Umaskini si kinyume cha haki za binadamu tu, ni matusi kwa ubinadamu! Umaskini kwa vijana na watoto ni maangamizi ya halaiki kwani ni umaskini wa leo, kesho na kesho kutwa. Shirika la kuhudumia watoto linabainisha kwamba watoto na vijana wanaokua kwenye umaskini na kukosa elimu, huduma ya afya, habari na fursa wana uwezekano mkubwa wa kubaki maskini na kuna uwezekano mkubwa kwamba na watoto wao nao watakuwa maskini.
Umaskini unazidi kuongezeka. Vijana wengi wanazidi kuwa walalahoi. Kama unabisha nenda mitaani, waulize vijana-katika kila kumi, sita ni masikini kwa viwango vya kimataifa, wanne kati yao ajira kwao ni ndoto! Hivyo kizazi kipya kinapaswa kutwaa jukumu la kuleta maisha mpya.
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA) mpya umeandaliwa. Tumshukuru Mola. Uchambuzi huu ulishatolewa, maoni yakawasilishwa na wadau mbalimbali kwa mamlaka zinazohusika. MKUKUTA umetoka, maoni ya wadau yamejumuishwa kiduchu. Bado mkakati haulengi kikamilifu asili ya umaskini-watanzania kunyonywa raslimali na maliasili zao pamoja na mgawanyo hewa wa mafao ya kiuchumi. Bado tutaona mrahaba wa kinyonyaji katika sekta ya madini na mishahara ya kukatisha tamaa katika sekta ya ajira. Nimekumbuka, si lengo la makala hii kuuchambua mapungufu na ubora wa MKUKUTA.
Suala ni utekelezaji si utelekezaji! Viongozi na wadau sasa wameanza kutambua mchango wa vijana katika hili. Lakini vijana tutekeleze namna gani? Tunaambiwa-kijana mmoja mmoja na asasi za vijana. Sawa! Lakini jeshi lisilo na uratibu linajiharibu. Kila kijana akitoa nguvu kivyake vyake, mchango wa vijana katika kutekeleza MKUKUTA utakuwa matone ya sukari katika bahari.
Hapa ndipo inapohitajika sera!Bila ya sera ya vijana MKUKUTA utagonga ukuta. Tanzania tuna sera ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996. Swali lenye jibu tata-bado tuna sera ya maendeleo ya vijana nchini? Wataalamu wa demokrasia na maendeleo wanasema sera ya sekta ikizidi miaka mitano inakufa, sera yetu ya vijana bado iko hai?Serekali iligundua jibu, ikaanza mchakato wa kuirejea sera hiyo kwa ajili ya kuiboresha miaka ya hivi karibuni. Lakini matokeo yamefutikwa. Unapopewa kitu kisicho kufaa ni sawa na asiye na kitu. Hatuna sera ya maendeleo ya vijana. MKUKUTA umetoka, vijana tunapaswa kutoa mchango wetu kufanikisha utekelezaji. Kama hivyo ndivyo, sera ya mpya ya vijana itolewe. Sera hii ijumuishe yale ambayo vijana tunapaswa kuyafanya kuchangia katika kutekeleza MKUKUTA.
Hata tukiwa sera ya maendeleo ya vijana kama msahafu au biblia inaweza kubaki kama mawazo. Tunapaswa kuwa na chombo cha utekelezaji. Tunapaswa kuwa na chombo cha kuratibu. Tunahitaji Baraza la Vijana Tanzania (BAVITA).
Wapo ambao watahoji, BAVITA la nini?Mbona tuna idara ya vijana, mbona tuna asasi na vikundi vya vijana, mbona vijana wamejaa mitaani na vijijini? Idara ya vijana ni chombo cha utekelezaji cha wizara ya kazi, maendeleo ya vijana na michezo. Haijaundwa kuwa chombo huru cha vijana. Mara baada ya kufungua mlango wa vyama vingi vijana watanzania tumekosa chombo cha kutuunganisha na kutuwakilisha bila kujali tofauti zetu. Tumepoteza hata uanachama katika vyombo mbalimbali vya kimataifa. Yanayoendelea ni hekaya za Abunuwasi!
Nilisema, bila kuwa na BAVITA mchango wa vijana katika kutekeleza MKUKUTA unakwenda ki-mimi mimi na ki-kule kule. BAVITA ndio chombo kinachopaswa kupewa mamlaka ya kuandaa na kuelekeza utekelezaji na ufuatiliaji wa sera ya maendeleo ya vijana nchini. BAVITA litahakikisha wadau mbalimbali ikiwemo asasi za vijana wanatimiza wajibu wao wa kuboresha maendeleo ya vijana zikiwemo harakati za vijana kutekeleza MKUKUTA.
Lakini BAVITA limeandelea kuwa ahadi ya kuonyeshwa pepo. Harakati zilianzishwa vizuri na vijana, hatua ilifikiwa ya kuunda. Serekali ikateka hoja mwaka 1998 kwenye Kongamano la Iringa. Ikaundwa kamati isiyomaliza kazi yake wala muda wake. Kamati ambayo sasa wajumbe wake wamevuka umri wa ujana na baadhi yao kwa sasa hawako tena nchini. Kilichofuata ni usanii,makongamano na warsha za kitaifa karibu kila mwaka kujadili kuunda BAVITA. Hata Taifa la Tanzania halikuchukua muda mrefu hivi kuundwa. MKUKUTA unataka utawala na uwajibikaji ili kuondoa umaskini. Kinachoendelea ni u-hewala na uharibikaji! Nasisitiza tena, bila baraza MKUKUTA utagonga ukuta.