lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

29 Januari 2008

Tunakosa washauri wa uchumi na fedha?

na
Edwin I.M. Mtei

MATAMSHI na maamuzi ya serikali ya hivi karibuni, yanaashiria ama hatuna washauri wa kiuchumi na fedha au tunapuuza ushauri huo. Nitatoa mifano michache:
Vyama vya wafanyakazi vikiongozwa na wakuu wao walitangaza kwamba walitaka kiwango cha chini cha mshahara kiwe sh 315,000 kwa mwezi. Mazungumzo yaliendelea baina ya waajiri na wafanyakazi, Serikali ikisimamia majadiliano kwa mujibu wa sheria.

Pia kulikuwa na tishio kwamba watumishi wake wangegoma kama kiwango cha sh 85,000 hakingepandishwa mpaka sh 315,000.

Sijasoma majibu ya serikali yaliyochambua madai haya ya wafanyakazi. Nilitegemea uchambuzi kuonyesha uwezekano wa nyongeza kiasi hicho, ukifafanua haja ya kutoa motisha kwa waajiriwa, tija kazini, athari za ongezeko kubwa katika mfumko wa bei na uwezo wa waajiri kulipa.

Katika mazingira ya utawala bora unaozingatia haki na uendeshaji wa uchumi endelevu, nilitegemea Wizara ya Mipango na Uchumi, Wizara ya Fedha na Wizara ya Kazi wangekaa na kuchambua kwa makini na kuonyesha ni kiwango gani cha chini kingeweza kuidhinishwa ili uzalishaji uendelee na papo hapo wafanyakazi wa kima cha chini waweze kumudu maisha.

Uchambuzi wa aina hii ulikuwa unafanywa katika enzi za awamu ya kwanza, na Rais Nyerere alikuwa anatangaza kila Mei Mosi, kima cha chini cha mshahara. Kima hiki kilizingatia mfumko wa bei tangu Mei mwaka uliopita, ukuaji wa uchumi na ongezeko la tija katika muda husika.

Baada ya uchambuzi huo mazungumzo baina wa wadau wote, yaani wafanyakazi, waajiri na serikali wangefuata ushauri unaotokana na huo uchambuzi yakinifu. Lakini miezi hii ya karibuni Waziri wa Kazi, John Chiligati, alikubaliana na wadau kadhaa na kutamka kima cha chini cha sh 150,000 na papo hapo kusema kuwa katika sekta fulani walipwe hata sh 315,000 kwa mwezi.

Wakati waajiri kadhaa walipoeleza kwamba tija ya viwanda vyao haiwezi kukidhi kiwango hicho na wafanyakazi wakagoma, waziri alitoa amri kwamba waajiri ni lazima walipe kiwango kilichofikiwa kisheria na pia hawawezi kufunga viwanda vyao!

Kama Tanzania hatutaki kurudia mtindo ule wa ruzuku kutoka Hazina ya Serikali ili wafanyakazi wasiwafungie mameneja wao viwandani, basi ni lazima tupime hoja zote za wadau, wakiwemo waajiri na wafanya kazi. Ni umbumbumbu kutoa amri eti kiwanda kiendelee kama hutoi ruzuku.

Hata katika mashamba huwezi kulazimisha mkulima mkubwa alipe sh 85,000 kwa mwezi kama mazao yake hayakidhi kiwango hicho. Ama mkulima huyo atapunguza vibarua au ataacha kupalizi, kupiga dawa, kutia mbolea au kunyweshea.

Matokeo ni kwamba uchumi utaathirika. Hakuna yeyote anayefaidika kwa kutoa maagizo na amri za kisiasa zisizotekelezeka.

Mfano mwingine ni matangazo yaliyotolewa na Serikali mwisho wa wiki kuwa kima cha chini serikalini kitakuwa sh 100,000 kwa mwezi kuanzia Januari mosi mwaka huu wa 2008.

Ghasia, Waziri anayehusika amesema watumishi wamekubaliana na uamuzi huo, na kwamba ongezeko hilo litagharimu Serikali sh 200 bilioni kwa mwaka. Lakini ameendelea kueleza kwamba serikali haina fedha katika bajeti yake ya sasa, bali wafanyakazi ni lazima wasubiri hadi Julai 2008 wakati bajeti ya mwaka 2008/2009 itakapoidhinishwa!

Magazeti yameeleza kwamba viongozi wa watumishi serikalini wamekubali kwa shingo upande, na wanasubiri.

Jambo linalotia wasiwasi ni kwamba kumekosekana ushauri wa kiuchumi na fedha hapa tena.

Kama kweli wafanyakazi wanahitaji nyongeza hiyo wamekubalije kusubiri? Malipo ya malimbikizo ya miezi sita yakilipwa Julai mosi, yatatibua mfumko wa bei kwa namna ambayo uchumi wa Tanzania wote utaathirika? sh 100,000,000,000 (bilioni mia moja) zikiingia katika mzunguko wa fedha siku moja, ni vurugu tupu; hasa kwa vile wahusika ni wafanyakazi wa kima cha chini ambao wamesubiri na wametaabika kwa muda mrefu? Bei zitapanda kiasi cha kumfadhaisha mfanyakazi.

Bidhaa zitakuwa adimu kiasi kwamba ongezeko hilo halitamsaidia mfanyakazi aliyepata ongezeko. Wananchi wengine watapandishiwa bei za bidhaa za kawaida wanunuazo.

Hapa naona serikali imekosa tena ushauri thabiti wa kiuchumi. Kama ni lazima kurekebisha kima cha chini, basi mishahara hiyo ianze kulipwa Januari 2008. Inajulikana kwamba serikali haitozi fedha zote za kodi zinazoidhinishwa siku ile ile bajeti inapoanza kutumika. Inakopa. Kwa hiyo inaweza kukopa Januari 2008, kama itakavyokopa Julai, 2008.

Kwa hiyo, kama serikali ni lazima irekebishe kima cha chini, basi Bunge liidhinishe fedha hiyo ya nyongeza katika kikao cha Januari 2008. Hii itamaanisha kila mwezi, kuanzia Januari 2008, sh 16.7 bilioni zinaingizwa katika mzunguko wa fedha nchini na labda kwa utaratibu huo tutaweza kujirekebisha polepole, badala ya kuingiza kwa mkupuo mmoja sh 100 bilioni Julai mosi.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl