lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

8 Mei 2007

Marekebisho ya Katiba nchini hayaepukiki

na
Edwin I.M. Mtei

TANGU Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania irekebishwe, kuzingatia uwepo wa vyama vingi vya siasa, mwaka 1992, kumekuwa na ubishi au majadiliano kwamba Katiba iandikwe upya, na kwamba ‘viraka’ vya kila mara katika Katiba yetu vimezidi.

Hata hivyo, hakuna chama chochote cha siasa ambacho kimeorodhesha kinaga ubaga kwamba ni kasoro gani zingezingatiwa endapo ingekubalika kwamba Katiba iandikwe upya.

Nataka kuandika mfululizo wa makala kadhaa kuchambua upungufu ninaoona katika Katiba ya nchi yetu, na katika uchambuzi huo nitakuwa nikipendekeza marekebesho ya Katiba ambayo, kwa maoni yangu, yataimarisha uhuru na demokrasia ya kweli ili kuleta maendeleo ya kuridhisha na ya kudumu katika taifa letu.

Bunge na uchaguzi wa wabunge

Nitaanza kuchambua Bunge likiwa ndilo chombo kinachodhihirisha demokrasia kwa kubainisha ushiriki wa raia katika maamuzi na uendeshaji wa nchi yao.

Kwa sasa Bunge letu lina aina zifuatazo za wabunge; wabunge wanaochaguliwa na raia katika majimbo ya uchaguzi, wabunge wanawake wanaochaguliwa na vyama vya siasa kulingana na uwiano wa kura ambazo vyama vilipata katika uchaguzi wa wabunge wa majimbo, wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, kutoka miongoni mwao, wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na Rais na Mwanasheria Mkuu.

Uchaguzi ulio huru na ulio wa haki ndiyo chanzo na kiini cha demokrasia ya kweli. Nitazungumzia taratibu za uchaguzi na muundo wa Tume ya Uchaguzi baadaye.

Lakini kwa leo niseme kuwa naamini kwa dhati kwamba kipengele kilichoingizwa katika Katiba ya Tanzania mwaka 2000 kumwezesha rais kuteua wabunge wasiozidi kumi, miaka 30 baada ya uhuru, ni kinyume kabisa cha uhuru na demokrasia na kinastahili kufutwa mapema iwezekanavyo. Hakina maana yoyote na kinafedhehesha na kudhoofisha maamuzi ya wapiga kura wakati wa Uchaguzi. Maamuzi hayo ni kwamba wawakilishi wao wawe na uwiano wanaoamua wanapopiga kura. Wabunge hawa kumi waondolewe katika Katiba.

Ninapendekeza pia kwamba baada ya miaka 45 ya uhuru na maendeleo ya elimu nchini Tanzania, sasa ni wakati muafaka wa Mwanasheria Mkuu kuteuliwa na rais kutokana na wabunge waliobobea katika fani ya sheria.

Mbunge huyo awe pia ni Waziri wa Sheria pamoja na Mwanasheria Mkuu. Mwanasheria aliyebobea na mwenye uzoefu wa kutosha serikalini anaweza kuwa ni mshauri mkuu wa huyo mwana siasa, kama ambavyo sasa Waziri wa Fedha na mawaziri wengine wanavyokuwa na wataalamu wanaowashauri katika fani zao wakati Bunge likiendelea.

Kwa hiyo, uwezo wa rais wa kuteua Mwanasheria Mkuu mfanyakazi serikalini awe mbunge ufutwe, bali rais awe na uwezo wa kuteua mbunge ambaye ni mwanasheria kuwa waziri na Mwanasheria Mkuu.

Utaratibu ulioingizwa katika Katiba wa kuchagua wabunge wanawake ili kuhakikisha jinsia zote mbili zina idadi za wawakilishi zisizopitana mno ni mzuri kwa wakati huu.

Mimi nategemea kwamba jinsi wanawake wanavyoongeza kujiamini na kupata elimu stahili, wakati utafika karibuni, ambapo idadi hizi zitalingana au hata wanawake wakazidi wanaume bungeni. Wakati huo hiki kipengele chenye upendeleo kitakuwa hakina sababu ya kuendelea kuwapo katika Katiba.

Nataka kusisitiza kwamba utaratibu wa sasa wa kuchagua wanawake wa viti maalumu kupitia vyama vyao vya siasa, kulingana na uwiano wa kura vyama vilizopata katika uchaguzi wa wabunge wa majimbo, ndiyo hasa unaotambua kwa usahihi makundi ambayo wananchi wamegawanyika kisiasa.

Nikiri hapa kwamba wapiga kura wengi wanashawishiwa na mambo mengine ambayo yanawafanya wapige kura kinyume na misimamo yao kisiasa, na hayo mambo ni lazima yashughulikiwe katika Katiba yetu ili kusimika uhuru na demokrasia ya kweli.

Lakini njia pekee ya kutambua kwa usahihi, misimamo ya wananchi kisiasa ni kwa kuhesabu kura zote zilizopigiwa vyama wakati wa uchaguzi wa wabunge wa majimbo.

Nchi nyingi duniani zina utaratibu kikatiba wa kupata wabunge wake kwa kuhesabu kura zote za vyama katika uchaguzi. Baada ya kuhesabu kura, vyama vyao vya siasa huteua wawakilishi kulingana na uwiano wa hizo kura kitaifa.

Utaratibu kama huo, kwa maoni yangu, unakosa wabunge ambao wanaweza kutetea masilahi ya majimbo fulani kutokana na kuchaguliwa na kura za kitaifa wote.

Napendekeza kwamba Tanzania tuwe na utaratibu unaojumuisha wabunge wa majimbo na wabunge waliochaguliwa kwa uwiano wa kura zilizopigiwa vyama vya siasa.

Tungeweza, kwa mpangilio huo, kuwa na Bunge ambalo nusu ya wabunge ni wa majimbo na nusu nyingine ni wabunge wa kitaifa waliochaguliwa kwa uwiano wa kura za vyama vyao.

Kama kwa mpangilio huu, Bunge litakuwa kubwa mno, basi napendekeza idadi ya majimbo ya uchaguzi ipunguzwe kulingana na idadi ya wilaya za utawala.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl