lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

11 Mei 2007

Marekebisho ya katiba hayaepukiki (2)

na
Edwin I.M. Mtei

MAPENDEZO yangu katika mgawanyo wa wabunge Tanzania Bara, wabunge wa majimbo wachaguliwe 150, wabunge wanawake viti maalum wawe 75, wabunge wa uwiano wa kura za vyama wawe 75.

Tanzania Zanzibar; wabunge wa majimbo wachaguliwe 28, wabunge wanawake wa viti maalum wawe 14 na wabunge wa uwiano wa kura za vyama wawe 14.

Jumla ya wabunge wote wangekuwa 356 idadi ambayo haingetofautiana sana na ya sasa, bali ingedhihirisha uwakilishi wa kidemokrasia zaidi kwa vile vyama vya siasa vingekuwa na uhakika zaidi wa kushiriki katika Bunge.

Hata kama Baraza la Wawakilishi likiendelea kuchagua wabunge watano, jambo ambalo sioni mantiki yake, mambo yasingekuwa mabaya mno.

Ningesisitiza kuwa majadiliano katika Bunge yakiimarika na kusisimka kutokana na kuongezeka kwa wabunge wa vyama vya upinzani, ndipo nchi itaweza kufanya maamuzi yanayosaidia maendeleo ya hakika zaidi.

Endapo serikali itakosolewa katika Bunge kwa umahiri zaidi, itajirekebisha mapema zaidi na wananchi watapata huduma bora zaidi na umaskini utaondoka nchini haraka zaidi.

Hakuna uzalendo wowote kung’ang’ania kuwa na Bunge linalopongeza serikali kila wakati, hasa kutokana na sauti za wapiga kura kadhaa kutosikika bungeni kwa vile mfumo wa uchaguzi ni mbovu.

Halmashauri za wilaya ziwe hivyo hivyo.

Maoni yangu ni kwamba kuna umuhimu wa haraka wa kuunda halmashauri za wilaya, majiji na miji kwa kuzingatia mfumo huu niliouelezea kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Yaani idadi ya kata ipunguzwe pale inapodhihirika kwamba madiwani wanaochaguliwa moja kwa moja ni wengi mno.

Kila kata ichague diwani kama ilivyo sasa, na hawa wawe ni nusu ya madiwani.

Nusu ingine iwe ni madiwani walioteuliwa na vyama vyao vya siasa, kulingana na uwiano wa kura zilizopigiwa na vyama hivyo katika uchaguzi wa madiwani.

Nusu ya hili kundi la pili iwe ni wanawake wa viti maalum vya madiwani. Nusu nyingine iwe ni mchanganyiko usiojali jinsia.

Pendekezo langu kwamba tushughulikie halmashauri hizi kwa haraka, linatokana na kudhihirika kwamba mfumo wa sasa wa kupata madiwani umeleta udhaifu mkubwa sana katika serikali ngazi ya mitaa.

Halmashauri nyingi nchini zimekuwa na viongozi wabovu, wasiojua au wasiojali majukumu yao. Kumekuwa na madiwani ambao wanadhani kuchaguliwa kwao ni fursa ya “kula” na ya kujinunulia sare za suti na majoho.

Udhaifu huu unaathiri zaidi maslahi ya umma kutokana na kwamba wataalam katika ngazi hii wana uwezo finyu au wanajumuika na madiwani “kula”.

Hata Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete ametambua udhaifu huu na makaripio aliyotoa hivi karibuni yanathibitisha kuna walakini katika ngazi hii ya utawala.

Maoni yangu ni kuwa, kama kungekuwa na upinzani wa kweli na jasiri katika halmashauri hizi, maamuzi mengi maovu hayangefanywa.

Naamini pia kwamba udhaifu wa huduma za kijamii na kiuchumi katika ngazi hii ya serikali, pamoja na uonevu na ubadhirifu wa mali ya umma uliokithiri, ungetambulika mapema na hatua za marekebisho kuchukuliwa kuepusha majanga kwa umma, iwapo mfumo wa uchaguzi wa madiwani ungehakikisha kuwepo kwa upinzani wa kweli na jasiri.

Nasisitiza kwamba, katika ngazi hii ya utawala, ndipo wananchi wa kawaida wanapofaidi au wanapoathirika kweli kweli kutokana na hali ya uwezo wa utawala.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl