Nimeona majibu ya Mhe. Mungai, Waziri wa Kilimo kuhusu
hoja yangu juu ya suala la Wakulima wa Mbarali.
Ameyachapisha kama matangazo ya kulipia katika
magazeti mengi ya tarehe 4 Agosti, 2006, nahisi ili
kuweka bayana yote yahusuyo suala hili. Kwa vile mimi
sina uwezo kifedha kuchapisha ufafanuzi wangu kama
tangazo, naomba wahariri wanaotaka haki itendeke,
wachapishe jibu langu hili kama taarifa ya habari ya
kawaida.
Kwa kifupi, katika makala yangu iliyotangazwa na
gazeti la ThisDay, nilishauri kuwa badala ya
kuwafukuza maelfu ya wakulima walioharibu mazingira
Mbarali, Serikali ingepeleka huko wahandisi wa maji na
wataalamu wa kilimo kufundisha na kusimamia hawa
kulima juu ya matumizi bora na endelevu ya maji na
ardhi. Nilisisitiza kuwa jukumu na wajibu wa Serikali
ni kuhakikisha kwamba wananchi wengi iwezekanavyo
wanatumia mazingira yao kwa njia endelevu badala ya
kuwaondoa na kuwapa wachache na wageni, ardhi ambayo
Mwenyezi Mungu amewapa. Nataka kurudia kwamba
Serikali itakuwa inakiuka wajibu wake ikifanya hivyo;
na itakuwa imepoteza huruma na uzalendo wake, na kwa
hiyo kustahili kuondolewa madarakani kidemokrasia.
Nasisitiza pia kwamba sio wakulima wa Mbarali pekee
yao wameharibu mazingira na jawabu ni kuwasaidia
waendeleze mashamba yao kisayansi badala ya kuwaondoa.
Nilimalizia hoja yangu kwa kushauri wapinzani waungane
na wakulima wa Mbarali katika maandamano ya amani
kwenda kumsihi Rais wetu, Mhe Jakaya Kikwete asitishe
mpango huu wa kuwafukuza kutoka katika ardhi waliolima
kwa muda mrefu katika nchi waliopewa na Mwenyezi
Mungu. Siyo kweli kwamba mimi ninawashawishi wakulima
hawa waandamane. Wao wenyewe, walitangaza nia yao ya
kuandamana kwenda Ikulu, kumwomba Rais wao aingilie,
baada ya kutoridhika na majibu ya Serikali
walipokwenda Dodoma. Na mimi nasema ingefaa wapinzani
wawaunge mkono. Mhe. Mungai anaona kwa hilo mimi ni
mchochezi! Kwa mtindo huu, Watanzania wengi watakuwa
ni wachochezi kwa vile hawakubaliani na hatua za Mhe.
Mungai.
Nimeona na kusoma maelezo ya Mhe. Mungai. Ni kweli
kuwa mashamba haya yalikuwa yanalimwa na shirika la
umma (NAFCO) wakati nikiwa Gavana wa Benki Kuu na hata
nilipokuwa Waziri wa Fedha. Kutokana na kushindwa kwa
NAFCO, wananchi binafsi walirudia kulima sehemu
walizokuwa wanalima hapo awali na Mhe. Mungai
anasisitiza kuwa “walikodishiwa”. Ninavyoelewa ni
kuwa wale wanaolalamika kwamba waendelee kuyalima,
wameyalima kwa takriban miaka kumi. Na nasema kwamba
kama Serikali ingewapa msaada wa ugani wa maofisa wa
Kilimo na wahandisi wa maji, wangeendelea kulima
mpunga kwa kutumia miundombinu kama mifereji ya
umwagiliaji na kuzalisha mchele kwa vile vinu vya
ukoboaji vya NAFCO vingeendelea kutumika tu. Serikali
au vyama vya ushirika vya hawa wakulima vingeweza hata
kuvikarabati. Pia nielewavyo ni kwamba mtu akilima
sehemu ya ardhi kwa muda mrefu (kama squatter), sheria
inaruhusu ifanywe ni mali yake halali. Mbona kwa watu
hawa sheria hii haitumiki?
Kama sera na maamuzi ya CCM ni kukumbatia wakubwa
wawili wanaoweza kuchukua hekta elfu sita kila mmoja,
basi huo ni uamuzi wa kutia mayai yote katika kapu moja
(au mawili?) Nielewavyo ni kuwa wakulima wengi kati
ya hawa “wakodishaji” walikuwa wana hekta kama 50 au
chini ya hapo. Maelezo kuwa wawekezaji hawa wapya
“walionunua” watatuongezea ajira si sahihi kwa vile
hata hawa “wakodishaji” walikuwa wanaajiri wasaidizi.
Naamini wafanyakazi wa hawa wawekezaji wawili watakuwa
kama manamba tu, badala ya kuwa wasaidizi.
Licha ya kwamba sina utaalamu wa kukadiria thamani ya
ardhi, naona kwamba hekta hizi 13,400, yaani eka
30,016 za mashamba haya ya Mbarali na Kapunga zimeuzwa
kwa wawekezaji kwa jumla ya shilingi billioni 5.811.
Huu ni wastani wa Shillingi 193,597 kwa kila eka. Je
hii ni bei ya ardhi katika kanda hii ya nchi yetu?
Sitaki kujiingiza katika malumbano na ubishi na Mhe.
Waziri Mungai kwa vile ana majukumu mengi mno, lakini
nasisitiza kuwa ni haki yangu kutoa maoni yanayohusu
maendeleo ya nchi yangu hata kama maamuzi yenyewe
yamefanywa na Serikali iliyochaguliwa. Maamuzi
yanayogusa maisha ya wananchi yanachambuliwa na yeyote
aliye ndani au nje ya Bunge na hivyo si uchochezi.
Mwisho kwa Mhe. Mungai kusema eti nigawie wananchi
wenye ardhi ndogo shamba langu kama naona huruma kwao,
ni kushindwa kujibu hoja na mjadala ulio mbele yetu.
Mjadala ni jinsi ya kuhifadhi mazingira kwa maendeleo
ya Watanzania wengi iwezekanavyo.
Kwa taarifa ya wasomaji, shamba langu la kahawa lina
hekta 20 (eka 52.16) tu. Lilikuwa linamilikwa na
mzungu kabla sijalinunua, na hakuna hata mwananchi
mmoja aliyehamishwa kunipisha! Hata hivyo namkaribisha
Mhe. Mungai kulitembelea aone kilimo cha kisayansi na
matumizi bora ya maji ya kumwagilia, mambo ambayo
nashauri wakulima wa Mbarali wangesaidiwa kuendeleza.
Majirani zangu wa Arumeru wanalitembelea mara kwa mara
na kuona mfano.
Mwisho naomba wasomaji wa makala hii, kwa heshima na
taadhima, waamue kama kweli inaashiria kuzeeka kwangu
vibaya kama huyu Mheshimiwa Waziri anavyodai katika
Taarifa yake kwa Vyombo vya Habari. Namkumbusha Mhe.
Mungai kwamba yeye na mimi tulikuwa wote na nyadhifa
za juu wakati wa Awamu ya Kwanza na naendelea
kumheshimu.
Mungu ibariki Tanzania.