lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

20 Juni 2007

Tanzania, CHADEMA, CCM na mjadala wa falsafa na itikadi
Lipi ni jibu? (2)

na

John Mnyika

Wiki iliyopita nilianza kuchangia mjadala ulioibuka kuhusu falfafa na itikadi. Katika makala yangu iliyopita nilijenga hoja kadhaa. Mosi; nilionyesha bayana kwamba viongozi mbalimbali wa serikali na CCM wanatoa kauli zinazokinzana kama chama hicho kinafuata itikadi ya ujamaa na kujitegemea au la. Pili; nilitoa ushahidi wa wazi kwamba mmoja wa wahunzi na watetezi wa itikadi hiyo hapa nchini Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere amewahi alitamka kama chama hicho kimeacha kifuata itikadi hiyo. Tatu; nikajenga hoja kwamba CCM na serikali yake inafuata mfumo wa soko holela lenye kujali zaidi maslahi ya wawekezaji toka nje, sera ambazo zina madhara kwa mwelekeo wa taifa na maisha ya wananchi wengi na si soko huria lenye sheria, kanuni na taratibu. Nne; nilieleza kwa lugha rahisi maana ya falsafa na itikadi. Tano; nilifafanua misingi ya falsafa ya nguvu ya umma na itikadi ya mrengo wa kati kama ambavyo inasimamiwa na CHADEMA na kuelezewa katika katiba yake. Sita; nilidokeza haja ya mjadala wa kitaifa kuhusu suala la falsafa na itikadi sambamba na mchakato wa kuandika katiba mpya ya nchi yetu. Saba; na kwa ujumla nilieleza umuhimu wa falsafa na itikadi kwa vyama vya siasa na kwa mustakabali wa taifa kwa ujumla.

Katika sehemu hii nilitaka kuanza kuchambua hatua kwa hatua njia ambayo taifa letu na vyama vya siasa vimepitia kifalsafa na kiitikadi kuanzia wakati wa Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere mpaka wakati huu wa Rais wa awamu ya nne Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Na hatimaye niweze kuchambua uhusiano baina ya falsafa, itikadi, sera na matukio mbalimbali yaliyotokea na yanayoendelea katika taifa letu. Kwa lugha rahisi, ningejibu swali - nini uhusiano baina ya falsafa na itikadi na maisha ya kila siku ya mwananchi? Lakini kutokana na hoja zilizoibuliwa na makala zingine za Toleo hilo hilo la Rai namba 713 na kwa sababu ya  maswali ambayo wasomaji wa gazeti hili wameyaelekeza kwangu, kutokana na makala yangu iliyopita -nimeona ni vyema nikaahirisha mtiririko huo nilioudokeza na nitaanza kuutoa katika makala yangu ya tatu kuhusu suala hili. Leo nitajikita katika hoja na haja za wiki iliyopita.

Msomaji mmoja ameniuliza hivi ni nini hasa tofauti kati ya falsafa na itikadi? Nilisema falsafa ni fikra au mtazamo wakati itikadi ni imani. Ukitaka kujua tofauti kirahisi chukua mwili wa mwadamu. Falsafa ni akili; ni kama kichwa kinachochea kufikiri na kufahamu. Wakati itikadi ni kama roho au moyo; ambao unabeba kuamini na hisia!

Mwingine aliyejitambulisha kama Wakili anayefanya kazi Arusha yeye alisema tusipoteze muda kujadili falsafa na itikadi; tuelekeze nguvu zetu kujadili masuala ya msingi yanayolikabili Taifa letu. Alisema kwamba hata Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini aliyasema haya alipotembelea nchini kwetu hivi karibuni kwamba matatizo yetu ni kutonufaika na rasilimali za nchi yetu na mzigo wa matumizi makubwa ya serikali. Na kwamba badala ya kuweka mkazo katika kuchambua falsafa na itikadi; vyama vya upinzani vielekeze nguvu katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na mfumo huru wa uchaguzi ikiwemo kupinga utaratibu wa maofisa wa serikali kutumika kama wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi za majimbo na kata. Nimeuchukua ushauri wake! Hata hivyo, Swali la kujiuliza; ni nini kinachoongoza fikra na imani yetu katika kuyafikia haya? Ni sera zipi; mikakati ipi; hatua zipi; zimetokana na nini? Hapa; mjadala kuhusu falsafa na itikadi bado hauepukiki. Nitajadili kidogo baadaye!

Mwananchi mmoja wa Morogoro yeye alisema “Mtibwa inawatesa wastaafu na wakulima kwa maslahi ya watawala. Kampuni hii haina uwezo wa kifedha na kimenejimenti. Tusaidieni bungeni na serikalini. Viongozi wa wakuu wa vyama waje Turiani watutetee. Watanzania tumekwisha; miezi mitatu tunazungushwa mishahara yetu”. Naamini ujumbe huu utakuwa umefika kwa wahusika na watafuatilia suala hili kujua ukweli wa mambo na kutafuta suluhisho. Lakini kwanini hali hii inatokea sasa? nitajadili pia kidogo baadaye!

Halafu nikapitia makala ya Muhingo Rweyemamu; “Niache Nizungumze kama mwendawazimu - II”. Yeye ameendeleza hoja zake za kutetea mtizamo wa mfumo wa utamaduni wa umaskini (cultural explanation of poverty) katika kuelezea asili na njia ya watanzania kuondokana na ufukara. Amejenga hoja kwamba tatizo la msingi la watanzania ni kuwa hawajiamini na hawatumii ubungo wao vizuri kubuni shughuli za kimaendeleo; ametumia sana mfano wa kompyuta inavyofanya kazi. Suala ni ‘fikra’ na ‘imani’; tunarudi pale pale kwenye mjadala wa falsafa na itikadi. Lakini kuna pahala sikutegemea pale alipoandika “Mimi (yeye muhingo) ni mkazi wa Mbezi, nitakosea kama nikisema Mbunge wangu wa Jimbo la Ubungo, amewahi kuchangia chochote katika maendeleo yangu. Hata asipokuwepo Keenja kama mbunge mimi sina tatizo. Na wakazi wengi wa eneo letu nimewahi kuwasikia wakisema hivyo. Vivyo hivyo kwa diwani. Naweza kuishi bila diwani na mbunge na nisipungukiwe na chochote. Nadhani sehemu kubwa ya watanzania, hawahitaji mbunge wala diwani”, mwisho wa kunukuu. Na aendelea mbele kusema kwamba tunahitaji kuwaheshimu viongozi wetu kikatiba; lakini hatustahili kuwatilia maanani kama washirika wakubwa wa maendeleo yetu! Maneno haya, ni gesi ya kuwasha mjadala mwingine mpana wa falsafa na itikadi. Nitayajadili kidogo baadaye!

Halafu nikasoma makala ya mchambuzi Prince Bagenda, iliyopewa kichwa “Mbowe: Tafakuri au malalamiko?”; yeye amezungumzia kwa ujumla suala la ahadi za viongozi wakati wa uchaguzi na dhana ya uwajibikaji. Katika uchambuzi wake ametoa hoja kadhaa ambazo nakubaliana nazo. Lakini ametoa pia hoja nyingi ambazo zinaturejesha tena kwenye mjadala wa falsafa na itikadi! Hoja za Bagenda zifuatazo zinahitaji mjadala. Mosi; si kila ahadi ambazo viongozi wanazitoa kwenye kampeni ndizo ambazo wananchi wanazitaka! Pili; ahadi zinazotolewa na viongozi lazima zifuatiliwe na wale ambao watafaidika nazo! Tatu; mambo yanayoelezwa kwenye kampeni hayawezi kuwa yale ambayo yataelezwa na kurejewa katika vikao vya kutunga sera na sheria! Nne; watu hawakati tamaa kwa sababu ya ahadi zilizotolewa wakati wa uchaguzi hazijatekelezwa. Watu hukata tamaa wakigundua kuwa serikali waliyoichagua haiwajali na imewatelekeza. Tano; masuala ambayo Mbowe anayazungumzia na masuala anayomuuliza Rais Kikwete mengi yametokana na uchaguzi na hivyo anayazungumza kuondoa dukuduku moyoni. Sita; Mbowe anashida ya nani amuulize ahadi zilizotolewa nchi nzima na hivyo ni lazima kujiuliza ni kwa mfumo gani ahadi hizo zitatekelezwa. Saba; Vilevile kuelekeza kila tatizo kwa Rais ni kumtwisha mzigo bila sababu, maswali fulani yanaweza kuelekezwa kwa wakuu wa idara nyingine ama kwa mawaziri kipindi cha maswali bungeni. Nane; kuna ufa mkubwa kati ya viongozi na wanachama wao pale ambapo viongozi hao wa vyama wanataka waonekane kama wanafanyakazi ya kupambana na serikali na chama tawala! Hizo hoja za Bagenda alizoziandika katika makala yake ya wiki iliyopita; ambazo zinaibua zaidi mjadala wa kifalsafa na kiitikadi.

Naanza kujadili!  “Tanzania, CCM, CHADEMA na mjadala wa falsafa na itikadi; lipi ni jibu?” katika muktadha wa haja na hoja nilizozianisha hapo juu kwa ujumla. Nitazijadili zaidi kwa kuzingatia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ (people’s power) na itikadi ya ‘mrengo wa kati’. Nitachambua pia katika muktadha wa itikadi ya ‘ujamaa na kujitegemea’ pale itakapokuwa muhimu.

Nikumbishe kidogo tu! kwamba falsafa ya CHADEMA ni kuamini katika “nguvu na Mamlaka ya Umma” (People’s Power) katika kumiliki, kuendesha, kubuni na kuendeleza mawazo, raslimali, uchumi na siasa za nchi. Aidha, falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma ndiyo msingi na chimbuko la kuundwa kwa dola ya nchi na kuwa umma ndio wenye madaraka ya mwanzo na mwisho katika kuamua hatma ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni....hivyo basi, falsafa ya “nguvu na mamlaka ya Umma” ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vinavyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na haki.

Nikumbushe kidogo pia! Kwamba CHADEMA ni chama cha mrengo wa kati kwa mujibu wa madhumuni yake na sera zake. Mathalani, ukipitia madhumuni ya kiuchumi ya CHADEMA, utabaini kuwa ni chama kinachoamini kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia raslimali za nchi yetu bila kuathiri uhuru wa Taifa, na kuhakikisha kuwa umma kwa ujumla unanufaika na raslimali zao. CHADEMA inaamini katika kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru ama soko la kijamii, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za watu, biashara huru na sekta ya watu binafsi bila kupoka mamlaka ya umma katika maeneo nyeti. Tunaamini katika soko huru sio soko holela. CHADEMA inaamini kuhakikisha matumizi bora ya raslimali asilia za nchi ili zichangie kikamilifu katika pato la taifa na hasa kuboresha huduma za kiuchumi zinazotumiwa na wananchi wote. Pia CHADEMA kinayo misingi muhimu katika sera na ajenda zake inayokiweka chama katika Mrengo wa Kati. Tunaamini katika siasa ambazo ziko juu ya vyama zenye kusimamia zaidi maslahi ya Taifa. Tunaamini katika umuhimu wa dini katika kujenga maadili ya mwanajamii mmoja mmoja bila kuifanya dini kuwa sehemu ya dola. Tunaamini kumiliki raslimali na mali miongoni mwa wananchi kunawapa uhuru zaidi hivyo tunataka kujenga chama na baadaye taifa lenye kutoa fursa, ambapo kila mtu bila kujali asili na hali yake anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake.

Sasa naendelea kujadili! Kwako wakili wa Arusha; tukikubali kufuata falsafa ya “nguvu ya umma”, tutaweza kuwawajibisha viongozi wetu kuweka sera zitakazohakikisha watanzania wananufaika na maliasili za nchi yetu kuliko wageni. Kama tutafuata itikadi ya mrengo wa kati tutaepukana na mzigo wa kuwa na serikali kubwa ambayo ni mzigo kwa walipa kodi. Tofauti na muundo wa kiserikali ya kijamaa ambao serikali kuu inakuwa pana yenye mikono kila mahali na kuwa mzigo kwa wananchi. Kama tutafuata itikadi ya mrengo wa kati tutahimiza dini na maadili ya taifa na hivyo kukabiliana na rushwa, ufisadi na matumizi ya anasa. Hivyo ndivyo tunavyoweza kuitikia changamoto ya Rais Mbeki. Kuhusu tume ya uchaguzi; ni suala wananchi kwa nguvu ya umma kudai katiba mpya kwa kuwa chini ya falsafa hii katiba ni mali yao; si mali ya si serikali ama kikundi kidogo cha watawala! Kama alivyosema Mahatma Ghandi; kila mwananchi anapaswa kuwa wakala wa mabadiliko anayotaka kuyaona; jiulize, wewe umefanya nini kuchangia mageuzi ya mfumo wa uchaguzi ili uwe huru na haki?

Kwako Mwananchi wa Turiani Morogoro; pole sana! hayo ndiyo madhara ya mfumo wa soko holela; ambapo haki za wafanyakazi huwa chini ya maslahi ya waoitwa wawekezeji. Na pale wawekezaji hawa wanapokuwa sehemu ya tabaka la mabepari uchwara wa ndani ama pale ubinafsishaji unapoambatana na ‘takrima’ ya asilimia kumi; hali huwa mbaya zaidi. Amka sasa! Falsafa ni nguvu ya umma. Ungana. Teteeni haki zenu. Hakuna cha kupoteza zaidi ya shida zenu. Nawe mwekezaji! Ewe serikali! Enyi viongozi wa vyama vya siasa. Kumbukeni itikadi ya mrengo wa kati. Hakikisheni kampuni zinaendeshwa chini ya mifumo ya soko la kijamii, unaoheshimu na kulinda haki na mali za watu. Haya ndiyo maeneo nyeti dola inapaswa kuingilia kati kwa kusimamia sheria zinazolinda maslahi ya wafanyakazi. Faraja yangu ni kuwa uliberali mamboleo (neo liberalism); huu mfumo wa soko holela bado haujatamalaki moja kwa moja katika nchi yetu. Tunayo nafasi ya mwisho ya kujinasua kabla hatujachelewa. Sehemu kubwa ya sera hizi bado zinasimamiwa na nchi wahisani; zinategemea ufadhili na uwekezaji  wao na hivyo hazina uendelevu! Tuanze kuzibadili sasa kabla hazijaota mizizi. Sera hizi; bado hazina hamasa ya umma; ni misamiati ya viongozi na watawala. Hazina mtaji wala msingi wa kijamii. Zinakumbatiwa na tabaka la watu wachache; ambao wameanza kujitenga mbali na tabaka la chini la walio wengi. Hawa wameshakata tamaa ya kukubalika na umma. Badala yake yake wanatafuta mamlaka toka kwa wahisani na mashirika ya kimataifa. Ndio maana ushahidi wao wa mafanikio ya sera hizi ni sifa toka kwa benki ya dunia na mashirika ya kimataifa. Kasi ya kukua kwao kwa uchumi haifahamiki na mwananchi wa kawaida lakini unajulikana na mataifa ya nje! Kama hayati Profesa Chachage angakuwepo hakika angewaita hawa “makuwadi wa soko holela” na si “Makuwadi wa soko huria”. Falsafa na itikadi ‘holela holela’ tayari zimeanza kulipua moto huko bara ya Amerika ya Kusini. Ona Hugo Chavezi kule Venezuela; angalia jirani zake Argentina; tazama kule Bolivia; fuatilia kule Chile! Hisia za utaifa zinaibuka. Tanzania hatujachelewa. Turudi kwenye “nguvu ya umma” sasa! Ama sivyo yatatukuta ya Amerika Kusini. Na tukifika huko wa kupoteza ni wote- wananchi na hata makampuni ya kibepari. Lazima tukifikiri ‘shinda-shinda’ (win-win). Turudi katikati; kwenye ‘mrengo wa kati’. Tutangulize mbele maslahi ya afrika (Pan Africanism). Yaliyotokea kwenye eneo la Madini Msalala; yanayotokea kwa wahadzabe; ni alama za nyakati. Tukichelewa; tutakuja kujuta.

Kwako Kaka yangu Muhingo Rweymamu: Hii ni hekaya ya kuku na yai! Kipi kimeanza? Ambayo mara nyingine hutufikisha kusema tu kwamba vyote vinategemeana. Umejenga hoja kwamba umaskini wetu ni sababu ya utamaduni wetu! Kwamba watanzania wengi ni maskini kwa sababu ni wategemezi kifikra na kimatendo. Umepingana kabisa na nadharia ya kwamba umaskini wetu umetokana na mfumo wa maisha (structural explanation of poverty). Naomba kutofautiana nawe! Na hata nikiamua kukubaliana nawe! Nini chanzo cha utamaduni huu? Sio itikadi ya ujamaa ya dola kufanya mpaka uzalishaji na hivyo kuondoa jitihada za mwananchi mmoja mmoja kujitegemea? Nyerere alijaribu sana kulifanya taifa letu lijitegemee (kwa maana ya dola) na kusahau kuweka mkazo kwamba taifa ni watu- ili taifa lijitegemee lazima watu wake mmoja mmoja wajitegemee! Hapa ndipo tunapopaswa kukubaliana kwamba tunahitaji falsafa ya ‘nguvu ya umma’; mfumo wetu wa elimu; karakana yetu ya fikra - itufikishe huko. Na zaidi tunahitaji itikadi ya mrengo wa kati - ili tuwe na sera ambazo zitawezesha kuwa taifa lenye kutoa fursa, ambapo kila mtu bila kujali asili na hali yake anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake! Mkulima anayelima kule kijijini anufaike na kilimo chake; msanii wa bongofleva anufaike na sauti yake; mcheza mpira aneemeke kwa miguu yake; yule mwalimu naye chaki yake imkomboe; yule polisi afanikiwe huku akiendelea kuwalinda raia. Kila mbuzi ale urefu wa kamba yake - kwa maana ya asili ya nahau hii; na si tafsiri ya mfumo wa soko holela yenye kuhimiza kila mtu ale rushwa katika sehemu yake ya kazi! Ni kweli hatuhitaji viongozi? Kama hatuhitaji mbunge wala diwani kwanini tuendelee kuwa nao wakitumia fedha zetu za kodi? Kwa nini tusitumie falsafa ya nguvu ya umma kuwawajibisha kama hawatimizi wajibu wao? Wewe ni mkazi wa jimbo la Ubungo; mimi nami ni mkazi wa jimbo hilo hilo; zaidi utakumbuka nilikuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo! Naelewa kwamba wananchi wamekata tamaa na baadhi ya wawakilishi (na si jambo zuri) lakini sikubaliani nawe kwamba hawajui manufaa ya kuwa wawakilishi bora. Huwezi kusema kwamba wananchi wa kwako Mbezi maeneo ya Makabe; Matosa; Malambamawili; Msuguri ambao wengine hulazimika kujazana kama mizigo kwenye landrover ama kutembea umbali mrefu kwenda majumbani mwao wakati ambapo wako jiji kubwa la nchi; eti hawahitaji mtu wa kuwakilisha kero zao. Ama wale wenye shida ya maji wakati Wizara ya Maji na Chuo cha Maji vyote viko Ubungo; mabomba makuu yanayohudumia mkoa wa Dar es salaam, yanapita hapo hapo jimboni kwao Ubungo; nao hawahitaji wawakilishi? Ama wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walioko Ubungo nao hawahitaji wabunge wa majimbo yao kwenda kutetea bajeti ya wizara ya elimu ya juu ili waondokane na sera ya soko holela ya kuchangisha hata watoto wa masikini? Tukifika pa kukatishwa tamaa na viongozi mpaka tukaomba wasiwepo tutaacha kabisa demokrasia ambayo ni utawala wa watu na kuingia katika mfumo wa sheria za mwitu (law of the jungle) ama uanaki (anarchism) ambavyo vyote viwili ni hatari kwa usalama wa taifa!

Kwako Komredi Bagenda; Mosi, viongozi wakitoa ahadi ambazo wananchi hawakuzitaka ni ishara ya kutofahamu mahitaji ya jamii ama kutofanya utafiti. Tiba ni kuzingatia falsafa ya nguvu ya umma. Sauti ya watu ni sauti ya Mungu! Pili; ni muhimu kwa wananchi kufuatilia ahadi chini ya falsafa ya nguvu ya umma ambayo inataka wananchi kuwawajibisha viongozi wao; lakini chini ya falsafa hii hii viongozi wanapaswa kuwajibika kwa umma kwa kutekekeza walichoahidi. Kwani aja ya mja hunena; muungwana na vitendo! Tatu; sayansi ya ilani za uchaguzi wa kisiasa inasema kwamba ilani ni mkataba kati ya wapiga kura na watawala; hivyo lazima vikao vya kutunga sera na sheria lazima virejee yaliyoelezwa kwenye kampeni. Ukitaka kuruka lazima uagane na nyonga! Nne; watu wanakata tamaa ahadi zisipotekelezwa kwa kuwa wengi huitafsiri kama ni ishara ya serikali waliyoichagua kutowajali na kuwatelekeza. Kumbuka; ahadi ni deni! Tano; si vibaya kwa yoyote kuzungumza kwa kuondoa dukuduku kama dukuduku linawahusu walio wengi lakini la ziada ni kuwa katika makala yake Mbowe hakuzungumza ya wakati wa uchaguzi tu kwa kiasi kikubwa aliifanyia tathmini ya utekelezaji hotuba ya Rais ya Kikwete ya Disemba 30, 2005 akifungua bunge mara baada ya uchaguzi ambao ki msingi ndio ulikuwa mkataba wa serikali ya awamu na nne na watanzania wote ikiwemo mimi na wewe. Kwa hiyo si Mbowe tu; hata mimi na wewe tuna haki ya kuhoji na pia kumsaidia Rais kufanikisha azma ya serikali yake. Hatuwezi kuachia Rais wetu peke yake aelemewe na mzigo wa utawala. Ndiyo falsafa ya nguvu ya umma katika vitendo! Sita; Mbowe anamuuliza rais kwa kuwa ahadi hizi zilitolewa sehemu mbalimbali na yeye kwa hiyo kwa vyovyote vile; kwa vile aliahidi ni wazi kuwa anajua kwamba serikali yake imeweka mikakati gani ya kuzitekeleza. Kama haujawekwa bado; basi ni ishara ya wazi kwamba Tanzania inahitaji mabadiliko ya mfumo wa utawala unaozingatia nguvu ya umma. Hii ni pamoja na kutekeleza sera ya mfumo mpya wa utawala (maarufu kama sera ya majimbo) yenye kuhakikisha viongozi katika maeneo yao wanakuwa na mamlaka ya kutekeleza ahadi zilizolenga katika maeneo yao na kuwajibika kwa wananchi moja kwa moja! Saba; kuelekeza tatizo kwa Rais si jambo baya kama suala hilo limetokana na kauli yake yeye mwenyewe; ni wajibu wa wakuu wa idara na hata mawaziri Bungeni kufafanua mambo yote ambayo yalielekezwa kwa Rais lakini yanawahusu wao zaidi. Kwani watendaji wa idara na wizara wanalipwa kwa kodi za wananchi kufanya nini kama si kuwajibika kwa umma? Hii ndio falsafa ya nguvu ya umma. Nane; hapawezi kuwa na ufa kati ya wanachama na viongozi wao kama viongozi wa vyama wanazungumza hisia za wanachama hao na wananchi kwa ujumla. Dhima ya chama cha upinzani si kupambana na chama tawala bali ni kuwajibisha serikali iliyoko madarakani (check and balances). Huku ni kuweka falsafa ya nguvu ya umma katika vitendo. Kazi ya vyama vya upinzani ni kutoa fikra mbadala! Na matokeo ya fikra na uwajibakaji ni matokeo ni ufanisi wa serikali iliyoko madarakani na manufaa kwa taifa kwa ujumla.  Na athari ya kutosikiliza sauti hizi za pembezoni ni kuhukumiwa katika mahakama ya umma wakati wa upigaji kura katika uchaguzi ujao. Na huu ndio msingi wa itikadi ya mrengo wa kati kwamba: tunaamini katika siasa ambazo ziko juu ya vyama zenye kusimamia zaidi maslahi ya Taifa.

Nawasilisha hoja hizi kuendeleza mjadala tuendelee kujiuliza - Tanzania, CCM, CHADEMA na mjadala wa falsafa na itikadi; lipi ni jibu?


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl