Uchaguzi wa Rais
Rais akiwa ndiye mkuu wa nchi, kielelezo na mwakilishi mkuu wa taifa ni lazima awe ni kiongozi
anayekubalika na aliyechaguliwa na wengi wa Watanzania. Kutokana na msingi huo, endapo katika
Uchaguzi Mkuu kuna wagombea zaidi ya wawili, maathalan watano (5), na hakuna mgombea aliyepata
zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa, basi ni lazima wale wagombea wawili wanaoongoza kwa
kura warudie kinyang'anyiro hicho cha uchaguzi. Kwa kawaida katika nchi nyingi marudio kama
hayo hufanyika baada ya majuma matatu au manne ili kuiwezesha Tume ya Uchaguzi kuchapisha
makaratasi ya kupigia kura mapya yenye maelezo na picha za hao wagombea wawili, pamoja na
kuandaa mambo mengine ya lazima. Ni lazima kurudia uchaguzi kama huo mapema ili vituo vya
kupigia kura viwe ni vilevile na wasimamizi wawe ni walewale wa Uchaguzi Mkuu wa awali. Pia
itakuwa wapiga kura wana vitambulisho na kadi zilezile walizotumia wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Kutokana na pendekezo hili muhimu katika kuimarisha demokrasia katika nchi yetu, ni lazima
Katiba ya Tanzania iliyopitishwa na Bunge mwaka wa 2000, irekebishwe kwa kubadili Ibara na.41(6)
ili isomeke ifuatavyo:-
"(6) Mgombea yeyote wa kiti cha Rais atatangazwa kuwa rais iwapo tu amepata zaidi ya nusu ya
kura zote halali zilizopigwa. Endapo hakuna mgombea aliyepata zaidi ya nusu ya kura hizo, Uchagazi
utarudiwa baada ya muda utakaopangwa na Tume ya Uchaguzi, ambapo wagombea watakuwa ni wale
wawili walioongoza kwa kupata kura nyingi zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa awali".
Naamini na kusisitiza kwamba badiliko hili katika Katiba ni muhimu sana katika kuhakikisha
umoja, mshikamano, amani na utulivu katika nchi yetu. Kwa mfano kama kuna wagombea wengi
inawezekana kabisa kwa mgombea aliyepata chini ya robo ya kura zote kutangazwa kuwa Rais wa
Tanzania. Kwa mfano tukiwa na wagombea watano uchaguzi ujao na wagombea wakapata:-
Kulingana na Katiba yetu ya sasa, mgombea wa Chama A aliyepata asilimia 24 tu za kura ndiye
atakayetangazwa kuwa Rais. Hii ni hatari sana kwa umoja na mshikamano wa Taifa kwa vile
Watanzania wapiga kura asilimia 76 watakuwa hawakumpitisha huyu awe Rais wao. Kiongozi kama
huyo huenda hata akawa amechaguliwa na kanda fulani ya nchi au na kabila moja kubwa na hii
itaathiri sana umoja na mshikamano wa Taifa letu.
Tukizingatia pendekezo la kurudia uchaguzi baina ya wagombea A na B, na mmoja wao akapata
asilimia 60 na mwingine 40, mshindi atakuwa anajiamini zaidi kwa kufahamu kuwa kuna wananchi
wengi wanaomuunga mkono ingawa yeye sio chaguo lao la kwanza bali ni chaguo lao la pili. Yaani
ikiwa ni Mgombea A atapata kura 60% atakuwa ameongeza kura 24% kwa 36% kupata ushindi. Endapo
ni Mgombea B atashinda, itakuwa ameongeza kura za 23% kwa 37% kuwa mshindi. Rais anayetambua
misimamo ya wananchi kuhusu umaarufu wake miongoni mwa wapiga kura Watanzania atakuwa makini
zaidi katika maamuzi yake na hatawatambia au kuwadharau kama inavyoweza kutokea endapo
amechaguliwa "kwa kishindo" na kwa mpigo.
Naamini kwamba hoja hii ya kurekebisha Katiba kuhakikisha uchaguzi wa rais unarudiwa endapo
mgombea anayeongoza katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu hakupata zaidi ya nusu ya kura halali
zilizopigwa ni nyeti sana. Nimekwishaeleza kwamba vyama vingi vya siasa, hata CCM, vinapata
viongozi wao kwa mizengwe, ujanjaujanja na rushwa. Mheshimiwa Rais Mkapa na Katibu Mkuu wa
CCM hivi karibuni walikiri hata hadharani kwamba kuna mizengwe na dalili za rushwa ndani ya
chama chao wakati huu tunapoelekea Uchaguzi Mkuu mwakani. Vitisho kwamba viongozi
wa ngazi za chini watafukuzwa kazi endapo CCM itashindwa vimetolewa hadharani. Kwa vile hata
takrima wakati wa kampeni (ambayo kwa wengi ni rushwa) imehalalishwa, basi tukijumuisha hayo
yote hakuna uhakika wowote kwamba atakayeshinda atakuwa ni chaguo huru la wapiga kura. Hasa
ikiwa huyo mshindi atakuwa amepata chini ya nusu ya kura, na kutangazwa, basi umati wa wapiga
kura (majority) Tanzania utakuwa umeporwa.
Namsihi Mheshimiwa Rais pamoja na Chama cha Mapinduzi, pamoja na viongozi wote wa vyama vya
siasa na wa Umma kwa jumla, wanaotutakia mema sisi Watanzania,wachambue na kuchanganua kwa
makini na kina hoja hii ya kurekebesha Ibara na.41(6) ya Katiba. Wajue kwamba wana wajibu wa
kuepusha Tanzania kutoka katika janga la mgawanyiko na vurugu. Naamini kwamba wote wana wajibu
wa kuhakikisha kuwa mrithi wa Mheshimiwa Mkapa atakuwa ni Mtanzania atakayechaguliwa na kura
zaidi ya nusu ya wapiga kura wa nchi hii. Mimi binafsi nahofia sana hatma ya nchi yetu endapo
kiongozi wetu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 atakuwa ni mtu aliyechaguliwa kwa mizengwe,
ujanjaujanja, rushwa, wizi wa kura na vitisho, na kwamba licha ya faulo hizo, akapata chini ya
nusu ya kura. Nasema hivyo kwa vile naona ni vyama vya siasa vichache sana hapa nchini ambavyo
havijakumbwa na dosari hizi. Kama haiwezekani kuziondoa hizo dosari, basi angalau tuhakikishe
kuwa ni zaidi ya nusu ya wapiga kura watakaokubaliana kuwa na huyo kiongozi. Hiyo ni njia
itakayotuepusha na mpasuko na migawanyiko katika nchi yetu. Tunasema "wengi wape"!
Ibara na.41(6) ikirekebishwa kulingana na hii hoja, inapendekezwa kwamba Tume ya Uchaguzi
itakiwe kupanga ili marudio ya uchaguzi wa Rais yafanyike majuma matatu au manne baada ya
matangazo ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu. Kwa kufanya hivyo gharama zitapungua, kwa kuwa
itawezekana kutumia vituo na vifaa vile vile vya Uchaguzi Mkuu. Wasimamizi watakuwa ni wale
wale na wapiga kura watakuwa na vitambulisho vile vile vya Uchaguzi Mkuu. Badiliko jipya
litahusu tu wagombea wawili walioongoza kwa kura za Urais, na karatasi za picha na maelezo yao
yataweza kuchapishwa na kusambazwa katika muda huo wa majuma matatu au manne.
Mengine Kuhusu Uchaguzi wa Rais
Kama nilivyoeleza katika mada yangu kuhusu vyama vya siasa, na jinsi ya kuimarisha demokrasia
na maendeleo nchini Tanzania, naamini kwamba kama tukiendelea na mtindo wa kutoa ruzuku kwa
wagombea urais tutazidisha idadi ya wagombea na kufadhaisha wananchi wakati wa kuamua wampigie
nani kura. Ruzuku kwa mashughuli ya siasa iwe tu ni ile itolewayo kwa vyama vya siasa
kujiendesha. Vyama vitakavyostahili kupata ruzuku hiyo viwe ni vile vilivyothibitisha umaarufu
wao kwa kuungwa mkono na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa wa-Bunge na madiwani. Wagombea wote:
yaani wa urais, ubunge na udiwani wasipewe ruzuku. Kwa kweli kama hata wagombea binafsi
wasiosimamishwa na chama chochote cha siasa wataweza kuwepo, (na Katiba inapaswa kuruhusu hilo),
basi itakuwa ni ubadhirifu wa fedha za umma wa hali ya juu kutoa ruzuku kwa wagombea ambao idadi yao
haidhibitiki na umaarufu wao haujulikani rasmi.
Hoja inaweza kutolewa kuwa ni wagombea, wale wenye fedha nyingi au watakaofadhiliwa na matajiri
ndio watakaoweza kufanya kampeni kikamilifu. Nchi nyingi zenye kutekeleza chaguzi huru za
kidemokrasia zinadhibiti viwango vya juu vya michango ya kusaidia wagombea toka kwa kampuni au
watu binafsi ili kupunguza mianya ya rushwa na uwezekano wa viongozi "kuwekwa mifukoni mwa
wakubwa". Ukiukaji wa viwango hivyo unaweza kufanya uchaguzi wa mgombea ukawa batili. Sheria
kama hiyo pia inapunguza uwezekano wa aliyechaguliwa kujisikia ana deni kubwa kwa makampuni au
watu binafsi waliomfadhili na kwa hiyo kuwapendelea kibinafsi katika kuwahudumia katika wadhifa
wake. Kwa mantiki hii, misaada isipodhibitiwa inakuwa haina tofauti na rushwa. Nashauri suala
hili lichambuliwe kwa kina.
Kwa maana nyingine, napendekeza kwamba Sheria ya Uchaguzi ifanyiwe marekebisho ili imtake kila
mgombea asivuke kiwango fulani cha matumizi kwa ajili ya kampeni. Kiwango hicho kiwekwe kwa
kuzingatia uwezo wa vyama makini ili wananchi (kitaifa, kijimbo na kikata) waweze kufikiwa na
mgombea husika. Kiwango cha msaada kwa mgombea kutoka kwa watu na makampuni binafsi kiwekwe ili
iwe ni marufuku kuvuka kiasi fulani. Sheria imwezeshe mgombea mpinzani katika taifa, jimbo au
kata kumtaka mpinzani wake athibitishe uhalali wa msaada ambao ana ushahidi kuwa umevuka
kiwango. Lakini ieleweke kuwa masharti ya viwango vya misaada yanahusu watu au kampuni binafsi
tu na siyo wahisani wa nje na wa ndani wanaofadhili rasmi na kwa uwazi uimarishaji wa maendeleo
ya demokrasia.