lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

3 Mei 2007

Mita zitumike kulipia ushuru wa kuegesha magari

na
Edwin I.M. Mtei

MIJI mingi duniani hudhibiti kuegesha magari katika barabara zake kwa kutoza ushuru magari yanayoegeshwa pembeni mwa barabara.

Ushuru huo hutumika pia katika kusafisha na kukarabati barabara hizo. Kwa kawaida, serikali za miji hiyo huweka mita maalum za kupokea hayo malipo, ili mwenye gari alipe kwa muda wa saa anazoegesha gari lake.

Katika miaka ya 1960 na 70, Jiji la Dar es Salaam liliweka mita katika barabara za katikati ya jiji na tulikuwa tunalipa sumuni au shilingi kama tuliegesha gari katika barabara hizo.

Baadaye, kutokana na uhuni na wizi kuzidi, hizi mita ziliondolewa na wakazi wa jiji tukawa hatulipii kuegesha magari.

Miaka ya karibuni, kumebuniwa mtindo wa kukusanya ushuru wa maegesho ya magari kwa kutumia wafanyakazi wa kampuni iliyopewa tenda ya kukusanya fedha hizo.

Mtindo huu sasa umeenea katika miji mikubwa ya Tanzania, na karibu kila manispaa inakusanya ushuru wa maegesho ya magari.

Ushuru wa maegesho sasa umekuwa chanzo cha mapato muhimu kwa miji.

Ingawa inakubalika kwamba kuegesha gari ni kupata huduma toka kwa mamlaka iliyojenga hiyo barabara, ni vizuri serikali iweke viwango vya ushuru ili gharama zisizidi mno kwa waegeshaji magari.

Kama kila manispaa ikijiwekea kiwango, tutaweza kuwa na gharama zisizokuwa na sababu, ambazo wale wanaoegesha watazitafutia njia za kuzifidia.

Kama ni wafanyabiashara labda wataongeza bei ya bidhaa wanazouza n.k. na umma utaathirika.

Hakuna tofauti na kodi nyingine, na ni lazima tuondoe uholela wa kutoza aina hii ya kodi.

Pia ni lazima serikali iweke utaratibu wa kisheria wa jinsi ya kukusanya ushuru huu.

Pale ambapo mita haziwezi kuwekwa, basi ni vizuri wafanyakazi wa manispaa wanaokusanya ushuru wajulikane na wasimamiwe ili matapeli wasijiingize na kuanza kutoza ushuru ambao haufiki panapokusudiwa.

Lazima ijulikane ni barabara za aina gani na za eneo lipi katika manispaa zinastahili kulipiwa ushuru endapo mtu ataegesha gari lake.

Siku hizi vibaka wanakuja hata vichochoroni na kuzuia gari lisiondoke, eti mpaka limelipa ushuru wa maegesho.

Barabara zenyewe hazijatengenezwa na manispaa, bali ni njia za mifugo au za watu au magari kujipitia tu.

Nyingi zimejaa matope au ni mahandaki tu. Kwa hiyo ni lazima kanda (zones) za manispaa ambako ushuru wa kuegesha unatozwa, zijulikane na zitangazwe kisheria.

Kumeibuka pia mtindo wa manispaa kuweka mawakala wa kukusanya ushuru.

Mawakala wengi wanaonekana ni watu walio na uhusiano wa kindugu na viongozi wa manispaa, na haileweki wamepata uwakala huo kwa vigezo gani.

Baya zaidi, mawakala wengi wanakusanya ushuru kwa kutoa stakabadhi za kampuni zao binafsi na si za manispaa husika.

Sina hakika kama ushuru wote unaotozwa unafika katika manispaa husika. Kwa hakika hakuna njia ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Mahesabu ya Serikali kuweza kuthibitisha kuwa fedha hizi zinafika zote katika manispaa, kwa vile hana uwezo wa kukagua vitabu vya wafanyabiashara binafsi ambao ni wakala wa manispaa.

Ukosefu wa wasimamizi wa vijana wa mawakala wanaokusanya ushuru, unawezesha vijana kupokea malipo ya maegesho bila kuyawasilisha manispaa.

Wengine hawatoi stakabadhi, hasa pale mwegeshaji wa gari anapotaka kuondoka haraka na kumpa tu bakshishi kijana “kwa kuangalia na kulinda gari lake”.

Tatizo kama hili lilikuwepo wakati tulipoanza ushuru wa kutumia barabara (Road Toll).

Wafanyakazi walioajiriwa kukusanya Road Toll, walijipatia fedha nyingi toka kwa watumiaji wa barabara waliokuwa wanataka kupitishwa haraka.

Waendesha magari wengi waliwatupia fedha na kuondoka na jamaa hawa waliinukia hapo.

Ili kutatua tatizo hili, serikali ilibuni mtindo wa kuweka Road Toll katika lita ya petroli au dizeli na kuacha kuweka vizuizi barabarani.

Ukusanyaji ushuru wa maegesho wa sasa unafanana sana na ule wa awali wa Road Toll na una mianya ya kupotea kwa fedha. Mianya hiyo inahitaji kushughulikiwa.

Kutokana na mahitaji ya mapato kwa miji yetu, na pia haja ya kudhibiti michango ya wananchi ili iende mahala husika, na pia ili kuzuia watu ambao si waadilifu kupata fedha haramu, napendekeza wizara zinazohusika ziangalie upya na kwa makini njia ya kukusanya ushuru wa maegesho ya magari.

Ikiwezekana manispaa zigharamie kuagiza mita ambazo zitatumika kukusanya ushuru huo na tuondokane na uwezekano wa kutapeliwa na wajanja.

Askari wa ulinzi wa manispaa wanaweza kutumika kulinda mita mchana, na ihakikishwe kuwa jioni fedha zote zinakusanywa kutoka katika mita na kupelekwa benki au mahala pa usalama zaidi katika ofisi za manispaa.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl