Utangulizi
Februari 6 mwaka 2008 Kamati Teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoundwa tarehe 13 Novemba, 2007 iliwasilisha taarifa yake bungeni. Kamati hiyo iliundwa kuchunguza mchakato wa Zabuni ya Uzalishaji umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond Development Company LLC ya Houston, Texas Marekani mwaka 2006.
Kutokana na uchunguzi wa kina ulioanishwa katika taarifa ya Kamati Teule, Bunge lilijulishwa kuwa mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa MW 100, uliopelekea Richmond Development Company LLC kuteuliwa na hivyo kusaini mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tarehe 23 Juni 2006 na baadaye kurithiwa na Dowans Holdings S.A tarehe 23 Desemba 2006, uligubikwa na vitendo vya ukiukwaji taratibu, kanuni na sheria za nchi na hivyo kujenga kiwingu cha mashaka ya upendeleo, ubadhirifu na rushwa ambavyo vimechangia kumuongezea mwananchi mzigo wa gharama za umeme.
Aidha, Kamati Teule ilithibitisha kuwa uteuzi wa Kampuni dhaifu kifedha, kiufundi na kiuzoefu na ambayo haina usajili Marekani wala Tanzania kama kampuni yenye ukomo wa hisa, yaani Richmond Development Company LLC, ulitokana na kubebwa na viongozi waandamizi wa Serikali.
Kamati hiyo ilibaini mapungufu makubwa na kamati ilitoa mapendezo mbalimbali na kutoa maelekezo kwa serikali kuhakikisha yanatekelezwa; Baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunda Kamati ya kusimamia utekelezaji huo.
Huu ni mwezi Juni, 2008 takribani miezi minne imepita toka Kamati iwasilishe taarifa yake Bungeni. Baadhi ya mapendekezo ya msingi yaliyomo kwenye kamati hayakuhitaji muda mrefu kiasi hiki kuweza kutekelezwa lakini mpaka hivi sasa serikali iko kimya kuhusu utekelezaji wake. Ni wakati wa kuyatafakari tena mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge na maazimio ya Bunge baada ya mapendekezo hayo.
Wananachi tutangaze wazi kuwa hakuna mkataba kati yetu na Richmond/Dowans:
Kamati tuele iliweka bayana kuwa, Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC ulikuwa wa uzalishaji umeme wa dharura kipindi ambacho nchi ilikuwa katika hali ngumu ya ukame uliokausha mabwawa yote ya kuzalishia umeme. Kamati Teule iliitaka Serikali kutathmini upya uhalali wa kuwepo na kuendelea kuwepo na mkataba huo kutokana na udanganyifu bayana uliofanywa na Richmond Development Company LLC kuhusu uwezo wake kifedha, kiufundi, na uzoefu wake katika masuala ya uzalishaji umeme; usajili na uwepo wake kisheria kama kampuni halali yenye ukomo wa hisa nchini Marekani na Tanzania; uhusiano wake kisheria na Kampuni kubwa ya Kimataifa ya Pratt & Whitney na utambulisho wa Mzungu mmoja kwa jina la John Perun kama mwakilishi wa Pratt & Whitney, mambo ambayo Kampuni hiyo kubwa ya Kimataifa imeyakanusha vikali.
Kamati Teule ilishuhudia bei za mitambo hiyo jijini Houston, Texas Marekani kwa watengenezaji kiwandani ikiwemo kampuni ya Kawasaki Gas Turbines – Americas ambayo iko chini ikilinganishwa na bei zinazotolewa na mawakala hao, jambo ambalo lingeiwezesha Serikali kununua na kumiliki badala ya kukodi kwa muda mfupi na kwa gharama kubwa. Mathalan, MW 105 zingepatikana kwa kununua mitambo sita ya MW 17,5 kila mmoja kwa gharama ya shilingi bilioni 56.25 badala ya shilingi bilioni 108.7 tulizotandikwa na Richmond Development Company LLC mitambo hiyo ikibaki mali ya wakodishaji. Kamati Teule ilithibitisha kwamba kauli iliyokuwa inatolewa mara kwa mara na baadhi ya viongozi wote tuliowahoji kwamba kipindi hicho cha ukame haikuwa rahisi kupata mitambo hiyo na ilikuwa ikigombaniwa na nchi nyingi kauli hiyo ilikuwa sio ya ukweli na upotoshaji mkubwa.
Ilielezwa kuwa Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A, kama ilivyo mikataba kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals inatoa unafuu usiostahili kwa makampuni hayo ya umeme na kuiumiza TANESCO na hatimaye watumiaji na walipa kodi kimapato, k.m mikataba hiyo kuwa na vipengele vya kuibana TANESCO kuyalipia makampuni hayo kodi zinazohusika na uendeshaji (operations), matengenezo/marekebisho ya mara kwa mara ya mitambo (maintenance) gharama za bima, ada za mawakili na washauri elekezi (consultants) gharama za mafuta na gesi ya kuendeshea mitambo, gharama za ukodishaji mitambo (capacity charges) ambazo TANESCO hulipa kila mwezi si chini ya wastani wa shilingi bilioni 2 kwa kila kampuni, izalishe au isizalishe umeme. Kamati Teule ilitoa rai kwa Serikali kuwa mikataba yote hii ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo mikataba ya madini inavyopitiwa upya sasa na Serikali. Bila kufanya hivyo, mzigo mkubwa wa gharama za umeme utawaelemea wananchi.
Lakini mpaka sasa serikali imeendelea kuutambua mkataba huu kwa niaba ya watanzania, miezi minne baada ya pendekezo hili. Ni wakati wa wananchi kuungana pamoja kutamka wazi kwamba hatuutambui mkataba huo; kwa kuwa umeingiwa na wawakilishi wetu kwa hila la bila ridhaa yetu. Hivyo, ni vyema mitambo yao ikaondolewa katika Jimbo la Ubungo.
Tushinikize malipo ya milioni 152 kwa siku kwa Dowans yasitishwe mara moja; fedha zilizolipwa mpaka sasa zirejeshwe
Kamati Tuele ilieleza bayana kuwa, Madhumuni ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC yalikuwa kuzalisha umeme wa dharura kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12) tu. Muda huo ungeweza kuongezwa baada ya kutathmini hali ya ongezeko la maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme nchini. Kabla ya muda wa tathmini hiyo haujafikiwa, wakati majadiliano yakiendelea GNT ikaongezea Richmond Development Company LLC muda wa kukodi mitambo hiyo kuwa miaka miwili (2). Kamati Teule haikuona vielelezo vyovyote vilivyojenga uhalali kwa GNT kuongeza muda huo. Uamuzi huo umeliongezea Taifa mzigo mkubwa wa gharama zisizokuwa za lazima. Mathalan, kwa upande wa capacity charges tu, TANESCO itailipa Dowans Holdings S.A jumla ya shilingi bilioni 54.8 kwa kipindi kilichongezwa cha mwaka mmoja. Aidha, GNT ilishindwa kutambua ulaghai wa Richmond Development Company LLC kuhusu mwakilishi wa Pratt & Whitney na hivyo kuamini karatasi ambayo ilikuwa haijathibitishwa na mawakili na diskette zenye picha za mitambo ya Pratt & Whitney, vielelezo ambavyo Kamati Teule iligundua na kuthibitisha kuwa vilikuwa vya kugushi. Vilevile, bila kujali kwamba TANESCO ingelezimika kuilipa Richmond Development Company LLC shilingi milioni 152 kwa siku kama gharama ya kuweka vifaa vyao nchini, GNT ikakubali kilegelege kuitoza Richmond Development Company LLC shilingi milioni 12 tu kwa siku kama fidia kwa ucheleweshaji wa kuanza kuzalisha umeme kulingana na tarehe iliyokubalika kwenye mkataba.
Tunasikitika kwamba hata baada ya kuelezwa mambo yote hayo, serikali bado imeendelea kuilipa kampuni ya DOWANS kiasi cha fedha sawa na takribani milioni 152 kila siku. Hivyo tunataka serikali iache kutumia vibaya fedha zetu na isitishe malipo hayo mara moja na kudai fedha zilizolipwa mpaka sasa zirejeshwe.
Mikataba iwekwe wazi kwa wananchi wa eneo ambalo mradi/uwekezaji unafanyika ili kujua haki na wajibu wao
Kamati tuele ilipendekeza wazi kuwa; Utaratibu tuliourithi kutoka kwa wakoloni na kuuzoea wa kuiona mikataba ya kibiashara kuwa ni siri hata kwa walipa kodi wenyewe na kuwa uwanja wa pekee wa watendaji, ambao Waziri wa Mipango Uchumi na Uwezeshaji Mhe. Dk Juma Ngasongwa (Mb) aliusifia bungeni tarehe 19 Aprili 2007 kuwa best practice wakati akijibu swali la Mhe. Masolwa C. Masolwa (Mb) Mbunge wa Bububu, umepitwa na wakati na unakiuka misingi ya demokrasia na uwajibikaji. Matokeo ya utaratibu huu ni kuwepo kwa mikataba mibovu inayoficha vipengele vinavyoibebesha Taifa mizigo mikubwa ya gharama zisizokuwa za lazima.
Wakati umefika sasa wa wananchi wa eneo husika kudai kuonyeshwa mikataba ya kibiashara ya maeneo yao ili kujua haki na wajibu wao. Mathalani, kuna malalamiko ya wakazi wa Jimbo la Ubungo wanaoishi karibu na mitambo ya Richmond/Dowans kuhusu masuala ya joto, mionzi na kelele zinazotokana na mitambo hiyo. Wananchi hao wanalalamikia kuwa waliahidiwa kulipwa fidia na kuondolewa katika maeneo ya jirani na mitambo hiyo. Maswali ya kujiuliza; Je, tathmini kamili ya madhara katika mazingira(EIA) ilifanyika kikamilifu kabla ya mradi huo? Je, suala la wananchi kulipwa fidia lilikuwa sehemu ya mkataba? Kama mkataba huu ungekuwa wazi mapema ikiwemo kwa wananchi wa jimbo la Ubungo, ni wazi kuwa wananachi wangeelewa haki na wajibu wao katika mkataba husika.
Serikali iache kuigopa TAKUKURU, ichukue hatua ya kubadili uongozi wa taasisi hiyo
Taarifa ya Kamati Teule ilidhihirisha wazi jinsi Taifa lilivyotumbukizwa kwenye hasara kubwa kutokana na mkataba huo wa Richmond Development Company LLC na Dowans Holdings S.A, kinyume na taarifa iliyotolewa na TAKUKURU (wakati huo TAKURU) kwamba Taifa halikupata hasara yoyote. Taarifa ya TAKUKURU ililenga kuficha ukweli (white wash) hivyo ikaishia kujikanganya kwa kukiri kuwepo kwa mapungufu lakini yasiyokuwa na athari. Taarifa hiyo imemong’onyoa kwa kiasi kiasi kikubwa hadhi na heshima ya chombo hiki muhimu cha kitaifa kilichopewa dhamana ya kupambana na rushwa na sio kuipamba ili kurejesha heshima ya umma katika taasisi hiyo. Kamati teule ilipendekeza mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi hiyo.
Mpaka sasa mabadiliko hayo hayajafanyika, na Mkurugenzi wa TAKUKURU ameendelea kuwa Edward Hosea ambaye ametuhumiwa hadharani kwa kuigeuza TAKUKURU kuwa Taasisi ya kulinda na kutetea rushwa. Ni wakati wa wananchi kutaka serikali iache kuigopa TAKUKURU na kuchukua hatua za haraka za kubadili uongozi wa Taasisi hiyo.
Mwakapugi, Mrindoko na watendaji vinara wachukuliwe hatua haraka
Kamati Teule iliainisha katika taarifa yake vitendo vya ubabe, ujeuri na kiburi vilivyofanywa na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini alimradi kampuni waliyoitaka iteuliwe kiasi cha kupindisha hata maamuzi ya Baraza la Mawaziri bila wasiwasi wowote, kukaidi ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma mara tatu mfululizo na kinyume na maagizo ya Baraza la Mawaziri lililotaka Sheria ya Ununuzi wa Umma izingatiwe, kukiuka sheria kwa makusudi kwa kuingilia mchakato wa zabuni wa taasisi nyingine ya ununuzi, kuvipuuza vyombo vya ndani vya maamuzi vya TANESCO (Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Zabuni n.k), kuilazimisha Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuridhia maamuzi yaliyofanywa na Wizara ya kuibeba Richmond Development Company LLC kinyume cha sheria na taratibu n.k. Wizara hiyo katika kuibeba Richmond Development Company LLC ilifikia hatua ya kupotosha kwa makusudi ushauri wa Wizara ya Fedha uliozuia malipo ya awali ya Dola za Kimarekani Milioni 10 katika Barua ya Dhamana ya Benki ya Richmond Development company LLC. Kamati Teule ilipendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha (Mb) na Katibu Mkuu Ndugu Arthur Mwakapugi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu kwa kuliingiza Taifa kwa makusudi kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara kubwa kwa nchi. Aidha Kamishna wa Nishati Ndugu Bashir Mrindoko naye ilipendekezwa achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya wa Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao ulijulikana dhahiri na Wizara toka mwaka 2004 kwenye mkataba wa Bomba la Mafuta. Ndugu Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua kampuni hiyo kusitisha mkataba wake na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura haujaanza.
Wakati umefika wa wananchi kuitaka serikali kuwachukulia hatua za kinadhamu Mwakapugi, Mrindoko kama ilivyopendezwa na Kamati teule. Katika hali ya kawaida ya uwajibikaji, ilitarajiwa Rais Jakaya Kikwete, mara baada ya Waziri Mkuu Pinda kuunda Kamati ya kusimamia utekelezaji wa maazimio ya Bunge kutokana na Taarifa ya Kamati Teule; angewachukulia hatua wateule wake, hususani makatibu wakuu waliohusika na kashfa hii kwa kuwasimamisha kazi wakati wote ambapo kamati inatafakari hatua za kinadhamu zinazopaswa kuchukuliwa.
Ni wakati wa kuchukua hatua
Ni wakati wa wananchi kuchukua hatua. Kwa kuwa makao makuu ya TANESCO yako jimbo la Ubungo; na kwa kuwa Kampuni ya Richmond ilikuwa Ubungo; Na kwa kuwa Kampuni ya Dowans iko Jimbo la Ubungo. Ni wakati wa wakazi wa Ubungo kwa niaba ya watanzania wengine, kujiunga pamoja chini ya ‘falsafa ya nguvu ya umma’; kuiwajibisha serikali kutekeleza mapendekezo ya Kamati Tuele ya Bunge mapema iwezekanavyo. Kwani mapendekezo hayo, si ya kamati tena, maamuzi ya wananchi kupitia maazimio ya Bunge. Ikumbukwe kwamba wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hivyo baada ya mapendekezo kupitishwa kama maazimio; ni jukumu la kila mdau kuhakikisha yanatekelezwa.