Tanzania ni kati ya nchi tatu barani Afrika zilizoteuliwa na shirikisho la soka Duniani FIFA ambazo kombe la Dunia litatembezwa. Mbali na Tanzania nchi nyingine barani Afrika ambazo kombe hili litatembezwa ni, Nigeria na Afrika kusini,duniani kote kombe hili litapata kutembelea jumla ya nchi 28. Hivyo Tanzania ni moja kati ya nchi tatu Afrika na ni moja kati ya nchi nchi 28 duniani ambazo zitabahatika kuliona kombe hilo.
Mengi yamesemwa kuhusu ujio huu wa kombe hili la Dunia hapa nchini kwetu hasa ukizingatia kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zenye wapenzi wengi wa soka barani Afrika. Hata hivyo yaliyosemwa na Waziri mwenye dhamana na michezo, Profesa Juma Kapuya akiwa sambamba na makamu wa kwanza wa rais wa shirikisho la soka TFF nchini bwana, Crescentius Magori hayawezi kuachwa yapite hivi hivi bila kutafakariwa.
Katika hafla fupi ya kuishukuru kampuni ya coca-cola ambayo ni moja ya wadhamini wa michuano ya kombe hilo itakayo fanyika nchini Ujerumani mwakani,hafla ambayo ilifanyika katika moja ya hoteli maarufu jijini Dar-es-Salaam, MOVENPICK,na kuhudhuriwa na Waziri wa kazi maendeleo ya vijana na michezo, Profesa Juma Kapuya sambamba na Mkurugenzi wa kampuni ya coca-cola ukanda wa Afrika mashariki na kati, bwana-Justin Melvin iliyofanyika hivi karibuni Magori na Kapuya walisema yafuatayo:
"Tanzania ina bahati kuwa miongoni mwa nchi 28 zilizoteuliwa na Shirikisho la soka duniani (FIFA) kutokana na FIFA kubaini jitihada zinazofanywa na nchi hii pamoja na vipaji tele ilivyo navyo katika soka" alisema Magori,akienda mbali zaidi bwana Magori alisema "Tumepiga hatua katika maendeleo ya soka, tunafanya vizuri na ndio maana FIFA imeonyesha kuzitambua jitihada zetu".
"Hii ni fursa ya pekee ambayo coca-cola itakuwa imetupatia,tulikuwa tukitazama kwenye luninga wakati tukio hili la kiulimwengu likifanywa na mataifa 32, sasa tutaweza si tu kuliona bali hata kukishika kikombe hicho na hii ni ishara kuwa tumepiga hatua" alisisitiza Kapuya kwa upande wake.
Kauli hizi, hasa ile ya Kapuya ambae kimsingi ni kauli ya serikali haitofautiani na ile iliyowahi kutolewa na rais wetu, Mh-Ben Mkapa wakati wa ziara ya aliye kuwa rais wa Marekani Bill-Clinton mkoani Arusha, rais wetu alisema, "Ukiona Clinton anakuja Tanzania ujue uchumi umekua"!
Haya ndio Kapuya anataka kutueleza sasa,kuwa kombe la Dunia kuja tu Tanzania hata kama watanzania wanaona nchi yao inaboronga lakini wakubali kuwa soka limepanda,hapana hii haiwezekani.
SWakati Kapuya na Magori wakitutaka watanzania tuamini wanavyotaka, shirikisho la soka duniani FIFA hivi karibuni limetoa takwimu za ubora wa soka duniani ambapo Tanzania imetajwa kuendelea kushikilia nafasi ya 175 katika ubora wa soka duniani, huku ikigalagazwa vibaya na nchi kama Kenya(92), Sudan(93), Rwanda(106), Uganda(109), Ethiopia(128), Burundi(143) na hata Eritrea(172).
Takwimu hizi ndizo zinanifanya nitiliea mashaka kauli za bwana Kapuya na Magori,,kuwa kuja kwa kombe la Dunia Tanzania ni ishara kuwa tumepiga hatua katika soka, kwani kwa mujibu wa takwimu hizo Tanzania ni nchi ya mwisho katika ubora wa soka Afrika mashariki,ni ya mwisho katika nchi za maziwa makuu, na ni ya pili kutoka mwisho katika nchi za Afrika mashariki na kati huku ikiitesa Somalia pekee yake,nayo nadhani ni kutokana na kutokuwa na mfumo wa utawala wa serikali inayo eleweka.
Ndiyo kama kweli matembezi ya kombe hili yamezingatia hatua iliyopigwa na nchi katika kuendeleza soka kwa nini kombe hilo lisingepelekwa Kenya ambayo ni nchi inyoongoza kwa ubora wa soka Afrika mashariki na kati? Kwa nini lisipelekwe Sudan ambayo ni ya 93? na nyinginezo ambazo ziko juu ya Tanzania kisoka hata liletwe hapa kwetu Tanzania ambayo ni nchi ya 175? Si wangelipeleka hata Eritrea ambayo ni ya 172?
Si kwamba ninapinga ujio wa kombe hilo hapa nchini kwetu,la-hasha! nimefurahi sana kombe ilo kuletwa kwetu,ninachopinga mimi ni tafsiri ambayo viongozi wetu wanataka kutusadikisha sisi wapenzi na mashabiki wa soka nchini "ati kuwa kuja kwa kombe hili ni ishara kuwa Tanzania imepiga hatua katika maendeleo ya soka"
Tunapozungumzia nchi zenye mikakati ya kukuza soka Afrika mashariki na kati huwezi kuitaja Tanzania na kama kuna nchi isiyojishughilisha na kukuza soka Afrika mashariki na kati basi Tanzania ni miongoni. Zipo nchi ndogondogo na tena tena jirani zetu kama Rwanda, Burundi, ambazo kila kukicha ni vita lakini wanatufundisha soka.
Tatizo kubwa la viongozi wetu wa michezo na hasa wa serikali wanadhani kila kitu wanaweza kukifanyia propaganda, wanapenda sana sifa za maneno kuliko vitendo, tunapenda sana sifa za siasa kuliko kitu chochote katika maisha yetu, na hili ndilo linarudisha nyuma kasi ya maendeleo katika nchi yetu.
Sikatai kuwa mpira ni siasa, siasa ni kila kitu na kila kitu ni siasa,ingawa siasa ni lazima itafsiriwe katika vitendo zaidi kuliko maneno,ni lazima siasa ilenge zaidi ukweli kuliko propaganda, tabia ya kuendekeza maneno na propaganda imepelekea sehemu kubwa ya jamii yetu kuamini kuwa siasa ni uongo na kila mtu muongo ni mwanasiasa. Hujasikia mtu anakwambia mimi siwezi kukopa mtu fulani kwa kuwa huwa analeta siasa sana katika kulipa?
Hata hivyo nakubaliana na bwana Magori kuhusu kauli yake kuwa "FIFA inatambua uwepo wa vipaji tele vya soka Tanzania" huu ni ukweli usiopingika kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za soka barani Afrika na hata duniani kwa ujumla.
Katika miaka ya 1974-1980 Tanzania ilikuwa moja ya nchi tishio katka soka la Afrika,vilabu vya Tanzania vya Yanga na Simba viliweza kufanya vizuri mno katika michuano ya kimataifa na hata timu yetu ya taifa iliweza kufanya vizuri zaidi, Mwaka 1980 Tanzania ilifanikiwa kushiriki fainali za kombe la Afrika na kufika hatua ya mzunguko wa pili. Magwiji wa soka wakati huo, akina Mohamed Salim, Peter Tino, akina Pondamali na hata rais wa sasa wa shirikisho la kandanda nchini TFF bwana Leodiga-Chila Tenga ni mashuhuda.
Tanzania ilianza kufanya vibaya katika soka mwanzoni mwa miaka ya 1988 ambapo vilabu na hata timu yetu ya Taifa iligeuka kichwa cha mwendawazimu kama alivyo wahi kusema rais mstaafu wa awamu ya pili, mzee Ally Hassan Mwinyi, maarufu kama mzee wa ruksa!
Tangu hapo mpaka hivi leo, Tanzania imekuwa kama nchi iliyopigwa laana katika soka, Tanzania iligeuka kuwa zaidi ya kichwa cha mwendawazimu kichaa kinaweza kumpanda na kukataa kunyolewa, Tanzania imebaki kuwa nchi ya kunyolewa kila siku, kuanzia vilabu vyake na timu ya taifa ndio usiseme, ni msiba!
Hata hivyo ukiongea na wazee wa zamani ambao wamepata kushiriki katika harakati za soka watakueleza wazi kabisa, kuwa zamani soka lilipewa msukumo na serikali,michezo ilikuwa moja ya sera muhimu na nyeti katika nchi hii. Leo suala la michezo limeachiwa vilabu na shirikisho la soka nchini TFF, Serikali haijaweka mkakati madhubuti wa kuimarisha soka nchini. Mfano hai ni jinsi timu zilivyotelekezwa na mikoa yao katika mashindano ya Taifa yanayoendelea.
Zamani michezo ilikuwa sehemu ya masomo shuleni, leo serikali inasema itaboresha michezo, huku serikali hiyohiyo inafuta mashindano ya michezo mashuleni, wapi na wapi? ndio kwani ni mashuleni ambako wanapatikana vijana na watoto waliosheheni vipaji ambavyo ni hazina katika maendeleo ya soka, lakini nani awaendeleze?
Tatizo kubwa la Tanzania elimu yetu haina dira! Kila kukicha watanzania wanalia na ajira, wanalia na uchumi duni. Lakini serikali haielewi kuwa michezo ni sehemu ya zana ambayo ni muhimu sana katika kukuza uchumi na kupanua soko la ajira kama ikiboreshwa. Leo nchi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla zinaingiza mabilioni ya shilingi kutokana na kuwekeza katika soka kupitia mapato ya vilabu na kuuza wachezaji nchi za nje hususani ulaya ambako soka limepiga hatua kupindukia. Uwekezaji sio kwenye dhahabu na almasi tu,serikali iwekeze kwenye soka pia, itafute wawekezaji ndani na nje ya nchi, itawapata tu ,mbona kwenye almasi inawapata?
Zamani soka si tu ilipewa msukumo kitaifa bali kuanzia ngazi ya kijiji, Programmu za soka ziliendeshwa wilayani na vijijini.Karibu kila kijiji kilikuwa na japo viwanja viwili au zaidi vya michezo, leo karibu viwanja vyote vimeporwa,ama kwa kuuzwa kinyemela au kugeuzwa mali ya chama tawala. Ukiuliza unaambiwa hiyo ndio bongo! Ukiwauliza wabongo wenyewe wanakwambia sisi tumesha zoea kwenda hivihivi,kwenda sawa lakini tujiulize kwa staili hii tutafika?
Zamani karibu kila shirika na kampuni lilikuwa na japo timu moja ya soka na makampuni na mashirika hayo yalikuwa yakitoa msukumo wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuwapatia wachezaji posho za kutosha zilzowawezesha kujikimu kimaisha. Ziliwajengea mazingira mazuri ya kazi yao hiyo na wengine kupewa ajira katika makampuni na mashirika hayo. Hii ni tofauti kabisa sasa ambapo huwezi kuamini kuwa timu inayomilikiwa na mgodi ambao kwa sasa ni wa pili kwa kuzalisha dhahabu Afrika lakini wachezaji wanaikimbia timu hiyo kutokana na kulipwa posho ndogo.
Watanzania ni vyema tukaelewa kuwa soka la bongo haliwezi kupanda kwa ama kuona au kushika na hata ingekuwa kunywea kombe hilo! Ni lazima soka iwe moja ya ajenda nyeti kama ulivyo Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA) au Mkakati wa Kurasimisha Raslimali na Biashara za wanyonge (MKURABITA). Ni lazima iwepo programmu maalumu kabisa ndipo tunaweza kupiga hatua katika soka, tofauti na hapo tutaambulia kunawa kama wasemavyo waswahili wetu.
Ndio,tutaendelea kuwa mashabiki na wapenzi wa vilabu vya ughaibuni kama ARSENAL, MANCHESTER, REAL MADRID, n.k. huku tukigeuka wakimbizi kila michuano ya kombe la Afrika na Dunia inapofika. Kweli, kwani haikuwa ajabu mwaka 2000 wakati wa michuano ya kombe la Afrika kumsikia mtu akikwambia, "mimi ni Senegal,mimi ni Nigeria", "mimi huwezi kunitoa Cameroun" na sasa tunajiandaa wengine kuwa Angola, Togo, Ghana na wengine Ivory Coast.
Hivyo basi ningependa watanzania wote wakiwemo, Magori na Kapuya, kuona kuwa, ujio wa kombe la Dunia ni changamoto kwa Tanzania kushiriki kwenye michuano ya kombe hilo au japo lile la Afrika siku za usoni, na kamwe tusihadaike na uteuzi wa Tanzania kuwa moja kati ya nchi chache kabisa duniani ambazo kombe la dunia litatembezwa.
FIFA, haijavutiwa na kiwango cha soka nchini, inawezekana tumepata nafasi hii kutokana na hali ya utulivu tuliyonayo ukilinganisha na nchi nyingine kama Burundi, Uganda, Ethiopia ama wazungushaji wanakuja kutalii mbuga za wanyama, mito, maziwa na kamwe si soka la bongo.