- Haya matunda ya mwingiliano wa kisheria na kukosa dira ya mipango miji ya muda mrefu.
- Gharama za maendeleo ni pamoja na gharama za kufuata sheria na haki za raia.
- Kikwete kuitikia mwito wa ‘wanakijiji’?
Maendeleo ni dhana pana na muhimu mno katika jamii yoyote duniani. Hakuna mtu au jamii yoyote isiyopenda maendeleo,mathalani raia kujenga makazi bora ni maendeleo, raia kulima mashamba ni maendeleo. Nawala hakuna jamii yoyote isiyopenda kujengewa barabara, shule, vyuo, vituo vya afya n.k. Sababu kubwa ya hilo nikuwa yote hayo na maendeleo.
Maendeleo hayaishii hapo tu, maendeleo pia ni pamoja na raia kupewa haki zao stahiki kwa mujibu wa sheria. Jamii isiyoongozwa kwa misingi ya haki na sheria, haiwezi kujisifu kuwa imeendelea ati kwa sababu tu, ina shule nyingi, ina vyuo vingi, ina vituo vya afya vingi, ina barabara safi n.k.
Utawala bora ndio msingi wa maendeleo, utawala bora ni utawala unaoendeshwa kwa misingi ya haki na sheria. Maendeleo yasiyozingatia haki na sheria, kwa vyovyote vile lazima yanazua tafrani katika jamii.
Kwa mfano, pamoja na ukweli kuwa raia wanapenda kupelekewa huduma za afya kwa kujengewa vituo vya afya vya kutosha, lakini kama inapobidi nyumba za baadhi ya raia zibomolewe ili vituo hivyo vijengwe, ni ukweli usiopingika kuwa suala la kuwalipa fidia walibomolewa nyumba hizo halipaswi kuwa na mjadala.
Kimsingi gharama hiyo ndio sehemu ya gharama za utawala bora na maendeleo. Hizo ndizo gharama za utawala unaozingatia si tu sheria, bali haki pia. Tafakuri yangu ya leo imenipeleka huko kutokana na migogoro kadhaa ambayo imekuwa ikiikumba wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi ambayo kwa sasa inaongozwa na Mh. John Pombe Magufuli kama waziri akisaidiwa na Bibi Ritha Mlaki kama Naibu Waziri.
Labda ili kuliezea sura ya tatizo hili kitaifa nitatumia mgogoro huu wa ardhi unaoendelea kati ya wakazi wa mtaa wa Kwembe kata ya Kibamba dhidi ya serikali.
Februari 8, mwaka huu, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Ritha Mlaki, alikana mbele ya bunge mjini Dodoma kwamba, wakazi wa Kibamba, wilayani Kinondoni, hawajawahi kuomba kuonana na waziri ili kuzungumzia mgogoro wa ardhi katika eneo lao. Alisema pia ya kuwa wakazi hao ni wavamizi.
Ritha alikuwa akijibu swali la mbunge wa Chadema viti maalumu, Halima Mdee, aliyetaka kujua hatua iliyofikiwa katika utatuzi wa mgogoro wa ardhi kati ya serikali na wananchi wa Kibamba.
Ni wazi ya kuwa Ritha hakusema ukweli. Na sihoji kusema uongo kwa sababu wakubwa wetu hawa hawajazoea kuitwa waongo hata wanaposema uwongo. Suala la pili na la msingi zaidi ni upofu wa dhana ya utawala bora hususani utawala wa sheria unaonekana kumsibu naibu Waziri huyu.
Kwa yoyote anayefuatilia michakato mbalimbali ya maendeleo ya nchi hii, ikiwa ni pamoja na mgogoro huo wa ardhi katika kata ya Kibamba, ataungana nami kushindwa kuivumilia kauli ya waziri huyo kwamba wananchi hawajataka kumuona kama alivyodai mbunge aliyeuliza swali halina ukweli. Ni kulipotosha bunge na kwa hakika, nikuwadharau wananchi.
Wananchi wamelalamika na kuweka wazi kwamba mwezi Januari, mwaka huu, kamati ya wananchi inayoshughulika na mgogoro huo wa ardhi, iliandika barua ya kutaka kuonana na waziri ambapo waliipeleka kwa waziri huku nakala yake ikipelekwa kwa katibu mkuu na kusainiwa kuwa imepokelewa.
Ni katika hali hii ninashangazwa na kauli ya Naibu Waziri kuwa ofisi yake haijapata barua hiyo. Ninashindwa kuelewa waziri huyu anamaanisha nini kwa kusema ofisi yake haijapata barua hiyo?
Kama barua imefika mlangoni mwa ofisi yake na kupokewa na sekretari wake, nakala ikapelekwa pia masijala na kupokelewa, sasa ifikishwe wapi hata ionekane imefika ofisini kwake? Au ofisi ya naibu waziri inaanzia wapi?
Inawezekana Mlaki alijibu swali hilo kabla ya kuwauliza watendaji wake ndio maana akajikuta anatoa jibu lisilo na ukweli wowote. Tabia hii ni kinyume na maadili ya kazi yake na kama spika wa bunge alivyoahidi wananchi kuwa hatovumilia majibu yasiyo na ufumbuzi wa matatizo ya wananchi.
Hapana shaka kuwa kwa makala hii, spika wetu amepata pa kuanzia kwani Mlaki si tu ametoa jibu lisilo na ufumbuzi wa tatizo bali ameongopa na kwa hilo amekiuka kanuni za bunge na kiapo chake na hivyo kuinajisi hata katiba nchi.
Katika suala la pili,inasikitisha kumsikia naibu huyu akiwaita wakazi halali wa maeneo hayo ambayo historia yake anaielewa vizuri kuwa ni wavamizi, hili ni tusi! Nitusi kutokana na ukweli kuwa Rita amewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni kabla ya kuwa mbunge wa Kawe.Kwa upande mwingine naamini Rita Mlaki anaufahamu wa sheria za ardhi ndio maana Mheshimiwa rais amemteua katika wizara hii. Waziri anapaswa kujua sheria za umiliki wa ardhi ikiwemo ardhi za vijiji ikiwemo ni katika mazingira ya kukaa kwa muda gani milki ya ardhi inamithilika na kuheshimiwa.
Labda ili kuliweka wazi suala hili ni vyema nirejee japo kidogo historia ya eneo lenye mgogoro, kati wakazi na serekali ambayo imetoa ardhi husika kwa Chuo Kishiriki cha Afya Muhimbili baada ya ‘kuinyang’anyaya’ kampuni ya biashara ya mifugo Tanzania (KABIMITA) ambayo ‘ilipatiwa’ ardhi hiyo na serekali mwaka 1978.
Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo walikuwapo hata kabla ya uhuru wa Tanganyika kuanzia miaka ya 1950, mwaka 1975 aliyekuwa Waziri mkuu Mzee Rashid Mfaume Kawawa maarufu kama Simba wa Vita ambae hadi leo ana makazi katika kata hiyo ya Kibamba, aliwapa wakazi hao eneo hilo ambapo kabla ya hapo lilikuwa likimilikiwa na ushirika wa NAFCO na
AISCO.
Baada ya mwaka mmoja,mwaka1976,uongozi wa mkoa wa Dar-es-Salaam uliwapeleka watu katika maeneo hayo kutoka maeneo ya mjini katika kile kilichoitwa “mkakati wa kupambana na umasikini kwa njia ya kilimo na ufugaji” badala ya kukaa mitaani na kuwa wazuraji,vibaka na hata majambazi. Baadaye mwaka 1978 KABIMITA ilikuja kuomba na kupewa na wananchi ruhusa ya kutumia sehemu ya ardhi yao kupitisha mifugo kupeleka kiwanda cha Tanganyika Packers.
Viongozi na wananchi wanaojali wanapaswa kujiuliza, Iweje wananchi ambao walipelekwa na serikali kwenda kuishi maeneo hayo tena chini ya mpango unaoeleweka wazi kabisa baada ya miaka michache waitwe wavamizi na serikali hiyohiyo? Hivi hapa ni nani mvamizi? Wakazi hao ambao baadhi yao walikuwapo hata kabla ya uhuru na wengine walioletwa serikali hiyohiyo au wote waliofuata baadaye?
Tukirudi nyuma, Mlaki kama kiongozi anaonekana si mtu makini, kwanini? Wakati Mlaki ni mkuu wa wilaya ya Kinondoni, alikuwa akiwahimiza wakazi wa maeneo hayo kujenga makazi bora na kulima mazao ya kudumu katika eneo hilo. Leo Mlaki ni naibu waziri wa ardhi, nawaambia watu haohao kuwa ni wavamizi.watanzania wanaojali na wenye kumbukumbu wajiulize, Hivi kuna Ritta Mlaki wangapi?
Inawezekana Mlaki anapenda Chuo kijenge tawi lake hapo, hilo ni jema, nawala katika hilo sina upinzani na Mlaki kwa kuwa hilo ni la maendeleo. Ugomvi wangu na Mlaki ni namna ya kutekeleza ajenda hiyo ya maendeleo.
Lakini hapa kuna masomo mawili makubwa tunaweza kujifunza kuhusu maendeleo katika muktadha wa ardhi. Mosi, kuhakikisha sheria za ardhi haziingiliani na hivyo kufanya ardhi moja igawanywe mara mbilimbili-lakini kutokuingiliana kwa sheria pekee hukutoshi, mfumo wa mawasiliano baina ya serekali kuu na serekali za chini zikiwemo za vijiji unapaswa kuboreshwa. Pili, tunapaswa kama taifa kuwa na dira na mipango miji ya muda mrefu-laiti utamaduni huu ungekuwepo tungejua hata chuo tutakachojenga miaka 20 ijayo tutakijenga wapi. Sasa jiji mathalani la Dar es salaam haieleweki wapi pametengwa kwa ajili ya shule, hospitali, viwanja vya michezo-kila mahali pamevamiwa na kuuzwa. Matokeo yake zinapotaka kujengwa huduma za jamii na miradi mingine binafsi wananchi wasio na sauti wanavamiwa na kuitwa wavamizi.
Lakini suluhisho la sasa kwa suala la Kibamba, naamini ingekuwa vyema kama Mlaki na serikali kwa ujumla kuzingatia sheria na haki katika kutekeleza ajenda mbalimbali za maendeleo ilikuepuka maendeleo yenye kuchochea migogoro katika jamii kwa kuanza na hili.
Sanjari na hili umefika muda muafaka kwa viongozi kuitika wito wa wananchi pindi wanapotakiwa kufanya hivyo kwani viongozi ni watumwa wa wananchi, kitendo cha Mlaki kukataa kuitika wito mpaka wakazi husika wameamua kupitia vyombo vya habari kuomba waonane na rais ni kinyume na dhana ya utumishi. Changamoto kwa Kikwete ni kukubali mwito ilikumfundisha kwa vitendo kiongozi mwenzake dhana ya utumishi.