wowote kununulia chakula na mahitaji mengine. Kwa hiyo ni jukumu la viongozi kuelimisha wananchi kwamba mifugo ni fedha na utajiri. Mtu tajiri hafi njaa kwa vile chakula anaweza kukinunua.
Tumepata kukabiliwa na njaa pia kutokana na mafuriko. Mashamba pamoja na mazao yanasombwa na maji ya mafuriko na kuathiri kilimo cha wenye kulima sehemu za mabonde ya mito. Hapa ndipo waathirika wanakuwa ni wale wasiokuwa na kipato kingine au akiba. Kwa vile majirani wa hawa waathirika ni lazima walipata mvua, wanaweza kuwa na chakula cha ziada kuuza. Lakini hata Serikali inaweza kutoa misaada kwa waathirika kama hawa endapo watakuwa hawana jinsi ya kujilisha.
Aina ya Mazao ya Kilimo
Ili kuepukana na njaa na umaskini nashauri kwa dhati kabisa kwamba uongozi wa nchi, usisitize kwa wakulima (na ikiwa ni lazima walazimishwe) kulima na kupanda tu yale mazao yanayostahimili hali ya hewa ya mahala husika. Ukitembelea sehemu nyingi za Tanzania utaona ukanda ulio na ukame au mvua hafifu wakulima wanalima mahindi kila msimu. Mara nyingi utaona mahindi yamekauka kabla ya kuwa na mbelewele. Lakini ukipita hapo mwaka unaofuata utakuta kwamba licha ya kwamba hakuvuna chochote msimu uliopita, mwenye shamba hilo anang’ang’ania kulima mahindi. Hata kama utabiri wa hali ya hewa unasema mvua itakuwa haba, utaona anapanda mahindi.
Najua kwamba ugali wa mahindi ndiyo chakula kinachopendwa sana nchini. Lakini hatuwezi kulazimisha mahindi yastawi kila mahali hapa nchini. Wakulima wafunzwe kulima zao mbadala, kama mtama, mihogo au alizeti pale ambapo mahindi hayawezi kustawi. Kama mkulima atavuna zao alilootesha kwa wingi, ama atajizoesha kula chakula hicho mbadala au atauza apate fedha za kununulia mahindi anayopendelea.
Nilipokuwa nasafiri na mtaalamu mmoja barabara kati ya Same na Mombo msimu mmoja, ilisikitisha sana kuona ukame wa sehemu ile. Mtaalamu huyo alinidokezea kwamba wakulima wa sehemu hiyo wanang’ang’ania kulima mahindi kila msimu eti kutokana na kwamba Serikali ilikuwa imetamka kwamba haitakubali mtu yeyote afe kwa njaa na kwamba itagawa mahindi ya bure au kwa bei ya chini sana. Kwa hiyo, hawa wakazi wa sehemu ile, wakivuna au wasipovuna mahindi, wana hakika watapata mahindi na kula ugali. Kwa maoni yangu, wakulima hawa wanajifedhehesha kwa kutoa jasho kila msimu bila kuvuna chochote, na kudidimia katika lindi la umaskini licha ya kupelekewa mahindi ya msaada kila wanapotaabika.
Ninachotaka kusema ni kuwa ili kuondokana na adha ya njaa na umaskini, ni lazima kilimo chetu kiwe ni cha mazao yanayostahimili hali ya hewa na aina ya ardhi ya mahala husika. Wakulima wasaidiwe kwa ushauri pamoja na kupatiwa mbegu bora ya aina ya zao linalostahimili pamoja na zana na pembejeo zinazohitajika. Endapo wengi wa wakulima wetu watalima na kuvuna kwa wingi, watayauza na kujinunulia mahitaji yao, na balaa la umaskini na njaa litatoweka au kupunguzwa sana.
Utamaduni wa Milo na Vyakula Asilia
Nimekwisha gusia kuwa mila na desturi za kutochinja ng’ombe na watu kufa njaa wakati mifugo inaweza kuliwa au kuuzwa haziingii akilini na kwamba tamaduni hizo zimepitwa na wakati. Pia sio lazima kula wali na ugali wa mahindi tu. Ni lazima tujizoeshe kula vyakula kama mihogo, mtama, magimbi, viazi vitamu, viazi vikuu na mviringo, vipere na ndizi. Ukisafiri ukaenda Nigeria au Ghana utakuta watu wenye afya, nguvu na akili, ambao vyakula vyao vikuu vingi ni mchanganyiko wa magimbi (yam), mihogo na ndizi (plantain). Ukitembelea Harare huko Zimbabwe, utaona maduka ya nyama ya ng’ombe iliyokaushwa kwa moshi au jua na inauzwa kwa bei nzuri tu. Ikiwa ni lazima wataalamu wetu wa mapishi wajaribu kufundisha jinsi ya kuandaa vyakula kwa mchanganyiko wa yale mazao yanayopatikana kwa urahisi ili viwe na virubitisho vinavyohitajika na pia ladha nzuri.
Kwa muhtasari, nasema kwamba njia moja ya kuondokana na adha ya umaskini ni wakulima kuzalisha mazao yanayostahimili hali ya hewa mahala wanapoishi. Mazao hayo yawe ni ya kibiashara, na yumkini yakilika basi wajizoeshe kuyala. Wakizalisha kwa wingi watayauza na kununua aina ya chakula kinachowaridhisha. Hivyo ndivyo tutaweza kuondokana na adha ya njaa.
Ni lazima tuondokane na dhana ya kwamba chakula ni mahindi tu. Kwa vyovyote vile tusipande mahindi mahala ambapo ni dhahiri kwamba hayatastawi. Tulime mazao yenye tija mahala hapo ili tuyauze tununue mahindi na mahitaji yetu mengine. Mwisho nasisitiza kwamba wakati wa kuoneana haya na wafugaji wanaozidisha idadi ya mifugo yao na kufanya nchi yetu kuwa jangwa na kutusababishia maafa makubwa kitaifa, umepita. Lazima idadi idhibitiwe na mahala pa kila mfugaji patengwe na afuge hapo hapo. Tuhamasishe ufugaji wa kisayansi na wa kibiashara.