lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

26 Desemba 2007

Uchaguzi wa Kenya: Tanzania tujifunze nini?

na
Edwin I.M. Mtei

UCHAGUZI uliofanyika Kenya wiki mbili zilizopita, umefedhehesha Wakenya na hata Afrika nzima. Wakati wa kampeni, wagombea na vyama vyao walionyesha ukomavu wa kisiasa na hata wakati wa kupiga kura kulionekana hamasa na utulivu vilivyotupa matumaini.

Lakini mambo yalivurugika wakati wa uhesabuji wa kura, hasa pale wasimamizi katika makao makuu ya majimbo walipojumuisha kura zilizopigwa na kuhesabiwa vituoni, kisha kupelekwa kwa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK).

Vurugu ziliongezeka wakati ECK ilipokuwa ikijumuisha na kuidhinisha rasmi matokeo yaliyokuwa yamewasilishwa kutoka majimboni. Hata kutangazwa rasmi kwa matokeo kulichochea vurugu, na mauaji yaliyokuwa yameshaanza, yalizidi kutokana na jinsi tume ilivyoonyesha kutokuwa huru.

Licha ya dalili za ECK kutokuwa huru, mwenyekiti wake wakati huo alisisitiza kuwa anazingatia katiba na sheria na kutangaza matokeo kama ifuatavyo:-

Mwai Kibaki alipata kura 4,584,721, sawa na asilimia 46.0; Raila Odinga alipata kura 4,352,993, sawa na asilimia 43.7; Kalonzo Musyoka alipata kura 879,903, sawa na asilimia 8.8 na wagombea wengine wote walipata kura takriban 150,000, sawa na asilimia 1.5.

Licha ya Kibaki kuongoza katika haya matokeo, hakuwa na zaidi ya nusu ya Wakenya wapiga kura waliojitokeza kumchagua kama kiongozi wao. Hata hivyo, mipango ya haraka haraka ilifanyika kumwapisha, na alikula kiapo cha urais katika muda wa takriban saa moja baadaye.

Sina hakika kwamba Sheria ya Uchaguzi ya Kenya inatamka vipi juu ya matokeo ambayo hayaonyeshi ushindi uliozidi asilimia 50, lakini busara za kidemokrasia zingetaka majadiliano baina ya viongozi hawa wawili (Odinga na Kibaki) kabla ya Kibaki kuapishwa kuwa rais.

Hasa pale ilipodhihirika kwamba wengi wa wabunge waliochaguliwa majimboni walikuwa wanamuunga mkono Odinga, basi Kibaki alipaswa kushauriana naye ili ijulikane kama wangeweza kuunda serikali ya mseto au la.

Kama Odinga angesema katika majadiliano hayo kwamba hataki kushiriki, basi Kibaki angemwendea Kalonzo aone kama wangeweza kushirikiana, kwa vile kwa pamoja wangekuwa na kura asilimia 54.8. Ingekuwa ni busara Kibaki kuanza majadiliano na Odinga kwa vile ushindi wa kiti cha rais peke yake hautoshi kama Bunge litakuwa linadhibitiwa na wapinzani. Hasa kwa vile Odinga angeungwa mkono na Kalonzo, wangekuwa pia na kura asilimia 52.5!

Funzo kwetu ni nini?

Katiba ya Tanzania inafanana fanana na ile ya Kenya, kwa vile zote mbili zinaruhusu vyama vingi vya siasa. Hata Tume ya Uchaguzi ni hivyo hivyo. Zote zinateuliwa na rais, na licha ya kwamba sisi Tanzania tunatamka kwamba tume ni lazima iwe huru, ubinaadamu unakuwepo, hasa pale Watanzania wengi, kama Wakenya, hawataki “kumwaga unga”. Wakina Kivuitu, Masauni na watu kama hao, wamezagaa kila kona!

Majukumu ya tume ni hayo hayo. Tume ya Uchaguzi ikishatamka kwamba mgombea ubunge amechaguliwa, ni mahakama tu ndiyo inaweza kuamua vinginevyo. Hapa kwetu ni zaidi, kwani tume ikishatamka mgombea amechaguliwa kuwa rais, hata mahakama haiwezi kuhoji!

Kwa hiyo kwa kuanzia, Tanzania ni lazima tuhakikishe kwamba tume yetu ya uchaguzi inakuwa huru na inaonekana huru. Ikiteuliwa na rais peke yake, kama sheria inavyotaka sasa, haiwezi kuwa huru. Kama tunanuia kwa dhati kujiepusha na majanga na maafa yaliyoikumba Kenya ya Kibaki, Odinga na Kivuitu, hatuna budi kubuni jinsi ya kuunda Tume ya Uchaguzi huru.

Sina haja ya kuwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba maafa karibu kama ya Kenya yalitufika mwaka 2000/2001, hasa huko Pemba. Licha ya kwamba rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ameonekana juzi akihutubia Wakenya, maafa ya Wapemba waliokimbilia Mombasa (Shimoni) na baadaye wengi wakawa wakimbizi wa siasa huko Uingereza, yaliyotokea wakati wa enzi yake, bado yangali katika kumbukumbu zetu. Aidha, “ mpasuko” wa kisiasa Zanzibar, licha ya ahadi za JK, upo hadi leo.

Pendekezo langu la dhati kabisa ni kwamba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ishughulikiwe sasa. Jambo moja linalohusu uendeshaji wa tume ni jinsi ya kuboresha orodha ya wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Matangazo yanayoendeshwa sasa kuhusu oboreshaji wa daftari hilo huko katika mikoa ya Mtwara na Lindi ni sawa.

Lakini tume ingetoa umuhimu kwa majimbo ambayo hivi karibuni inategemewa kutangaza chaguzi ndogo kutokana na wabunge wao kufariki au kuondolewa bungeni na mahakama. Itakuwa ni aibu tume kupelekwa mahakamani na Mchungaji Mtikila tena, wakati majimbo hayo yatakapokuwa yanaendesha kampeni za chaguzi ndogo na hapo hapo ikijulikana kwamba tume ingeweza kuboresha daftari hilo kwanza katika majimbo yenye chaguzi ndogo.

Pendekezo langu la pili ni kwamba, katiba na sheria ya kuunda Tume ya Uchaguzi zirekebishwe mapema. Zisisitize uadilifu kwa wanatume na watumishi wake. Zisisitize wanatume kutofungamana na chama chochote cha siasa. Labda sheria itamke kwamba baadhi ya wanatume wawe ni wateule wa vyama vya kidini na vya wanaharakati wanaotetea haki na usawa ambao wamebobea katika fani zao kwa misimamo ya ujasiri na uadilifu.

Kama itakuwa ni lazima rais ateue baadhi ya wanatume, basi na viongozi wa vyama vikubwa vya siasa nao wapewe fursa ya kuteua baadhi ya wanatume. Wawe ni watu waliotosheka, na uteuzi wa wanatume wote uidhinishwe na Bunge baada ya wanatume kuhojiwa. Muda wao wa utumishi kama wanatume uwe ni miaka kumi na iwe ni marufuku mwanatume kuondolewa madarakani kutokana na msimamo wake katika maamuzi halali ya tume.

Ili tume iwe huru, bajeti yake iwe inaandaliwa na Katibu wa Tume akishirikiana na Hazina na iwe ni sehemu ya Mfuko wa Pamoja Maalum (yaani Consolidated Fund Services) kama ilivyo kwa asasi ambazo hazihojiwi bungeni, kwa mfano; rais, Mahakama Kuu, madeni ya taifa na malipo ya wastaafu.

Tatu, maafa na machafuko mithili ya Kenya yanaweza kutokea Tanzania 2010 endapo katiba yetu itaendelea kama ilivyo sasa. Hapa nazungumzia hasa Ibara 41(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyorekebishwa mwaka wa 2000. Ibara hii inasomeka ifuatavyo:-

“(6) Mgombea yeyote wa kiti cha rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa rais iwapo tu amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote.”

Niwakumbushe Watanzania wenzangu kwamba, kabla ya rekebisho hili la katiba, ibara hii tangu zama za chama kimoja ilikuwa inatamka: “Mgombea yeyote wa kiti cha rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa rais iwapo tu amepata zaidi ya nusu ya kura zote halali zilizopigwa…” Hisia zangu ni kwamba, ifikapo 2010, tukiwa na wagombea kiti cha rais wanane kama ilivyokuwa 2005, huenda matokeo yakawa kama yalivyotangazwa huko Kenya wiki mbili zizopita.

Nahisi kwamba inawezekana kabisa mgombea wa chama kitakachoongoza akapata asilimia 30, wa chama kitakachofuata akapata asilimia 25, wa chama kingine akapata asilimia 20 na waliobaki wakagawana hizo asilimia 25 zilizosalia.

Endapo katiba hii itakuwa haijarekebishwa mwaka 2010, basi mgombea atakayepata asilimia 30 hizo atatangazwa amechaguliwa kuwa rais. Na kwa vile, mizengwe, mbinu chafu, hata “takrima” zinaweza kutumiwa, nahofia ubishi mkali, mithili ya vituko vya Kenya, utatukabili hapa Tanzania.

Watanzania wa kizazi kipya wanataka demokrasia ya kweli inayotoa haki sawa kwa wote. Kwa hiyo ni lazima turekebishe katiba yetu irudie ule msimamo uliokuwepo kabla ya marekebisho ya 2000, pakiwa na badiliko linalotamka kwamba uchaguzi utarudiwa baina ya wagombea wawili walioongoza kwa kura. Yaani tutamke katika katiba yetu kwamba:

“Mgombea yeyote wa kiti cha rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa rais iwapo tu amepata zaidi ya nusu ya kura zote halali zilizopigwa. Endapo hakuna mgombea aliyepata zaidi ya nusu ya kura, wagombea wawili walioongoza kwa kura nyingi, watarudia uchaguzi, ambao utaandaliwa rasmi kwa ajili yao mapema iwezekanavyo kabla ya miezi miwili kupita tangu siku ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu.”

Naamini kwa dhati kabisa kwamba rekebisho hili litawaepusha Watanzania na vurugu na machafuko mithili ya vituko vya Kenya vya hivi karibuni.

Ninawasihi viongozi wote wa nchi yetu wanaohusika watafakari kwa makini pendekezo hili ili kuepusha watu wetu na maafa.

Licha ya kwamba wasuluhishi maarufu wa kimataifa wamezuru Kenya kuwafanya watulizane na wakubaliane, naamini pia kwamba suluhisho thabiti la Kenya ni kwa Tume Huru ya Uchaguzi (labda ya kimataifa kwa sasa) kusimamia uchaguzi mpya baina ya Kibaki na Odinga.

Kwa vile hakuna mmoja kati yao aliyepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, basi utaratibu wa kurudia uchaguzi uandaliwe na wasimamizi wa kimataifa wahusishwe badala ya ECK. Baadaye Katiba ya Kenya pia inaweza kurekebishwa kama nilivyopendekeza kwa Tanzania.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl