Yapo maneno mawili ambayo tunapenda kuyatamka kila mara,nayo ni sheria na haki.
Maneno haya si tu kwamba tunapenda kuyatamka bali kuyapata pia katika maisha yetu kama raia, ingawa kipi tuanze kupata kati ya haki na sheria ni mjadala wa kuku na yai.
Wakati wengine wakidai haki zifuate sheria ,baadhi wanadai sheria zifuate haki,hata hivyo pamoja na tofauti za kimtazamo juu ya nini kifuate kingine makundi haya mawili kwa pamoja yanakiri kuwa yote yanataka sheria na haki.
Sheria na haki ni dhana mbili ambazo kimsingi ni vigumu kuzitenganisha, sheria zipo ili kulinda haki na haki hutambuliwa kwa uwapo wa sheria za kulinda haki husika.
Kwa mantiki hiyo hapo juu sheria isiyo toa au kulinda haki ni sheria katili kwa upande mmoja na haki isiyo kwa mujibu wa sheria ni batili.
Nimetafakari haya baada ya pita pita yangu huku na kule na kukutana na watu waliokuwa kwenye mazungumzo yanayo husu upanuzi wa barabara,labda ili kufanya uchambuzi yakinifu ningependa kuelekeza hoja zangu juu ya malalamiko yanayo husu upanuzi wa moja ya barabra kuu nchini, ile itokayo Morogoro kwenda Iringa ,maarurufu kama barabara ya Morogoro.
Pengine kabla sijajenga hoja juu ya barabara hii nadhani ni vyema nikadondoa japo kwa ufupi historia ya kisheria kuhusu barabara kuu nchini ikiwemo hii ya Morogogoro ili hoja zangu ziweze kueleweka vizuri.
Mwaka 1932, wakati wa mkoloni, ilitungwa sheria ya barabara nchini, sheria hii inatambua na kuelezea uwapo wa barabara za umma nchini. Kiambatanisho cha sheria hii kinaitaja barabara itokayo Morogoro mpaka Iringa, maarufu kama barabara ya Morogoro kama barabara ya umma, pamoja na mambo mengine, sheria hii inampa waziri mwenye dhamana na barabara uwezo wa kuamua juu ya upana muafaka wa barabara za umma kwa kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali.
Mnamo mwaka 1967, waziri mwenye dhamana ya barabara nchini alitoa notisi namba 161 kwenye gazeti la serikali, kupitia tangazo hilo upana wa barabara uliongezwa kutoka futi 33 za mwaka 1932 na kufikia futi 75, hii ni kutoka katikati.
Sheria hii ya mwaka 1967 ndio umekuwa msingi wa 'bomoa bomoa' na 'chukua chukua' inayotekelezwa na serikali chini ya mwavuli wa kile kinachojuulikana kama upanuzi wa barabara ya Morogoro. Hata hivyo ni vyema ikumbukwe kuwa tangazo hilo la serikali halikueleza juu ya maeneo yanayo milikiwa na watu binafsi.
Suala la kwanza, utekelezaji wa sheria hauzingatii kikamilifu wakazi ambao wameyamiliki maeneo hayo kabla ya mwaka 1967 ambao kimsingi sheria hii imewakuta,hivyo wanahaki ya kulipwa fidia. Pamoja na ukweli kuwa katika miaka hiyo majengo yalikuwa bado hayajatamalaki lakini sehemu kubwa ya ardhi ilikuwa ni ama mashamba ya watu au maeneo ya ufugaji ambayo kwa muda wote huo yamekuwa yakirithishwa au kuuzwa vizazi hadi vizazi mpaka kufikia hatua ya sasa ya kuendelezwa. Kwa serikali inayofuata sheria zinazojali haki, watu hawa wanastahili fidia kwa kuwa sheria hii iliwakuta.
Suala la pili ambalo serikali hailizingatii ni juu ya wale ambao wameikuta sheria lakini wakapata haki ya kumiliki maeneo hayo baada ya sheria na hivyo kuwafanya kuwa na haki ya msingi ya kudai fidia. Wakazi hawa wanastahiki haki ya fidia pamoja na ukweli kuwa sheria hii iliwatangulia kutokana na ukweli kuwa sheria iliwatangulia na haki ya kumiliki ardhi kama mali binafsi ikafuata.
Kwa msingi huo watu hawa wameipata haki baada ya sheria na serikali inapaswa kuelewa hivyo kwani serikali iliwaacha kwa makusudi wayaendeleze maeneo hayo ambayo ghafla yamewekewa mabango ya kuwataka waondoke maeneo hayo mara moja!
Hawa ni raia ambao serikali imewabariki waendelee kukaa maeneo hayo kwa kuwapelekea huduma za msingi ambazo kisheria hutolewa maeneo halali yanayo tambulika kisheria. Serikali imewawekea miundo mbinu ya umeme, maji, simu na wengine wamepewa mpaka hati miliki na wizara ya ardhi. Iweje wizara ya barabara imwambie mtu kuwa ardhi anayo imiliki si halali wakati amesha milikishwa ardhi hiyohiyo na wizara ya ardhi? Au wizara ya barabara na ile ya ardhi ziko chini ya serikali mbili tofauti?
Maana ukitafakari undani wa suala hili utabaini kuwa serikali iliwapatia haki wananchi hawa ambayo kimsingi kama inataka kuwaondolea haki hii, haina budi kuingia gharama ili kuwanyang'ang'anya haki hiyo.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa kila raia anaamini kuwa serikali anapaswa kufahamu sheria kuliko raia. Serikali isiyo fahamu au isiyosimia sheria haifai! Kwani kwa vyovyote vile haiwezi kuongoza kwa msingi wa utawala wa sheria ambao ndio muhimili muhimu wa utawala bora.
Ni katika mazingira kama haya wananchi wanahimizwa kuchagua wawakilishi wao mathalani,wabunge na madiwani wenye uwezo na utashi wa kujenga hoja katika kulinda na kutetea haki zao za msingi.
Ni viongozi wa namna hiyo ndio wanaoweza kuhakikisha kuwa haki za raia zinazingatiwa wakati wa utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kisheria ikiwa ni pamoja na hili la upanuzi wa barabara ya Morogoro.
Maendeleo yana gharama kubwa ingawa pamoja na ukweli huo hakuna asiye penda maendeleo.Hata hivyo pamoja ukweli huo, ni vyema kabla ya kuyapokea maendeleo hayo ikawa ni aghalabu kujihakikishia mambo kadhaa ili kuepuka maendeleo yenye walakini ndani yake.
Mosi ni vyema gharama au hasara (opportunity cost) zitokanazo na kutafuta maendeleo zisizidi faida zitokanazo na maendeleo hayo. Pili gharama au hasara za kutafuta maendeleo zigawanywe sawia kwa wadau wote wanaonufaika na maendeleo hayo. Na mwisho wa yote ningependa kurudia na kusisitiza kuwa,ili kuleta maendeleo yasiyo na walakini wala mushikeli, ni vyema upanuzi wa barabara uzingatie haki na sheria.