Kikwete: Mafiga Matatu - ndio!, lakini...
Kuna mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema binadamu mwenye akili ya kiasi hujadili kuhusu watu, binadamu mwenye akili za kawaida hujadili kuhusu matukio na binadamu mwenye akili zilizotukuka hujadili kuhusu masuala. Makala hii ni enzi kwake na itajadili masuala, na si kujadili Kikwete na wengine. Lengo ni tutafakari masuala kadhaa "chagua mafiga matatu, "Siasa si ushabiki wa Simba na Yanga" na "chagua Chama kwanza!" Haya yamekuwa yakisemwa sana wakati huu wa kampeni. Nitayajadili katika muktadha wa demokrasia na maendeleo nchini.
Ngoja nichokoze tafakuri kwa kutumia habari iliyotoka kwenye gazeti la Mtanzania la Novemba 29, 2005 iliyobeba kichwa "Kikwete awapasulia jibu Keenja na Rita". Ndani ya habari hii tunaambiwa Mgombea wa urais wa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amewapasulia wazi wagombea wake wawili kuwa hawauziki kwa kuwa wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi wa majimbo yao sambamba na kushindwa kuchangia katika kuwatatulia kero zao za msingi.
Hii ni habari ya kutia matumaini. Ni ishara ya uwazi na uadilifu. Lakini tunapata pia habari ya kukatisha tamaa kwamba pamoja na kutambua udhaifu bado Kikwete akatoa hoja ya kwamba hawa bado wanapaswa kuchaguliwa ili CCM iweze kupata "mafiga matatu" kwani "chagua Chama kwanza" mambo mengine baadae. Na hoja inaendaelea kujengwa kwenye magazeti mengine kwamba kuna haja ya kuondoa ushabiki wa Simba na Yanga ndani ya CCM ili hata wale wanachama ambao wamekuwa wazalendo na kuunga mkono wagombea bora bila kujali wako chama gani waweze kurejea "kundini" kwa kuwaunga mkono wagombea wa CCM. Haya yamejadiliwa katika kikao cha Kinondoni lakini ni mambo ambayo yalijadiliwa, yanajadiliwa kupitia makala hii na yaendelee kujadiliwa tunapoelekea kupiga kura Desemba 14.
Tuanze na suala la "mafiga matatu". Hoja inayotolewa na Kikwete na wengine ni kwamba wananchi wachague wagombea kwa mtindo wa mafiga matatu. Hoja ya nyongeza ni kuwa mafiga hayo yatoke CCM. Mafiga hayo ni Rais, Mbunge na Diwani. Katika suala hili, nakubaliana na hoja ya kwanza lakini sikubaliani na hoja ya pili.
Mpishi yoyote makini hulenga kuhakikisha mafiga yanamwezesha kupika. Mpishi makini huangalia mafiga yanayowezesha chungu kukaa vizuri, chakula kisimwagike, kiive, apakuwe, kiliwe. Mpishi makini hana lengo la kuhakikisha mafiga yako sawa sawa lakini mbinu ni kuhakikisha yapo sawa. Nia ni kuona chungu hakipinduki. Maendeleo ni chungu cha chakula, kiongozi ni figa, kura ni Mpishi. Mpishi makini hachunguzi figa kwa rangi, anaangalia figa lililo sawa ambalo litawezesha chungu kukaa vizuri. Mpiga kura makini anapaswa kuchangua kiongozi bora ili apate maendeleo. Kikwete anakiri kabisa kuwa mafiga yake ni mabovu. Vipi amlazimishe Mpishi kuyapikia? Ndio maana nasema nakubaliana na hoja ya mafiga matatu kama zana ya kukibeba chungu cha maendeleo. Mpishi makini akikosa mafiga bora ndani ya nyumba yake anatoka kwenda kutafuta na akikosa huazima kwa jirani. Upinzani umeanzishwa kutoa viongozi mbadala,haya ni mafiga bora yanayopaswa kuchaguliwa. Tukiendelea kuyaacha mafiga yale yale ambayo tunaona ni mabovu, chungu hakitakaa, kitamwagika na tutalala na njaa ya maendeleo. Tutaendelea kukosa viongozi wenye kuwajibika na kuhamasisha nguvu za kutatua kero za wananchi.
Suala la pili ni "Siasa si ushabiki wa Simba na Yanga". Hii ni dhana nzuri ingawa sikubaliani na ilivyotumiwa. Moja ya sifa ya msingi ya shabiki wa timu ni kuishabikia timu katika hali na mazingira yoyote. Haya ndio yanayotokea kwenye ushabiki wa Simba na Yanga. Katika hili shabiki huwa sambamba na timu hata pale timu inapofungwa kupindukia. Shabiki huendela kupiga debe hata pale timu inapochezesha wachezaji wabovu. Lakini Kikwete na wengine wanasema siasa si ushabiki wa Simba na Yanga. Nakubaliana nao. Kama hivyo ndivyo, basi wana CCM hawapaswi kulazimika kuishabikia timu yao hata pale inapofungwa kupindukia. Hawapaswi kuipigia debe hata pale inapochezesha wachezaji wabovu.
Viogozi walioshindwa kuwatumikia wananchi na kuchochea maendeleo wameifungisha timu yao. Tukiweka ushabiki wa Simba na Yanga pembeni wachezaji wa namna hii wanastahili kupumzishwa.
Suala la tatu ni "Chagua Chama kwanza". Hii ni hoja pofu. Ni hoja finyu. Ni hoja ya kibinafsi. Tunachopaswa kutazama kama watanzania ni utaifa na uzalendo. Tena hata haya si ya kuyatazama kwanza. Anachopaswa kutazama mpiga kura ni neema na maendeleo na si Chama. Mpiga kura anachopaswa kutafakari anapokwenda kupiga kura Desemba 14 ni kwa vipi kura yake inamwezesha kupata maendeleo na hatimaye neema. Ndio maana hata baba wa Taifa aliwahi kutamka "CCM si mama yangu". Chama kimoja hakiwezi kuwa mama wa wote na wala hakiwezi kabisa kuwa mama wa yote. Kikwete na wengine kumbukeni wosia wa baba; "ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora" Wala hakusema ili tuendelee tunahitaji chama. Siasa safi aliyosema Mwalimu ni siasa ya uwajibikaji, sio siasa ya kulindana hata pale wajibu unapotelekezwa. Uongozi bora aliousema Mwalimu ni uongozi wa utumishi na uadilifu sio uongozi wa kushindwa kutekeleza ahadi. Mwalimu alitoa wosia kwamba katika kuchagua viongozi tuchague viongozi bora watakaotokana na mchakato wa siasa safi. Nyerere alipinga kwa vitendo suala la "chama kwanza", mwaka 1995 Mwalimu pamoja na kumpigia debe Mkapa kwenye urais, hakuendekeza "chama kwanza" kwani kwenye ubunge wa Musoma vijijini alimpigia debe Ndobho wa upinzani na hatimaye akamshinda mgombea wa CCM. Mfano mwingine mzuri ni wananchi wa Karatu, Hai na Kigoma Ujiji ambao wamechagua CHADEMA na kuona mwanzo mzuri wa mabadiliko. Inawezekana, timiza wajibu wako!