lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

26 Desemba 2007

JK anashauriwa vibaya kuhusu rushwa, uzembe

na
Edwin I.M. Mtei

Rushwa na uzembe unaowahusu viongozi na wakubwa, hautadhibitiwa Tanzania kama Rais Jakaya Kikwete ataendelea kuchukua hatua kama anavyoshauriwa sasa.

Na jinsi rushwa na uzembe wa wakubwa unavyoota mizizi na kuenea nchini, ndivyo dhiki na umaskini vitakavyoshindikana kutokomezwa hapa nchini na imani kwa rais wetu itakavyoendelea kupungua.

Kuna mambo kadhaa ya msingi ambayo ni lazima yazingatiwe kama rais anadhamiria kwa dhati kushughulikia suala hili. Nitayataja kwa kifupi.

Kwanza, ni lazima tutazame katiba inasema nini kuhusu majukumu ya rais na uwezo (powers) wake katika masuala ya uteuzi na usimamizi wa utekelezaji na uendeshaji wa serikali. Ibara ya 35(1) ya Katiba ya Muungano wa Tanzania inatamka kwamba “Shughuli zote za utendaji za serikali zitatekelezwa na watumishi kwa niaba ya rais.”

Ibara ya 36(2) ya katiba inaendelea kutamka: “Mamlaka ya kuwateua watu kushika nafasi za madaraka katika utumishi wa serikali, na pia kuwaondoa katika madaraka, kuwafukuza kazi na kudhibiti nidhamu ya waliokabidhiwa madaraka yatakuwa mikononi mwa rais.”

Madaraka haya makubwa yanadhihirishwa zaidi pale Ibara ya 37(1) ya katiba inapotamka kwamba: “Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na katiba hii au sheria kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa.” Hii ndiyo sababu hata Baraza la Mawaziri (Cabinet) kikatiba linamshauri tu rais, na yeye anaweza kukataa au kukubali maamuzi ya Baraza la Mawaziri.

Pili, kwa maoni yangu, vituko vya hivi karibuni vimedhihirisha kwamba kuna dalili za rushwa au uzembe miongoni mwa watumishi wa umma ambao ni wateule wa rais. Rushwa na uzembe huu unasababisha maslahi yetu kama Watanzania au taifa kuathirika.

Hata viongozi serikalini, wengi walipojaribu kuzuru mikoa kadhaa kuelezea misimamo ya serikali, wananchi waliwazomea katika mikutano yao ya hadhara, jambo ambalo limepunguza imani ya raia kwa viongozi wao wa kiserikali.

Hata Rais Kikwete ambaye hapo awali alikuwa kipenzi chao, umaarufu wake umeshuka, kama utafiti wa wasomi hivi karibuni ulivyoonyesha. Ushauri wangu wa dhati ni kwamba, kuna umuhimu wa kuchukua hatua za haraka.

Nimemsikiliza mheshimiwa rais akieleza kwamba serikali haiwezi kukurupuka na kuanza kufukuza watumishi kwa hisia tu, bila taasisi husika kufanya uchunguzi na watuhumiwa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Kwa heshima na taadhima, ni lazima niseme kwamba kwa hilo rais kashauriwa vibaya.

Ukweli ni kwamba, taasisi za uchunguzi kama polisi na TAKUKURU, haziwezi kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazowahusu watu wazito kuliko hata wakuu wa taasisi zao wakati hao wazito wanaendelea kukalia viti vyao vya madaraka. Huo si utamaduni wa Kitanzania au hata wa nchi nyingi nyingine. Msemo wa kimataifa ni kwamba “panya hawezi kumfunga paka kengele”.

Tatu, kama hao wakubwa wanatuhumiwa, na wanafahamu Mhe. Rais ameagiza uchunguzi ufanywe, wanaweza kutumia fursa ya kuendelea katika nyadhifa zao kutokomeza ushahidi wowote ambao ungewatia hatiani. Kwa hiyo, kama rais anadhamiria kwa dhati kupata ukweli juu ya shutuma hizo, ni lazima waachie ngazi kwanza ili uchunguzi ufanyike na ionekane unafanyika bila vipingamizi.

Endapo uchunguzi utaendelea wakati watuhumiwa wakiwa madarakani, hata ripoti ikiandikwa na kusema kwamba yote yaliyowahusu yalikuwa ni uzushi, baadhi ya Watanzania hawataamini. Kwa hiyo imani kwa rais wetu itaendelea kushuka.

Niwakumbushe Watanzania wenzangu kwamba, wakati wa enzi za Mwalimu Nyerere, mteule wa rais akitiliwa shaka tu juu ya uaminifu au uadilifu wake, Mwalimu alikuwa anasitisha uteuzi wake au alikuwa anamhamishia katika madaraka mengine mara moja.

Hata kama uzembe ungedhihirika katika idara au wizara, waziri aliyekuwa na madaraka ya kusimamia wizara hiyo kisiasa alilazimika kujiuzulu. Mfano wa kihistoria ni ule wa Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Mhe Mwinyi alijiuzulu kutokana na Idara ya Polisi kushindwa kuzuia mauaji yaliyotokea Malampaka, mkoani Shinyanga. Baadaye kidogo Mhe. Mwinyi aliteuliwa kuwa balozi wetu huko Misri.

Funzo hapa ni kwamba, wananchi waliendelea na imani kwa rais wao, kwa vile ilidhihirika kwamba aliwajibisha hata wale waliokuwa na dhamana ya kusimamia wizara kisiasa. Mwishoni Mwinyi alirejea nyumbani, akawa Makamu wa Rais na hata akamridhi Mwalimu Nyerere mwenyewe. Ukomavu wa kisiasa ulidhihirika, kwamba watumishi wakiwajibishwa wanaweza kujirudi au kujirekebisha hata hatimaye kutoa huduma za kutukuka.

Mifano ya wizara kuboronga katika kuidhinisha mikataba iliyoathiri na itakayoendelea kuathiri maslahi ya taifa letu katika kipindi hiki cha Rais Kikwete ni mingi mno, na imezagaa kila upande. Tumekosa umeme na maendeleo ya kiuchumi kuathirika, kutokana na mikataba ya Richmond/Dowans, licha ya malipo ya gharama za kutisha.

Tunaendelea na mkataba wa IPTL unaotulazimisha kulipia gharama kubwa za umeme kupitia TANESCO licha ya kuwa kuna dalili za kuboronga au kutokuzingatia maadili wakati wa kufikia makubaliano. Katika shirika la simu na shirika la ndege ni hivyo hivyo.

Mikataba ya madini ndiyo hasa inaonyesha dalili za rushwa kunuka na wananchi wanajua kuna mushkeli. Waliohusika na yote haya wangeweza kuchukuliwa hatua za kisiasa kama nilivyoeleza, si tu ili imani ya wananchi irudi, bali wakubwa wengine serikalini watambue kuwa wakiteleza watawajibishwa bila kusita.

Rais Kikwete alipoingia madarakani alionyesha ari ya kutoa maamuzi haraka pale alipoteua tume kuchunguza yale mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge ambayo watu walitilia shaka kwamba polisi walihusika. Tume ilitoa ripoti mapema na hata ofisa mwandamizi wa polisi alikuwa mmoja wa wale waliofikishwa mahakamani.

Watanzania wengi tulikuwa na matumaini kutokana na hatua hiyo. Cha ajabu ni kwamba hadi leo haijulikani kesi ile ya mauaji imefikia wapi. Hata ile kesi ya Mkuu wa Mkoa aliyeua kwa risasi dereva wa daladala lililokwaruza shangingi lake, nayo karibu umma uisahau.

Sisi wananchi tunauliza, huu ni uzembe wa polisi katika kufuatilia au ni juhudi za wakubwa kukingiana kifua? Mhe. Rais kama angewajibisha viongozi husika ambao ni wateule wake, labda haki ingeonekana inatendeka nchini.

Madaraka ya rais kuendesha nchi kwa maslahi ya Watanzania hayaonekani yanatekelezwa kwa kudhamiria kwa dhati. Uwezo wa kuchukua hatua kuwajibisha wazembe au watuhumiwa wala rushwa bila kungojea ushahidi zaidi anao rais kwa mujibu wa katiba.

Historia itamtukuza Kikwete kama akichukua hatua za kasi zaidi zitakazopunguza rushwa na uzembe miongoni mwa wateule wake. Kama itaendelea kuonekana kwamba wakubwa hawawajibishwi, basi hata katika ngazi za chini mlungula na kuzunguka mbuyu havitakoma. Na hii ndio inaathiri zaidi maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl