lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

11 Septemba 2007

Nilipinga, naendelea kuipinga mikataba ya siri

na
Edwin I.M. Mtei

KATIKA majadiliano niliyokuwa nayo na waandishi wawili wa gazeti la RAI walionitembelea nyumbani kwangu wakitokea Dar es Salaam, moja kwa moja mwanzoni wa wiki hii, nilisisitiza kwamba mikataba tuliyo saini wakati nikiwa serikalini au Beki Kuu, ilikuwa ikitangazwa na mingine kuwasilishwa bungeni pale sheria ilipotaka hivyo.

Hata ile niliyosaini nikiwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki haikuwa ya siri. Ni jambo la kusikitisha kwamba RAI katika toleo la Alhamisi la Septemba 5, linamaanisha kama vile nimebeza msimamo wa Mheshimiwa Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Chama chetu cha CHADEMA juu ya jambo hilo.

Katika mazungumzo yangu na waandishi wa RAI, nilisisitiza kwamba sasa Tanzania haitishi wawekezaji kutoka ng’ambo tena, kama ilivyokuwa wakati wa zama za Awamu ya Kwanza.

Kwa hiyo ni lazima katika madini tuhakikishe wazawa wanakuwa wabia wa hawa wawekezaji wageni na pale ambapo Watanzania hawajitokezi vya kutosheleza, basi serikali ichukue hisa katika makampuni hayo.

Hii si tu kuhakikisha kuwa asilimia kubwa ya faida ipatikanayo inabaki hapa nchini, bali hasa wazalendo ni lazima kufuatilia kwa karibu mienendo ya haya makampuni kwa kukaa kama wakurugenzi katika bodi zao.

Niliwaeleza msimamo wangu kwamba ni vizuri serikali ikawezesha wachimbaji wadogo wanaokutwa katika sehemu zenye madini kushirikishwa kama wanahisa pamoja na wawekezaji wageni.

Ikiwa ni lazima hawa wenyeji washirikishwe wakiwa katika vikundi au vyama vya ushirika.

Kuwaondoa wenyeji kwa kuwalipa fidia ni kama kuwanyang’anya urithi ambao Mwenyezi Mungu aliwatunuku katika makazi yao ya asili.

Kuwajengea shule au hospitali si hoja, kwa vile mwekezaji yeyote anaponufaika ana wajibu wa kujenga shule, zahanati na barabara kwa jamii inayomzunguka.

Katika kusisitiza uwazi katika mikataba ili kuondoa uwezekano wa rushwa (na ni ukweli usiopingika kwamba sasa Tanzania inanuka rushwa!), niliwapa RAI sheria mbili nilizozinukuu katika gazeti la Serikali ya Afrika Kusini.

Hizi Sheria zinaonyesha bayana jinsi wenzetu Afrika Kusini walivyo wawazi. Nimetaarifiwa kwamba RAI sasa linamilikiwa na mwana CCM mwandamizi na kama kupuuzwa kwa ushauri wangu kunamaanisha sisi hatutafuata nyayo za hawa wenzetu, nahofia rasilimali zetu zitatokomea kwa wapita njia na umma wa Tanzania tutaendelea kudidimia katika lindi la umaskini. Ole wetu Watanzania!

Hata hivyo nafarijika kwamba kutokana na jinsi umma wa Tanzania unavyoafiki msimamo wa Zitto, kuna matumaini kwamba ujasiri, uzalendo na umakini wa kizazi kipya kikiongozwa na Mbowe na Zitto, tutavuka mapema. Iko siku! Rushwa na ufisadi vinatokomea!

Katika mazungumzo yangu na RAI nilisisitiza kwamba Zitto Kabwe ameelezea kutoridhishwa kwake na jinsi wataalamu wa wizara walivyopuuzwa na Waziri Karamagi na hasa kwamba hata Tume ya Mazingira ilitakiwa kuridhika na mipangilio ya kuendeleza mradi wa machimbo ya dhahabu wa Buzwagi kabla ya mkataba kusainiwa.

Badala ya msisitizo huo, hawa waandisi wa RAI wanakuza mfano nilioutaja kwamba mkataba wa TAZARA ulitiwa saini na serikali tatu za China, Tanzania na Zambia huko Beijing, China. Kwani mkataba wa TAZARA ulikuwa wa siri?

Mtu mwenye akili timamu anaweza kulinganisha mkataba wa TAZARA na mkataba wa Buzwagi? Utawezaje kulinganisha kitu kinachojulikana na kitu ambacho hakijulikani?

Watanzania wataendelea kumiminika maefu kwa maelfu katika mikutano ya Zitto na Mbowe, hadi kieleweke ni nini hasa Waziri Karamagi kaidhinisha, na kwa nini hakuuambia umma wa Tanzania mpaka alipohojiwa bungeni?

Cha ajabu ni kwamba hata Bunge lenyewe (pamoja na wingi wa wana CCM huko bungeni) hawakujua lolote juu ya mkataba huo kabla ya Zitto kuliibua suala hilo.

Naandika makala hii fupi kwa ‘Mtanzania’, ambalo ni gazeti dada la RAI, nikiwasihi wasahihishe mapema, na pia kwa magazeti mengine ili ikiwezekana msimamo huu binafsi wa muasisi wa CHADEMA, chama cha Mhe. Zitto na Mbowe, uweze kujulikana.

Tutaweza tu kupiga hatua za maendeleo thabiti kwa kuwa waadilifu, wakweli, wazalendo wanaopenda na kuhurumia watu wao, tukijiamini na tukiwa jasiri kama hawa viongozi wa kizazi kipya.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl