Tamko la J.J. kujibu mapigo ya Makamba
Tanzania Daima la Machi 29, 2005 (toleo na. 118) limeripoti maelezo ya Makamba akijibu hoja zangu nilizotoa kuhusu mkoa wa Dar es salaam kuchangisha mamilioni ya shilingi katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Naomba nianze kwa kusema kwamba namheshimu sana Makamba kama Mkuu wa Mkoa ambao mimi ni mkazi wake lakini zaidi kama "babu" yangu. Pia nirejee tena kauli yangu kwamba sina nia ya kubeza michango ya kimaendeleo kwa sababu mimi binafsi ni mwanaharakati wa maendeleo.
Pili naomba nimpongeze Makamba kwa majibu yake, ni viongozi wachache sana wenye unyenyekevu wa kujibu malalamiko yanayotolewa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa kimaendeleo.
Hata hivyo, nasikitika kwamba Makamba hajajibu hoja za msingi nilizozibainisha. Bado nasisitiza kwamba uamuzi wa uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam kuwasau wananchi muda wote na kukurupuka kipindi cha uchaguzi ni ulaghai.
Naomba Makamba akiri kwamba toka uongozi wake uingie tena madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2000, kwa kumbukumbu zangu, hakuna shule hata moja ya sekondari mpya waliyoijenga katika Jimbo la Ubungo zaidi ya Kiluvya. Vipi leo waamue kujenga shule 11 katika mkoa wa Dar es salaam kwa mkupuo? Nasema uamuzi huu unalenga kuwaghilibu wananchi kwamba serekali inawaletea maendeleo kwa kasi.
Makamba anajisifu kwa ahadi ya kupeleka wanafunzi 3000 sekondari kwa mkupuo mwaka huu. Wakati utathibitisha ukweli wa ahadi hii. Lakini hoja ambayo Makamba anapaswa kuijibu ni kwamba kama uongozi wake ungetumia busara na kuandaa chakula kama hicho cha hisani mwaka 2001 ungeepusha vijana zaidi ya 15,000 kukosa elimu ya sekondari. Hii inadhihirisha hoja yangu kwamba uongozi "ulisinzia" miaka yote hiyo na "kukurupuka" majuzi ukiwa na nia ya "kulaghai" wapiga kura. Napenda kumkumbusha Makamba kwamba "usingizi" wa viongozi wenzake umesababisha vijana takribani 37,000 waliofaulu darasa la saba kukosa nafasi za kuendelea na sekondari kwa kipindi hiki cha miaka mitano. Hawa ndio vijana walioko mitaani wanaokimbizwa na "askari wake wa jiji"! Mimi naamini, kwa misingi wa mapato na wadau mbalimbali wa maendeleo 'waliojazana' katika mkoa wa Dar es salaam, na kwa kuthibitishiwa na chakula cha hisani kilichofanyika majuzi - Makamba alikuwa na uwezo wa kujenga shule ya sekondari katika kila kata ya mkoa wa Dar es salaam.
Makamba anapaswa pia kujibu, kwa nini achangishe pesa kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana kipindi hiki wakati ambao malalamiko yaliyo "mezani" kwake ni kwamba pesa za mikopo zipo kwenye bajeti za manispaa ila tatizo ni kwamba haziwafiii walengwa? Tena cha kusikitisha zaidi ni kwamba kwa miaka kadhaa mfululizo manispaa zimekuwa "zikilalama" kwamba fedha hizi hubaki kutokana na kukosa wanawake na vijana "mwafaka" wa kuwakopesha. Wanawake na vijana waamini vipi kwamba hizi za sasa zitatolewa kwa namna inayostahili.
Wakati huohuo, sitaki kuamini kwamba kauli ya "akishinda ubunge nitakuwa bosi wake" imetoka kwa Makamba, kama ndivyo basi namtaka Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aombe radhi. Kauli kama hii ni ya kijinga na inaashiria "ulevi" wa madaraka. Naomba nimkumbushe Makamba kuheshimu demokrasia inayotaka mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mitatu ya dola. Kama mbunge nitakuwa katika mhimili wa bunge (legislature) na wala sitegemei kuwa mtumwa wa Makamba (utawala). Kauli ya Makamba inawakilisha hisia za viongozi wengi wa serakali ambao wamediriki kujiamini wako juu ya bunge na hivyo kulifanya bunge kuonekana kama "kibogoyo" - chombo kisicho na "meno". Naomba nimhakikishie Makamba kwamba nitakuwa mtumwa, mtumishi na mwakilishi wa wakazi wa Ubungo na umma wa watanzania kwa ujumla na si vinginevyo.
Naomba kuchua fursa hii kumwomba Makamba ajibu hoja aliyonukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba pamoja na mambo mengine mamilioni ya shilingi yaliyochangishwa siku hiyo yanalenga pia kuchangia mkutano mkuu wa CCM. Kama hili ni kweli, basi chakula hicho cha hisani chini ya Jina la Rais kilikuwa ni "takrima" na "ulaghai". Wananchi waliitwa bila kujali itikadi na manispaa zilichangia milioni 45 za walipa kodi ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali.