UCHAGUZI wa Rais unaendeshwa rasmi kwa utaratibu ulioainishwa katika ibara ya 41 ya katiba. Maoni yangu ni kuwa, kuna mushkeli katika ibara ndogo ya 41(6). Hii inasomeka: “Mgombea yeyote wa kiti cha rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa rais iwapo tu amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote.”
Katika kuchambua ibara hii ndogo, ningetaka kuwakumbusha Watanzania kwamba, katiba yetu wakati tulipokuwa na chama kimoja cha siasa (TANU au CCM) ambako kulikuwa na mgombea mmoja tu wa kiti cha rais, tulikuwa tunapiga kura za “NDIYO” au “HAPANA”.
Wakati huo, katiba ilikuwa inatamka kwamba, mgombea kuchaguliwa ni lazima apate kura za “NDIYO” zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa.
Vinginevyo, chama kingelazimika kuleta mgombea mwingine. Tulipopata demokrasia ya vyama vingi, mwaka wa 1992, katiba ilibadilishwa na kutaka “Mgombea yeyote wa kiti cha rais…apate zaidi ya nusu ya kura zote halali zilizopigwa.” La sivyo, uchaguzi ungerudiwa na wagombea wote na mgombea ambaye angepata kura nyingi kuliko yeyote mwingine, angetangazwa kuwa mshindi wa kiti cha rais.
Hapa tulithibitisha kuwa, nusu ya kura zilizopigwa ilikuwa muhimu na bora.
Kwa sababu ambazo sizielewi, marekebisho ya mwaka 2000, yaliingiza kipengele cha sasa kwamba, mgombea “atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa rais iwapo tu amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote”, kama nilivyonukuu hapo juu.
Kwa hiyo, sasa inawezekana kabisa kwa mgombea wa Tanzania kutangazwa mshindi wa kiti cha rais, hata kama amepata chini ya nusu ya kura zilizopigwa.
Kwa mfano, kama kuna wagombea saba, inawezekana kabisa mgombea anayeongoza kwa kura nyingi zaidi akapata asilimia 25 tu na hao wengine sita wakagawana hizo asilimia 75. Kwa mfano, asilimia 20, 15, 15, 10, 10 na 5. Rais aliyechaguliwa na robo ya wananchi, kwa msemo mwingine, rais ambaye amekataliwa na robo tatu (75%) ya wapiga kura, hatajisikia ni kiongozi halisi. Hatajiamini na hata akizomewa na wale anaowahutubia, itaonekana si ajabu.
Majukumu na madaraka ya Rais wa Tanzania ni makubwa mno kuruhusu mfumo unaowezesha utawala uendeshwe na mtu aliyepata chini ya nusu ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa taifa zima (minority government).
Kwa hiyo, napendekeza ibara Na. 41(6) ya katiba irekebeshwe ili uchaguzi wa rais urudiwe endapo hakuna mgombea aliyepata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa.
Wagombea watakaoshiriki katika uchaguzi wa marudio wawe ni wale wawili tu walioongoza katika uchaguzi wa awali.
Ili kupunguza gharama za kurudia uchaguzi, Tume ya Uchaguzi ihakikishe inapanga uchaguzi wa marudio ufanyike mapema iwezekanavyo ili iwezekane kutumia vituo vile vile vya kupigia kura na vifaa na wasimamizi wale wale.
Ikifanyika hivyo, gharama za nyongeza kubwa zitatokana tu na kuchapisha makaratasi yenye picha za hawa wagombea wawili na maelezo yao pamoja na kuzisambaza nchi nzima.
Nisisitize kuwa, ni wagombea wawili tu walioongoza kwa wingi wa kura ndio watashiriki marudio kwa vile kuwaruhusu wote kunaweza kutoa matokeo yale yale ya awali.
Mtindo wa kurudia wawili wanaoongoza unatumika katika nchi nyingi duniani, zenye vyama vya siasa zaidi ya viwili vinavyoshiriki katika uchaguzi wa rais.
Kushiriki kwa wawili tu, kunahakikisha kwamba lazima mmoja kati yao apate zaidi ya nusu ya kura, ambaye atatangazwa mshindi.
Ningetaka kuelezea hisia zangu kwamba, tukipata rais ambaye anatambua kuwa Watanzania zaidi ya nusu hawakumfanya yeye ni chaguo lao la kwanza, rais huyo hatakuwa anawatambia wananchi kwa dharau na kejeli, kama inavyoonekana kwa viongozi wa hivi karibuni.
Kwa hakika rais anayeridhia kwamba waziri aliyemteua anaweza kutamka hadharani kwamba Watanzania wanaweza kula nyasi bora tu ndege ya rais inunuliwe, hangekuwepo. Kwa maana nyingine, viongozi wataheshimu umma zaidi, wakitambua kuna wanasiasa wengine ambao hawako mbali mno nao kwa chaguo la wapiga kura.
Ibara ya 41 (7) pia ina utata inapotamka: “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”
Licha ya kwamba natambua ni muhimu sana nchi iwe na kiongozi mkuu mtendaji, kila wakati, na kwamba kusiwe na muda mrefu ambapo nchi ina wasiwasi, ni lazima tujiwekee mfumo na utaratibu ambao haukaribishi matumizi mabaya ya madaraka ili kunufaisha binafsi watu wenye uroho wa madaraka.
Hapa namaanisha kwamba, inawezekana kabisa kwa rais kuteua viongozi wa tume ambao watatangaza yeye rais kama ni mgombea, au chama chake kimeshinda uchaguzi, kinyume cha ukweli. Katiba inatoa mwanya huo, na hakuna njia ya kuhoji au kuchunguza.
Ni lazima tufanye utafiti tujue nchi nyingine zinafanyaje kuhakikisha Tume ya Uchaguzi inatenda haki. Pia tufahamu endapo kuna ushahidi wa kukiuka taratibu na sheria ili upande mmoja ushinde, ni hatua gani zinachukuliwa na hizo nchi.
Tusipofanya hivyo, tutakuwa tunaandaa mazingira ya watu kufanya fujo na kuvunja amani ili wapate haki zao za msingi. Nakaribisha mawazo ya wengine au maelezo kwamba nchi nyingine zinatatuaje tatizo kama hili. Makala ijayo nitazungumzia Tume ya Uchaguzi.