lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

29 Mei 2007

Marekebisho ya katiba hayaepukiki (4)

na
Edwin I.M. Mtei

RAIS ndiye mkuu wa nchi na ishara ya utaifa wetu. Katiba yetu inamfanya kuwa ndiye kiongozi mkuu mtendaji wa serikali (Executive President) na amiri jeshi mkuu.

Rais pia ndiye mwenye kauli ya mwisho juu ya maaumuzi muhimu ya mhimili wa kutunga sheria (Bunge), kwa maana kwamba ni lazima rais akubali na kuridhia muswada uliopitishwa na Bunge kabla haujawa sheria.

Katiba inampa pia rais uwezo wa kutoa msamaha au kupunguza makali ya maamuzi ya Mahakama Kuu kama mhimili wa kutoa haki.

Kuna nchi nyingi duniani ambazo ma-rais wake si watendaji wakuu, bali ni wakuu wa nchi na ishara ya taifa tu. Watendaji wao wakuu serikalini huwa ni mawaziri wakuu (nchi nyingine huitwa chancellor), ambao wanawajibika kwa Bunge na wananchi wapiga kura.

Ma-rais hao hutia saini miswada ya Bunge baada ya kushauriwa na mawaziri wakuu na kuongoza sherehe za itifaki (ceremonial figure head).

Maoni yangu ni kuwa, kwa vile rais wetu kila siku atakuwa ni kiongozi wa chama cha siasa kinachoshinda uchaguzi, basi ni vema aendelee kuwa kiongozi mkuu mtendaji wa serikali kama ilivyo sasa.

Kumekuwa na mawazo kwamba, majukumu ya rais (powers) ni makubwa mno, na kwamba ama yapunguzwe au mengine yatekelezwe kwa masharti ya kushauriana na vyombo fulani.

Ukweli ni kuwa, sheria nyingi zinatamka kwamba rais atashauriwa na vyombo vinavyohusika katika kutekeleza mambo yanayohusu sheria hizo.

Na nilivyodokeza katika makala niliyozungumzia uchaguzi wa Bunge, endapo Bunge litakuwa imara na kuwa na wabunge jasiri wenye kujali kila wakati maslahi ya taifa na wananchi, matendo maovu ya serikali hayatakuwepo au yatakemewa mapema.

Kwa hiyo, marekebesho ya katiba yanayoimarisha Bunge kwa kusimika demokrasia ya kweli na kuhakikisha sauti za wapinzani zinasikika, ndiyo jawabu la kuhakikisha rais hatumii madaraka na majukumu vibaya.

Hata hivyo, pendekezo ambalo lingeimarisha uadilifu, utaifa wetu na uwajibikaji katika utendaji serikalini, ni kwa Bunge kuhusishwa katika kuidhinisha uteuzi wa mawaziri na wakuu wengine katika wizara pamoja na Mahakama Kuu.

Kama ilivyo kuhusu uteuzi wa Waziri Mkuu ambapo Rais wa Tanzania anatakiwa kuwasilisha jina la mbunge aliyechaguliwa katika jimbo la uchaguzi, ili lijadiliwe na kuidhinishwa kwa kupigiwa kura bungeni, utaratibu huu ungefuatwa na rais katika teuzi nyingine kama nilivyotaja hapo juu.

Utaratibu huu ungeondoa hisia za rais kuwa na upendeleo, na pia ungeweza kufichua udhaifu au maovu ya weteule, ambayo rais hawezi kuwa na habari nayo.

Pia si vizuri kwa viongozi wa serikali na Idara zake zote, katika nchi kubwa kama Tanzania, kuwa ni watu ambao wote walifahamiana na rais kibinafsi.

Hapa nieleweke kwamba, sisemi kuwa rais wetu anafahamiana na viongozi wote.

Hapa nazungumzia mfumo na utaratibu ambao unampa rais uwezo wa kuhakikisha “anawafahamu” wote kabla ya kuwateua.

Mfumo wa aina hii ni mbaya. Bunge ambalo lina wawakilishi kutoka pande zote za nchi, lihusishwe rasmi katika uteuzi wa wakuu hao.

Kumekuwa na ubishi na majadiliano marefu juu ya matakwa ya katiba kwamba, rais ni lazima awe ni mwanachama wa chama cha siasa, aliyependekezwa na chama kugombea kiti cha u-rais (Ibara ya 39(2) ya katiba).

Licha ya kwamba ibara hii inakingana na haki na uhuru wa raia binafsi, ni vizuri kutambua kuwa uchaguzi wa rais una gharama kubwa sana.

Kwa hiyo, kuingiza idadi ya watu isiyothibitika katika orodha ya wagombea u-rais, si tu inatishia uwezo wa taifa kifedha, bali huenda kukafadhaisha wapiga kura.

Kuongeza dhamana inayotakiwa mgombea kuweka kabla ya kuchukua fomu ili kudhibiti idadi, itafanana sana na kusema kwamba ni matajiri tu wanaweza kuongoza Tanzania.

Wale wanaotetea katiba ya sasa, wana sababu za msingi kwamba bila chama cha siasa na sera pamoja na wafuasi, kiongozi hawezi kuunda serikali yake binafsi na kuongoza nchi.

Hata hivyo, kama mtu binafsi anaweza kupata idadi ya wananchi kumpigia kura kiasi cha kushinda uchaguzi, ni kwamba yeye ana wafuasi wananchi zaidi ya chama!

Mtu kama huyo, labda atatokana na kugawanyika kwa chama kikubwa. Kwa hiyo ili kusimika uhuru na demokrasia kamili, katiba ingebadilishwa kuruhusu watu binafsi, lakini gharama za kuweka jina lolote katika orodha ya wagombea, lazima igawanywe kwa wagombea wote walipie sawa.

Endapo mgombea binafsi atakuwa na wafuasi wengi, ataweza kulipia, na wale wanaoteuliwa na vyama watalipiwa na vyama vyao.

Hapa ningeweza kuongeza kwamba, katika ngazi za ubunge na udiwani, kunaweza kuwa na wazalendo wazuri sana wenye misimamo na mielekeo ya kuimarisha maendeleo ambao si wanachama wa chama chochote cha siasa.

Kama wangewezeshwa kusimama, ingekuwa kwa manufaa ya umma.

Kwa hiyo, hata kama rais ni lazima awe na chama cha siasa, katiba ni lazima ibadilishwe kuruhusu mgombea wa ubunge na udiwani (hata viongozi wa vijiji na mitaa) awe ni mtu yeyote, hata kama hana chama.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl