Mjadala kuhusu falsafa na itikadi umeibuka tena rasmi. Nimesoma mahojiano ya mwanasiasa kijana David Kafulila akizungumzia CHADEMA ni Msingi na makala ya mchambuzi mahiri aliyoyapa kichwa “Itikadi ya Mrengo wa Kati si jibu. Nimesoma pia makala ya Mwenyekiti wangu-Freeman Mbowe kuhusu suala hili. Ni dhahiri mjadala umefumuka rasmi. Suala la falsafa na itikadi si la wanasiasa na vyama tu, ni suala la kitaifa; tulijadili. Katika makala yake Prince Bagenda kimsingi, amebeza itikadi ya mrengo wa kati. Si lengo la sehemu hii ya kwanza kujibu hoja kwa hoja uchambuzi wa Bagenda kuhusu mrengo wa kati. Lengo la makala ya leo ni kueleza ni nini hasa itikadi ya mrengo wa kati. Katika makala yake Freeman Mbowe amebainisha hoja mbili kubwa- Mosi, kwamba CCM haifuati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa vitendo kama inavyotangaza kwa maneno na nyaraka zake (kwa maneno mengine CCM inakiuka katiba ya nchi). Pili; kwamba kitendo cha serikali ya CCM kuweka kwenye katiba ya nchi kwamba Tanzania ni nchi ya itikadi ya siasa na ujamaa na kujitegemea ni kinyume na dhana ya demokrasia ya vyama vingi ambayo inataka uhuru wa fikra na kiitikadi. Nitachangia kwa kiasi hoja hizi (kwa maana nyingine vyama vyenye itikadi tofauti na ujamaa na kujitegemea vinakiuka katiba ya nchi). Nitajadili!
Kwa tafsiri rahisi, falsafa ni fikra na mtazamo wakati itikadi ni imani. Maneno haya mawili ni muhimu sana katika medani ya siasa na maendeleo kwa ujumla. Nimewahi kupitia katiba za vyama mbalimbali vya siasa nchini, nimewahi kupitia Azimio la Arusha, nimewahi kusoma maamuzi ya Zanzibar (ambayo wengi huyaita Azimio la Arusha) na ninayo kama rejea ya msingi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukipitia nyaraka zote hizi utaona kwamba mjadala kuhusu falsafa na itikadi ni suala lisiloepukika.
Mwaka 1991 Mwenyekiti wa CCM wa wakati huo, Ali Hassani Mwinyi wakati huo alijitokeza na kutoa hotuba ndefu akitetea maamuzi ya Zanzibar na kusisitiza kwamba CCM inafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea, namnukuu: “ Inaelekea kuna hofu kwamba Azimio la Arusha linageuzwa. Kwa hiyo, tokea mwanzao, kabla ya kusema lolote, nataka tuelewane kwamba siasa yetu bado ni ile ile ya Ujamaa na Kujitegemea. (Makofi). Haikugeuka wala hatutazamii kuigeuza. Kwa hali yoyote sisi Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi hatutaigeuza Siasa hii. (Makofi) . Kule Zanzibar tulizungumza mambo mengi, miongoni mwao, ni kutoa tafsiri ya baadhi ya vipengele vya Azimio ili vifanane na wakati tulionao.”
Lakini miaka kadhaa baadaye, Muasisi na Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitamka wazi kwamba CCM haifuati siasa ya ujamaa na kujitegemea, nikinukuu kitabu chake cha uongozi wetu na hatma ya Tanzania : Halmashauri Kuu ya Taifa iliketi Unguja ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi. Na walikuwa na haki ya kufanya hivyo, maana sera ni yao, ubaya wao ni kwamba jambo lenyewe walilifanya kwa hila na hadi sasa wanaendelea kuwadanganya wananchi kwamba sera ya CCM bado ni Ujamaa na Kujitegemea.’ Haya ni maneno ya kiongozi ambaye alishiriki moja kwa moja kuandika Azimio la Arusha na misingi ya siasa ya ujamaa na kujitegemea! Mwaka 2000, mwaka mmoja tu baada ya baba wa Taifa kufariki, serikali ikapeleka bungeni mabadiliko ya Katiba na kuweka tafsiri finyu ya ujamaa na kujitegemea! Mwaka 2006, Agrey Mwanri-Mbunge wa CCM akichangia katika Bunge la Kwanza la Bajeti alijenga hoja nzito kwamba nchi hii haina itikadi, kinachoendelea hapa ni shughuli tupu. Mwaka 2007, Agrey Mwanri huyo huyo, baada ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alijenga hoja kinzani wakati wa kuchangia mjadala kuhusu muswada wa rushwa; kwamba nchi yetu bado inafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea. Na kwamba bila siasa hii; mustakabali wa taifa utakuwa mashakani. Hapa ndipo tulipofika! Je, mustakabali wetu hauko shakani?
Kauli hizi zinahitaji kujadiliwa. Inaweza kuonekana hili ni suala dogo. Lakini hilo ndio chanzo ya matatizo ya watanzania. CCM inafuata sera ya Ubepari uliokubuhu na mfumo wa soko holela. Ndio maana leo wageni na wawekezaji kutoka nje wanapewa kipaumbele zaidi. Ukuaji wa uchumi unawanufaisha wachache na matabaka katika jamii yanazidi kuongezeka, Uzalishaji umepungua na tumegeuzwa wachuuzi wa bidhaa toka nje.Kwa upande mwingine mzigo wa huduma za kijamii katika sekta za elimu na afya unazidi kuwa mzigo kwa watanzania maskini.Chama tawala kinapokosa itikadi maana yake kimekosa dira. Chama kinapokosa itikadi yake hakiwezi kuandaa sera na kutoa mwelekeo wa Taifa!
Niweke pia bayana kwamba ujamaa ni neno tamu; ni tamu linapobeba dhana ya undugu na usawa. Lakini inapochukua sura ya dola kufanya uzalishaji wa moja kwa moja hapa hupoteza maana. Kujitegemea ni suala zuri. Hasa linapotekelezwa kwa vitendo bila kuegemea wahisani. Hata hivyo maneno haya yanapotumiwa hivyo sivyo na vyama visivyo na dira wala mwelekeo dhana hizi zinapoteza dhima na maana yake!
Bagenda amejenga hoja kwamba vyama vya upinzani nchini vinaiga itikadi za kimagharibi na ameshambulia moja kwa moja itikadi ya CHADEMA ya Mrengo wa kati. Anasahau kwamba CHADEMA ni chama hakijatoka nchi ya misingi yake ya asili. Wakati wa mabadiliko ya Katiba ya CHADEMA mwaka 2006, ambayo yalihusisha mchakato wa kutuma timu za kukusanya maoni ya wanachama toka ngazi ya wilaya, nilikuwa mjumbe katika kamati ya itikadi. Kamati hii iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mwesiga Baregu-Profesa wa siasa na mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA. Kamati hii iliratibu mchakato wa kuweka bayana itikadi ya chama katika katiba. Hapo nyuma tulisema CHADEMA inaamini katika falsafa na itikadi ya nguvu na mamlaka ya umma. Sasa tumeamua kuweka bayana falsafa yetu na itikadi yetu. CHADEMA tunaendelea kuwa na falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma. Huu ni msimamo wetu wa asili: Kwamba falsafa ya CHADEMA ni kuamini katika “nguvu na Mamlaka ya Umma”(People’s Power) katika kumiliki, kuendesha, kubuni na kuendeleza mawazo, raslimali, uchumi na siasa za nchi. Aidha, falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma ndiyo msingi na chimbuko la kuundwa kwa dola ya nchi na kuwa umma ndio wenye madaraka ya mwanzo na mwisho katika kuamua hatma ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni....hivyo basi, falsafa ya “nguvu na mamlaka ya Umma” ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vinavyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na haki. Hii ni falsafa tuliyokuwa nayo ambayo tunaiendeleza.
Kwa upande mwingine tulipitia madhumuni ya kuanzishwa kwa CHADEMA pamoja na sera za chama. Tumejitafakari kiitikadi na kuona tutamke bayana katika katiba yetu tuko wapi. Mkutano mkuu uliamua kwa kauli moja kwamba CHADEMA ni chama cha itikadi ya MRENGO WA KATI(center party). Kwangu mimi itikadi ni imani. Ni imani inayotuunganisha. Ni imani inayotuongoza. Ni imani inayotuelekeza. Ni imani tunayoielekea. Dhana ya “Mrengo wa kati” pengine itaeleweka vyema kama nitasimulia kisa cha dola moja ya kifalme kama ifuatavyo.
“Katika ufalme huo palikuwa na baraza ambalo lilikuwa na wajumbe wa makundi matatu. Kundi moja lilikuwa upande wa kulia: Hili lilikuwa ni kundi la watawala, wakati wote lilitetea utawala, nidhamu ya kijamii na maslahi ya watu binafsi. Kundi la pili lilikaa upande wa kushoto: Hili lilikuwa likitetea umuhimu wa dola kuhudumia wananchi ikiwemo umiliki wa pamoja wa njia zote za uzalishaji mali na kuweka mkazo katika haki za matabaka. Kundi la tatu lilikaa katikati: Hili lilikuwa likitetea umuhimu zaidi wa dola kuwawezesha wananchi, likiweka mkazo katika uhuru na uwezekano wa kuboresha maisha ya mwanadamu na jamii. Kundi hili la tatu ndio asili ya itikadi ya mrengo wa kati.
CHADEMA ni chama cha mrengo wa kati kwa mujibu wa madhumuni yake na sera zake. Mathalani, ukipitia madhumuni ya kiuchumi ya CHADEMA, utabaini kuwa ni chama kinachoamini kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia raslimali za nchi yetu bila kuathiri uhuru wa Taifa, na kuhakikisha kuwa umma kwa ujumla unanufaika na raslimali zao. CHADEMA inaamini katika kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru ama soko la kijamii, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za watu, biashara huru na sekta ya watu binafsi bila kupoka mamlaka ya umma katika maeneo nyeti. Tunaamini katika soko huru sio soko holela. CHADEMA inaamini kuhakikisha matumizi bora ya raslimali asilia za nchi ili zichangie kikamilifu katika pato la taifa na hasa kuboresha huduma za kiuchumi zinazotumiwa na wananchi wote.
Pia CHADEMA kinayo misingi muhimu katika sera na ajenda zake inayokiweka chama katika Mrengo wa Kati. Tunaamini katika uzalendo na kuthamini mila na desturi zetu zilizo nzuri. Tunaamini katika uhuru chini ya sheria zilizo nzuri. Tunaamini katika siasa ambazo ziko juu ya vyama zenye kusimamia zaidi maslahi ya Taifa. Tunaamini katika umuhimu wa dini katika kujenga maadili ya mwanajamii mmoja mmoja bila kuifanya dini kuwa sehemu ya dola. Tunaamini taifa linaundwa na watu, hivyo uhai wake unawategemea watu, na mabadiliko yake yanatokana na watu. Tunaamini kumiliki raslimali na mali miongoni mwa wananchi kunawapa uhuru zaidi hivyo tunataka kujenga chama na baadaye taifa lenye kutoa fursa, ambapo kila mtu bila kujali asili na hali yake anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake. Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazofanya CHADEMA kuwa chama cha mrengo wa kati.
Hatahivyo, hatuamini kwamba itikadi ni suluhisho pekee la matatizo katika taifa. Tutaendelea na utamaduni wetu wa kuwa na itikadi laini (relaxed ideology) badala ya itikadi iliyojibana (restrictive ideology). Tutaendelea na msimamo wetu wa kutaka mabadiliko kwa vitendo (pragmatism). Hiyo ni imani, matumaini na mwelekeo wetu. Tunahitaji vyama viwe na falsafa na itikadi ili wananchi wachague ni chama gani kiwaongoze katika wakati gani. Lakini hatuhitaji itikadi ya chama kimoja ndio iwe itikadi ya taifa lote kikatiba. Ingawa tunahitaji mjadala wa kitaifa. Ili tuwe na misingi ambayo tutakubaliana kwa pamoja kama taifa katika katiba mpya, misingi hii kila chama kitaonyesha ubunifu na umahiri wa kuizingati, kuitafsiri na kuitekeleza kupitia falsafa, itikadi, sera na shughuli zake. Nawasilisha hoja hizi kuendeleza mjadala tujiulize- Tanzania, CCM, CHADEMA na mjadala wa falsafa na itikadi; lipi ni jibu?