lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

3 Aprili 2007

Siwaelewi kuhusu rushwa ya rada

na
Edwin I.M. Mtei

LAZIMA nikiri kwamba sielewi msimamo wa viongozi wa Tanzania kuhusu rushwa iliyolipwa wakati serikali yetu iliponunua rada iliyotugharimu dola za Kimerikani milioni 41 badala ya bei yake ya kawaida ya dola milioni 28.

Tumeelezwa na rais wetu kwamba, Serikali ya Uingereza ilikubali kuidhinisha kampuni ya nchi hiyo iiuzie Tanzania chombo hicho kinachotumika kwa ulinzi wa kitaifa.

Tumesoma katika magazeti na kuona kwenye televisheni kwamba, Waingereza wanaotuonea huruma, wanashutumu serikali yao katika Bunge lao, si tu kwa kukubali kuuza chombo ambacho kinazidi mahitaji yetu, bali pia kwa kufumbia macho dalili za rushwa zilizoandamana na uuzaji wa rada hiyo.

Tumeambiwa kwamba, uchunguzi unafanywa Uingereza na vyombo vya serikali yao kuthibitisha ni nani katika Kampuni ya BAE Systems iliyouza hiyo rada, alihusika na kulipa rushwa ili chombo hicho kiuzwe kwa bei hiyo ya kuruka.

Imekwishatajwa kwamba, Mtanzania mmoja alilipwa asilimia 30 ya bei hiyo kama ‘commission’ na kwamba malipo hayo yalipelekwa kwenye akaunti ya benki huko Uswisi.

Yaani huyu Mtanzania alipokea dola milioni 12.3 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 16. Kwa lugha ya kawaida, hizi ni fedha za ufisadi. Kwa sheria za Kiingereza, aliyemlipa hiyo hongo ametenda kosa la jinai.

Huenda naye huyo Mwingereza alipata kifungu chake binafsi kabla ya huyo Mtanzania kuchukua kitita chake cha asilimia 30. Huyo Mtanzania aliyezipokea hizo pesa, huenda hayuko tena Uingereza na huenda hathubutu hata kurudi Tanzania kwa vile hilo ni kosa la jinai pia hapa kwetu.

Badala ya kuchunguza kwamba huyu Mtanzania alipokea hiyo hongo kwa niaba ya viongozi na maofisa gani wa serikali yetu, rais wetu analaumu Serikali ya Uingereza kwa kuruhusu hiyo rada kuuzwa kwetu kwa bei hiyo ya juu.

Mheshimiwa Kikwete anadai kwamba, Uingereza itufidie hizo fedha za ziada. Hizi fedha za ziada zililipwa Mtanzania na huenda amezigawa kwa viongozi na maofisa wa Serikali ya Tanzania, walioidhinisha na kutia saini mkataba wa unununzi. Sielewi mantiki ya madai ya Mheshimiwa Rais.

Hata hivyo, kwa vile Waingereza watachukua muda kujibu madai ya Rais Jakaya Kikwete, na watajibu tu pale wanapobaini ni nani mhusika wao na wa kwetu, inaonekana sisi wa Tanzania tunaweza kusubiri mpaka wananchi wasahau suala hili.

Nasema siwaelewi Watanzania wenzangu kuhusu kusubiri zaidi maelezo ya suala hili, kwa vile uongozi wetu unamaanisha kwamba wale watumishi waliojadili mkataba wa ununuzi hawahusiki na rushwa hii ambayo kiwango chake kinatisha.

Kama serikali yetu bado haijaomba mamlaka husika huko Uswisi kuzuia hiyo akaunti ya benki, utakuta kila senti imetolewa na kuhamishiwa tusikojua. Na sielewi kwa nini tunachukua muda kuchukulia hatua wale waliohusika na majadiliano kuhusu hiyo bei na kuidhinishwa kwake.

Ni lazima serikali inawajua kwa vile hata kumbukumbu zipo za ununuzi huo na ni miaka minne au mitano tu imepita tangu majadiliano hayo yafanyike. Kwa vile wakati hii rada ikinunuliwa kulikuwa na manung’uniko juu ya bei yake, na Serikali ya Rais Benjamin Mkapa ikang’ang’ania kuidhinisha, huenda hata viongozi kadhaa waligawiwa hiyo kamisheni ya asilimia 30.

Kwanini sisi wananchi tusiamini kwamba kuna wakubwa wanalindwa na Rais Kikwete? Mbona shilingi bilioni 16 ni kiasi kikubwa mno kwa serikali kukifanyia mzaha?

Imeelezwa kwamba, fedha za malipo haya ni mkopo toka benki ya huko Uingereza. Huu mkopo ulikuwa wa mwaka 2002 na haijaelezwa kama Tanzania imekwishamalizia kuulipa au bado.

Kwa vile waliojadili masharti ya huo mkopo ni hao hao maofisa wenye uchu wa kujirundikia utajiri wa haraka haraka, labda hata hiyo benki ililipa kamisheni kubwa kwa hawa maofisa ili waidhinishe riba ya kiwango cha kutisha. Riba iliyokubaliwa na iliyolipwa ni kiasi gani?

Ijulikane kwamba, ni walipa kodi wa Tanzania - wewe na mimi, tunalipa madeni yote ya serikali. Katika huu mkopo tumeongezewa malipo ya ziada ya zaidi ya sh bilioni 16, ili tutunishe mifuko ya hawa maofisa waandamizi wala rushwa.

Labda tumeongezewa pia riba kubwa ili watu hawa wasiokuwa na huruma na umaskini wetu, wazidi kutanua matumbo yao ya ulafi mchafu. Ni hawa watu wasiokuwa na chembe ya uzalendo au huruma na wananchi wavuja jasho wanaofilisi nchi yetu kwa kutufanya tuongezewe kodi.

Nisisitize hapa kwamba, wananchi wanalipa kodi kila siku wanunuapo mahitaji yao muhimu; chakula, nguo, kandambili, mitumba ya viatu, mafuta ya taa, umeme huko nyumbani, n.k.

Kila wakati unaposafiri kwa basi unachangia kodi iliyolipwa wakati basi na magurudumu ya basi yaliponunuliwa, pamoja na spea na dizeli viliponunuliwa. Na hizi kodi zitaendelea kutubana na kupunguza kipato chetu zaidi ili hawa wala rushwa wazidi kupanua vitambi vyao, endapo ufisadi hauondolewi miongoni mwa watumishi wa umma. Kama hatutawataka viongozi wetu kushughulikia ufisadi kikamilifu na kuutokomeza nchini, kamwe hatutashinda vita dhidi ya umaskini.

Ni jukumu letu sote, na kwa hili la rushwa ya rada tuwaambie kwa kupaaza sauti kwamba, wote waliohusika na majadiliano pamoja na kuidhinisha mkataba wa ununuzi, washughulikiwe sasa bila kuwasubiri Waingereza na uchunguzi wao. Wanajulikana.

Kamwe hatuwezi kushinda vita dhidi ya umaskini na kuwaletea Watanzania maisha bora kama tutafumbia macho au kuwaonea haya, viongozi au maafisa waandamizi wanaodhihirika kwamba ni wafisadi.

Hata kama Waingereza watatufidia hasara tuliyopata kwa kununua rada kwa bei ya kuruka, chanzo na kiini cha hiyo rushwa ni sisi wenyewe kutokana na ukosefu wa uzalendo, uzandiki na ulafi wa watu ambao wamepewa majukumu ya uongozi wa jamii. Lazima wang’olewe na mizizi yao ichomwe na kuteketezwa kama tunanuia kwa dhati kupata maendeleo ya kuridhisha na ya hakika.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl