lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

10 Februari 2007

Rushwa ya kamisheni inavyolipwa

na
Edwin I.M. Mtei


KATIKA majadiliano juu ya rushwa ya wakubwa, niliyoshiriki hivi karibuni, ilionekana watu wengi hawajui mbinu za kawaida zinazotumika kupokea au kulipa rushwa baina ya wakubwa.

Nimeamua kuandika makala hii kwa lugha nyepesi ili umma ufahamu mazingira yanayotuzunguka. Ni matumaini yangu pia wale wenye jukumu la kutokomeza rushwa miongoni mwa watumishi walio chini yao, wanaweza kuelewa zaidi jinsi mianya ya rushwa itakavyozibwa.

Kwanza, nifafanue kwamba nazungumzia rushwa zinazolipwa na kampuni zinazouza bidhaa, mitambo au huduma kubwa kubwa ambazo mara nyingi hulipiwa kwa utaratibu wa mafungu mafungu (installments).

Mikataba mingi ya ununuzi wa aina hii, hutamka kwamba fungu la malipo ya kwanza litalipwa siku ile ya kutia saini au muda fulani baada ya kutia saini. Utaratibu kama huo unawezesha mnunuzi kupata idhini au kibali kama cha Bodi au Baraza la Mawaziri, na pia muuzaji aweze kuandaa au kuthibitisha kuanza kutengeneza bidhaa/mitambo inayohusika.

Ufafanuzi mwingine ambao ningetaka kutoa ni kwamba, katika mazingira ya Tanzania, wapokea rushwa ya aina hii huwa ni wale wanaojadili na/au kuidhinisha mikataba ya manunuzi/mauzo. Ndio sababu naita hizi ni rushwa za “wakubwa”.

Pia ifahamike kwamba, hawa wanatambua fika kuwa ni kosa la jinai kuomba rushwa. Hata wauzaji wengi wa nchi za nje, sheria zao pia haziruhusu rushwa, ila kutokana na ushindani mkubwa wa kibiashara baina ya mataifa, serikali nyingi za nje hufumbia macho kamisheni ndogo ndogo (oiling and greasing) kama ni njia za kulainisha mtiririko wa biashara.

Kwa hiyo, pale mnunuzi mkubwa anapotaka kamisheni kubwa (ufisadi), muuzaji akikubali, inakuwa ni siri kubwa ya hao wawili, kwa sababu wanajua wanatenda kosa la jinai.

Ijulikane pia kwamba, muuzaji wa bidhaa, mitambo au huduma, hatumii fedha zake kulipa rushwa. Anatumia makato kutoka malipo anayopokea kutoka kwa serikali au shirika linalonunua ili kumlipa huyu mtumishi fisadi.

Pia ieleweke kwamba huyu mtumishi fisadi na meneja wa kampuni muuzaji, labda hawatakutana tena baada ya mkataba kusainiwa. Kwa hiyo kama mapatano yao ya siri yanasema, kwa mfano, afisa wa mnunuzi atalipwa asilimia 30 ya bei ya bidhaa husika, basi yule meneja wa muuzaji anaandika na kusaini cheki kiasi cha fedha hiyo kumlipa huyo afisa bila kuweka tarehe (undated cheques).

Cheki hizo (au hiyo) hazitaonyesha hata jina la anayelipwa, lakini zitahusu akaunti ya hiyo kampuni ambapo mnunuzi atatakiwa kupeleka malipo ya bidhaa inayonunuliwa kwa bei ya kuruka. Mla rushwa atahifadhi hizo cheki kwa njia ambayo upekuzi hautaweza kufanikiwa kuzipata kwa urahisi.

Nimeshaeleza kwamba, kwa kawaida malipo yanafanyika kwa mafungu mafungu na kiasi cha kila fungu kinaainishwa katika mkataba. Fungu la kwanza ambalo linaweza kulipwa wakati mkataba unapoidhinishwa, huyu afisa fisadi naye siku hiyo hiyo huwasilisha cheki yake ya asilimia 30 katika benki ya huyo muuzaji.

Huyu afisa fisadi ataandika tarehe kwenye cheki na labda ataandika jina la mkewe au kampuni yake au jina lolote la bandia ambalo amelibatizia akaunti aliyofungua Uswisi au nchi nyingine, kwa ajili ya kupokea hiyo rushwa toka kwa benki ya muuzaji. Hali kadhalika fungu la pili litakapolipwa na serikali au shirika, vivyo hivyo, huyu mla rushwa atawasilisha cheki yake na kuendelea na unyonyaji wake haramu wa fedha itokanayo na jasho la wananchi.

Malipo yoyote yanayofanywa kutekeleza mkataba, utakuta huyu mfisadi ana makato yake kutokana na zile cheki alizoandikiwa wakati wa kukubali na kusaini mkataba uliokuwa na bei ya kuruka.

Hivi karibuni nilisikiliza majibu ya Mheshimiwa Rais wetu akisema fedha za malipo ya jenereta za Richmond hazikuwa zimelipwa. Hapa alimaanisha kwamba hakuna rushwa iliyokwishalipwa. Hiyo ni kweli. Rushwa kubwa, kama ilikuwepo, haiingii kwenye akaunti ya mfisadi mkubwa hadi hapo mnunuzi wa hicho kifaa atakapolipa.

Suala si wakati wa kulipa, bali ni kama bei ya ununuzi wa jenereta ilifikiwa kwa ahadi au makubaliano ya kutoa rushwa. Suala ni kama bei ya hizo jenereta ilikuwa kubwa kuliko thamani yake. Ni wakati mnunuzi atakapolipa ndipo mla rushwa atakapopokea kamisheni yake.

Kutokana na mpangilio wa malipo ya gharama au deni linalohusu bidhaa inayonunuliwa kwa rushwa, itadhihirika kwamba maafisa wanaofaidika na ufisadi watakuwa na hamasa kubwa sana ya kuhakikisha mwajiri wao analipa.

Niongeze hapa pia kwamba, iwapo mwajiri wa afisa fisadi alipata mkopo kununulia hiyo bidhaa/mtambo, mara nyingi utakuta hata huo mkopo ulipatikana pia kwa hao maafisa kulipwa rushwa na hiyo benki.

Kwa hiyo, riba itakuwa kubwa kuliko ambapo mteja mwingine angekopa toka benki hiyo. Huo ndio ukweli wa madhara ya rushwa ya wakubwa katika maendeleo ya nchi. Endapo haitatokomezwa tutazidi kudidimia katika dhiki ya lindi la umaskini.

Nchi ya Uswisi ni maarufu katika kuficha siri za wateja katika benki zake. Kwa hiyo walarushwa wengi wamekuwa wakiweka fedha zao huko. Hata hivyo, kutokana na Uswisi kujiunga na Umoja wa Mataifa na hivi karibuni pia na Umoja wa Ulaya, pamoja na masharti ya dunia ya utandawazi, usiri wa benki za Uswisi umepungua kidogo.

Siku za karibuni, imewezekana hata fedha za ufisadi zikarejeshwa kwa nchi husika baada ya wenye akaunti kufunguliwa mashtaka katika mahakama za nchi zao na kupatikana na hatia. Kwa hiyo kwa upande wetu Tanzania, kuna matumaini kidogo endapo uongozi wetu utadhamiria kwa dhati kushughulikia walarushwa wakubwa.

Kuna wakubwa wengine wanaopeleka fedha zao katika nchi ambazo hazina kodi (tax-free havens kama Panama, Bermuda, Cayman Islands n.k.), lakini kutokana na juhudi za kimataifa za hivi karibuni za kudhibiti uhamishaji wa fedha haramu zinazolipia ugaidi, labda hawa walarushwa watabanwa na kubainika kwa urahisi endapo watahamishia fedha zao huko.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl