IMENITIA bumbuazi na kunikatisha tamaa kabisa kusoma tangazo lililochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima la Januari 6, 2007, ambalo lilitolewa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU).
TAKURU walitoa tangazo hilo kujibu wakifanya kile ambacho awali kilifanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), cha kujibu hoja zilizokuwa zikitolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, aliyekuwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi waliokiunga mkono chama chake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.
Pamoja na mambo mengine, wakati wa ziara yake hiyo ya kichama, Mbowe alizungumzia masuala kadha wa kadha ya kitaifa, miongoni mwa mambo hayo likiwa ni tatizo la rushwa, ambalo sasa linaonekana kuwa gonjwa sugu.
TAKURU katika tangazo lake hilo walisema kuwa, hakuna orodha yoyote ya majina ya wanaotuhumiwa kwa rushwa iliyowasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Jambo la ajabu ni kwamba, TAKURU wanatoa kauli hiyo miezi kadhaa baada ya Rais Kikwete mwenyewe kukaririwa akiwaeleza wananchi kule Rukwa kwamba alikuwa akiwajua walarushwa kwa majina na kuwa alichokuwa akikifanya ni kuwapa muda wa kujirekebisha.
Je, kwa kauli yake hiyo, Rais Kikwete hakuwa akimaanisha kuwa alikuwa na orodha ya majina ya walarushwa? Au TAKURU wanataka kutuambia kuwa hayo majina aliyosema anayo aliyapata wapi kama si kwa kuletewa?
Hata kama ni kweli kuwa Kikwete hanayo majina hayo, basi tuna kila sababu ya kuamini kwamba ama TAKURU imezembea sana au ina njia nyingine za kutimiza majukumu yake bila kumhusisha rais wetu ambaye ametangaza kwamba anadhamiria kutokomeza rushwa katika nchi yetu.
Kama TAKURU wanategemea Rais Kikwete atumie ile orodha ambayo ilikabidhiwa kwa Rais Mkapa wakati Jaji Joseph Warioba akikamilisha ripoti yake iliyoshughulikia ‘mianya’ ya rushwa miaka ya 1996/97, basi hata Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ana haki ya kudai kwamba ni vema Rais Kikwete akaishughulikia.
Ni vema vyombo vyote vyenye jukumu la kushughulikia rushwa vikafahamu kwamba, Watanzania wengi wana akili pia ya kuona na kutambua wala rushwa, ingawa hawana mamlaka ya kisheria ya kuchukua hatua ambazo kimsingi zilipaswa ziwe zikitekelezwa na TAKURU.
Hakuna asiyejua kwamba watu wengi wameathirika kutokana na watumishi wa umma kutaka kulipwa rushwa kabla ya kutuhudumia, suala ambalo liliwekwa bayana kwenye Ripoti ya Tume ya Warioba.
Sisi tunaishi na wakubwa ambao maisha yao yanadhihirisha wazi wazi kwamba, wana kula rushwa. Hii ni kutokana na staili na kiasi cha mali waliyojilimbikizia kuzidi mapato yao ya haki. Maofisa wa TAKURU wanaishi katika Tanzania ipi ambayo haina watu wa aina hiyo?
Sisi tunajua kuna miiko ya kazi za umma inayotaka mwajiriwa kutamka na kuorodhesha mali aliyo nayo wakati akiajiriwa, na kuorodhesha mali yake anapoacha kazi au baada ya kila miaka fulani.
Lakini sharti hili linaonekana kupuuzwa na viongozi wengi katika Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ushahidi wa hili ni rais, viongozi wa Awamu ya Tatu walioingia kwa mbwembwe za kutangaza mali zao, wameondoka wakiwa wamefunga midomo.
Lakini si hao tu, hata hawa walioingia sasa madarakani hakuna hata mmoja aliyetangaza mali zake hadharani kama walivyofanya watangulizi wao, wanaotoka katika chama kile kile chenye mtazamo na mwelekeo ule ule. Hili linatueleza nini?
Kama hata TAKURU katika kutekeleza majukumu yake hawafuatilii hilo, sisi umma tunawalipa mishahara ya kazi gani? Kwa kweli Rais anapaswa kuwafukuza kazi.
Katika hotuba zake, Mbowe alijaribu kufuatilia ahadi za Rais Kikwete kwamba angechambua upya mikataba ya uwekezaji na ununuzi wa mali ya umma, ambayo inanuka rushwa.
Ahadi hizi zilitupa matumaini sana sisi ambao majukumu yetu ni kutoa changamoto kwa wenye kutawala. Sasa TAKURU inajibu kwamba “haijawahi kusafisha waliohusika na tuhuma za rushwa”!
Tunaweza kuuliza TAKURU: Ni manunuzi na mikataba gani imechambuliwa na taasisi yenu, na mmeridhika vipi na vipengele vyake? Kama hamjaita nakala za mikataba inayolalamikiwa, mnafanya nini juu ya hiyo mikataba? Mnastahili mishahara yenu?
Mbowe alitaja mikataba mingi ambayo hata kimataifa inatiliwa shaka: Ununuzi wa radar, ununuzi wa ndege ya rais, mikataba ya IPTL na Richmond. Haya yote ni mambo ambayo umma wa Tanzania unadai kupata ufafanuzi.
Na malalamiko haya si siri. TAKURU wanaweza kukiri kwamba hawajachunguza lolote juu ya hii minong’ono?
Kama TAKURU hawajachunguza, basi wanatushangaza sana. Wanatukatisha tamaa. Ole wetu Watanzania.